Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Msiwe na presha tunafuzu Afcon- Morocco

Muktasari:

  • Taifa Stars imeshiriki fainali za Afcon mara tatu ambazo ni 1980, 2019 na 2023.

Dar es Salaam. Kocha mkuu wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Hemed Suleiman ametamba kuwa timu hiyo itafuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 zitakazofanyika Morocco.

Morocco alisema kuwa wachezaji walioitwa kwenye kikosi hicho, wameonyesha utayari na morali katika maandalizi ya mechi mbili zilizobakia za kuwania kufuzu Afcon dhidi ya Ethiopia na Guinea hivyo anaamini Watanzania watapata furaha.

“Muelekeo ni mzuri na kila mchezaji aliyeitwa katika kikosi cha sasa ana malengo ya kufanya vizuri. Kila mmoja anatamani kufanya kitu kizuri. Mimi naamini tunapiga hatua.

“Kila timu ina nafasi. Hata Ethiopia nao wana nafasi labda niweke wazi Tanzania hatujawahi kufuzu kirahisi. Kwa hivyo mimi sitaki kuangalia timu nyingine ziko vipi. Kitu cha msingi ni kuhakikisha sisi tunapigana kwa ajili ya kutafuta ushindi,” alisema Morocco.

Morocco alisema kuwa muda ambao wamepewa kujiandaa na mechi hizo japo haotoshi, wanahakikisha watautumia vyema ili wawe tayari kwa ajili ya michezo hiyo.

“Ukilinganisha siku za nyuma, sasa hivi ndio tumepata siku nyingi zaidi, siku tano. Hapo nyuma tulikuwa tunapata kama mbili hivi.

“Mimi nafikiri timu ya taifa iko vizuri, kuna kitu kinaendelea. Naamini tutaendelea kujisukuma kadri ambavyo inawezekana kuhakikisha tunafanikiwa,” alisema Morocco.

Taifa Stars inayoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi H, itakabiliana na Ethiopia, Novemba 16 jijini Kinshasa, DR Congo na Novemba 19 itakabiliana na Guinea hapa Dar es Salaam.

Kundi hilo linaongozwa na DR Congo ambayo tayari imeshakata tiketi ya kufuzu Afcon baada ya kukusanya pointi 12 na Guinea iko nafasi ya pili ikiwa na pointi sita, Taifa Stars iko nafasi ya tatu na pointi nne na inayoshika mkia ni Ethiopia iliyo na pointi moja.