Mwakinyo ajitetea kwa kipigo, Edo Kumwembe atoa neno
Bondia Hassan Mwakinyo. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Michael Soro amepigana mapambano 45 kati ya hayo ameshinda 39, ametoka sare mara mbili na amepoteza mapambano sita.
Saa chache baada ya Hassan Mwakinyo kupoteza pambano lake dhidi ya Michael Soro huko Ivory Coast, bondia huyo amesema kuwa alikuwa dhaifu kimwili ingawa amekubali matokeo.
Mwakinyo alipoteza pambano hilo kwa TKO katika raundi ya tisa na kumfanya akose mkanda wa IBO ambao alikuwa anauwania.
Bondia huyo wa uzani wa kati, amesema kuwa hakuwa katika hali ya kawaida wakati wa pambano hilo licha ya maandalizi mazuri ambayo aliyafanya kabla.
"Napenda nitoe pole za maumivu kwa wote mlioumizwa au kutoelewa kilichotokea jana. Siyatetei matokeo ya kupoteza kwangu na siumii sababu ndio mchezo. Kinachoniumiza zaidi ni mimi kuwa dhaifu kiasi cha kushindwa kujitetea.
"Hata namna ya upiganaji wangu haukuwa ule mliouzoea. Ilikua ni mechi ngumu ambayo niliweka bidii zangu kwenye mazoezi ya nguvu sana. Na ndio mechi ambayo nilicheza nikiwa niko dhaifu na mwepesi sana yote kwa yote ni matokeo tu na hakuna budi kupokea," amesema Mwakinyo.
Ushindi huo umemfanya Soro afikishe idadi ya mapambano 38 aliyoshinda, akitoa sare mawili na kupoteza manne.
Katika hatua nyingine, Mchambuzi wa Michezo Tanzania, Edo Kumwembe kupitia ukurasa wake wa Instagram, ametoa neno baada ya pambano hilo la Mwakinyo.
"Hii kitu imeniuma lakini sina cha kufanya. Watanzania wengi wanashangilia Mjomba wangu @hassanmwakinyojr kupoteza fight yake. Nimemuita mjomba kwa sababu mimi Mama anatokea Tanga.
"Tatizo ni mjomba Hassan au Watanzania?..tufungue mjadala. Ingekuwa pambano la ndani sio shida. Lakini sisi na yule jamaa Soro lilipaswa kuwa pambano la sisi dhidi ya yeye.
"Hili limekuwa tofauti. Imekuwa kama vile sisi na Soro dhidi ya Mjomba Hassan. Labda kuna mahala Anko amekosea wakati akijenga maisha yake ya mchezo huu. Vyovyote ilivyo yeye ndiye bondia bora zaidi Tanzania kwa sasa.
"Hata hivyo mahusiano mazuri na jamii yako ni kitu muhimu katika maisha ya kila siku. Nani anamchukia Mbwana Samatta kiasi cha kufurahia akikosa goli?..sidhani. All the best Anko Hassan. WE WILL RISE AGAIN," ameandika Kumwembe.