Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Msuva alivyosimulia furaha ya bao la kihistoria

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' Simon Msuva

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’, Simon Msuva, amefichua kwamba moja ya nyakati za furaha zaidi katika maisha yake ya soka ni kufunga bao lililoisaidia Tanzania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zilizofanyika Morocco, akieleza kuwa mafanikio hayo yalikuwa ya kipekee kwa Watanzania wote.

Amesema hali ya shangwe iliyoonekana katika uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya ushindi huo ni jambo ambalo hawezi kulisahau kutokana na umuhimu wa mashindano hayo kwa taifa.

“NIlivyowafunga Guinea na tukafuzu AFCON, nafikiri ile furaha haikuwa peke yangu. Hata ukiangalia ule umati ilikuwa ni furaha ya Watanzania. Siwezi kusahau kwa sababu yale ni mashindano ambayo kila mtu anatamani kuingia," alisema Msuva.

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' Simon Msuva akiwa amebebwa nan nahodha wa timu hiyo Mbwana Samatta baada ya kufunga bao lililoipeleka Tanzania, AFCON 2025 Morocco.

Msuva alisema kufuzu AFCON ni ndoto ya kila mchezaji na taifa lolote la soka Afrika.

“Ukiangalia wakati tunawatoa Guinea, walikuwa na wachezaji wakubwa pale uwanjani. Walikuwa na mchezaji anacheza Dortmund na yule aliumia sana kushindwa kufuzu AFCON.

“Natokea ligi ya barani Asia. Kiuhaliisia mimi simfikii kwa hatua kubwa aliyopo lakini furaha yangu ni lile bao nililofunga ambalo kwangu mimi ni furaha kubwa kwa sababu niliona kwamba nimeibeba Tanzania na wachezaji wenzangu,” alisema Msuva.

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' Simon Msuva wakati alipokuwa na Wydad Casablanca ya Morocco.


Wakati mgumu aliopitia

Hata hivyo, nyota huyo alisema moja ya nyakati ngumu zaidi katika maisha yake ya soka ni kipindi alichokaa nje ya uwanja kwa miezi sita kufuatia mgogoro wa kimkataba na klabu yake ya zamani uliomlazimu kuwasilisha kesi katika Shirikisho la Soka la Duniani (FIFA).

Amesema kipindi hicho kilimletea changamoto kubwa kwani baadhi ya watu walimchukulia kama hana nidhamu bila kufahamu ukweli wa kilichokuwa kinaendelea.

“Nilivyokuwa Wydad nikakaa nje kwa miezi sita. Ule wakati ndio siwezi kuusahau kwa sababu ilinifanya nionekane sina nidhamu wakati mimi ndio nilikuwa sahihi na wao hawakuwa sahihi.

“Nakumbuka kipindi kile timu ilikuwa kwenye mashindano makubwa ya Ligi ya Mabingwa Afrika na walikuwa wamebakiza michezo michache kuingia katika fainali. Lakini nilijitoa nikarudi nyumbani ili niweze kupambania fedha yangu na mwisho wa siku nilipoenda FIFA hatimaye walinilipa haki yangu. Na hiyo ndio changamoto ambayo siwezi kuisahau,” alisema huku akisisitiza kuwa uzoefu huo ulimfundisha umuhimu wa kusimamia haki zake.

Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said (katikati), kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi (kulia), wakiwa pamoja na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo Simon Msuva (kushoto)


Akoshwa na Hersi

Msuva amesema kwamba Rais wa Yanga, Hersi Said ni mtu wake wa karibu lakini amekuwa akiongea pia hata na viongozi wengine wa mpira kutoka timu nyingine.

“Si yeye tu nayezungumza naye. Viongozi wengi nakutanana nao hata viongozi wa Simba na Azam huwa naongea nao.

“Hersi pia ni mtu wangu wa karibu napenda kile anachokifanya. Anakuwa anajichanganya, anaongea na watu. Hii yote ni kutokana na kuwa watu wanapenda kumuona na kusikia nini anazungumza, alisema Msuva.

Mshambuliaji huyo wa Al Talaba ya Iraq alisisitiza kwamba anapenda kuwa karibu na watu akieleza kuwa hapendi kuonyesha dharau kwa watu kwa sababu ya jina au sehemu aliyopo.

“Jamii yetu hii iliyotuzunguka ndio imetufanya kuwa hapa. Usidharau ulipotoka au watu kwa sababu tayari umeshapata jina au upo kwenye nafasi fulani kwani kuna kesho. Hatujui yule uliyemuacha mtaani atakuwa sehemu gni. Tuishi kwa upendo hatuijui kesho yetu,” alisisitiza.

Mshambuliaji wa Tanzania, Simon Msuva wakati alipokuwa na Klabu yake ya Al Talaba ya Iraq


Maisha ya Uarabuni

Msuva alisema anapokuwa katika mazingira ya Uarabuni ambako amecheza kwa muda mrefu, lugha ya Kiarabu ndio hutumika zaidi katika mazungumzo na ndio sababu iliyomfanya ajitahidi kujua lugha hiyo.

“Kiarabu sikijui kabisa kama navyojua kiswahili kwa hiyo huwa nakisikia na kujua mtu anaongea nini na ana maanisha nini na mimi nachoweza kujibu najibu“ alisema.

Kuhusu chakula, Msuva anasema ilimlazimu kuzoea kwa sababu tayari anakuwa yupo kwenye mazingira mengine.

“Chakula nimeshazoea kwa sababu nimeshafika kwenye nchi ya watu hakuna namna ilibidi nizoee tu. Ukikutana na chakula ambacho sio sawa na cha kwenu lakini utakula tu.

“Vyakula kama wali, nyama na viazi huwa wanavipika kama sisi lakini utofauti ni ladha ya kwao na ya kwetu inatofautiana kidogo,” alisema Msuva.

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' Simon Msuva


Ukaribu na nyumba za ibada

Msuva alieleza kuwa anapenda sana kuacha alama kwenye nyumba za dini, sehemu ambayo aliitaja kuwa ya muhimu sana katika maisha yake.

“Najitahidi sana kutoa misaada kanisani hata wazazi wangu tunashirikiana sana. Sijawahi kujenga Msikiti lakini huwa mara nyingi ikitokea msaada wowote huwa nachangia pia," alisema Msuva.


Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' Simon Msuva


Maisha baada ya soka

Hata hivyo, Msuva hakuweka wazi kuwa akimaliza kucheza mpira anataka kuwa na shughuli gani lakini nyota huyo alisema ataendelea na shughuli za mpira hapo baadaye.

“Kwa sasa hivi siwezi kuongelea sana hicho kitu lakini bado nitaendelea kuwa kwenye mazingira ya mpira. Siwezi nikatoka nje ya mpira na kusema kuwa nitakuwa na shughuli nyingine,” alisema Msuva.

Al Talaba msimu wa 2025-2026 ilimaliza katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi kuu Iraq huku Msuva akimaliza msimu huo kwa kufunga mabao tisa.

Katika timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ mshambuliaji huyo aliandika rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa baada ya kufikisha mabao 25 Desemba 27, 2025 wakati alipopachika bao dhidi ya Uganda kwenye mchezo wa AFCON 2025 nchini Morocco.