Mo Dewji amleta straika Mghana Simba

BAADA ya kuwepo maneno mengi mtaani hasa vijiwe vya kahawa na hata mtandaoni bilionea wa klabu ya Simba, Mohamed ‘MO’ Dewji amejiweka pembeni, bilionea huyo ameamua kufanya kweli kwa kuwataka mabosi wa klabu hiyo kumleta haraka straika raia wa Ghana.
Ipo hivi. Mo Dewji alimvutia waya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ na kumwambia yeye, viongozi wengine na benchi la ufundi waingie sokoni kusaka mchezaji yeyote mkali wanayemtaka kikosini na fasta, Try Again alimwagiza Ofisa Mtendaji Mkuu anayemaliza muda wake, Barbara Gonzalez kuwasiliana na USM Alger ya Algeria ili kumalizana na Kwamem Opoku.
Straika huyo huyo Mghana ambaye Mwanaspoti liliwahi kukudokezea alikuwa kwenye rada za Simba, amesaliwa na mkataba wa mwaka mmoja na Simba inamtaka hata kwa mkopo ili aungane na kina Moses Phiri na kuliamsha kikosini kwa mechi za ligi ya ndani na ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika. 
Opoku kwa sasa anacheza kwa mkopo Najran ya Saudi Arabia na kama mazungumzo ya Barbara anayeiwakilisha Simba pamoja na wale wa klabu ya USM Alger yakienda vizuri, huenda akawa nyota wa kwanza kusajiliwa kupitia dirisha dogo. 
Barbara katika kuhakikisha anafanikiwa kupata saini ya Opoku inamtumia Wakala wa Nelson Okwa, anayekipiga Simba kwa sasa kutoka Nigeria, ili kuongeza nguvu na kuhakikisha mshambuliaji huyo mwenye uwezo wa kufunga anapatikana.
Baada ya kufanya mawasiliano na uongozi wa USM Alger, kwa sasa Simba inasubiri majibu kutoka kwa timu hiyo na kutakiwa pia kutoa kiasi gani cha pesa kama thamani ya usajili pamoja na masilahi mengine yakiwemo yale ya mchezaji binafsi.
Simba ikiwa inasubiri majibu ya kumpata Opoku, awali mpango wao wa kwanza ulikuwa kumnasa straika, Cecar Manzoki iliyesaini mkataba wa miaka miwili kabla ya msimu huu kuanza ila dili hilo linaweza kuwa gumu.
Kupatikana kwa Manzoki aliyekuwa chaguo la kwanza licha ya kuwa na mkataba wa miaka miwili na Simba limekuwa gumu kutokana na mchezaji huyo kuwa na zaidi ya asilimia 80, kuongezewa mkataba na timu ya Dalian Professional ya China wenye masilahi mazuri zaidi ya yale Simba iliyotaka kumpatia. Alipotafutwa Barbara alisema yupo njiani kwenda kuangalia fainali ya Kombe la Dunia, ila mara baada ya kurejea Dar es Salaam na kumaliza muda wake ofisini hapo, Simba itakuwa imefanya usajili.
Barbara alisema anataka kuondoka kwenye nafasi hiyo, huku Simba ikiwa imefanya usajili wa wachezaji wazuri kwa kuongeza nguvu kwenye maeneo machache kulingana na mapungufu yao ya mzunguko wa kwanza.
“Kabla ya kumaliza muda wangu kwenye hii nafasi usajili utakuwa umefungwa na miongoni mwa eneo ambalo tutaongeza wachezaji ni straika na hatutasajili mmoja bali tutaleta wapya wawili,” alisema Barbara na kuongeza;
“Tusubiri tu baada ya muda mfupi hilo ambalo nimeliweka wazi hapa kwa mara ya kwanza linakwenda kutimia, mbali ya washambuliaji wawili kuna maeneo mengine machache tutaongeza nguvu.”