Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MZEE WA FACT: Hii ndio Brazil aliyocheza Pele

Muktasari:

  • Yaani kwa kifupi Pele alitajwa na sheria kama mlima, au mbuga ya wanyama au kitu chochote ambacho ni nyara.

Dunia imeshangazwa na kiwango kilichooneshwa na timu za Brazil kwenye mashindano ya Klabu Bingwa ya Dunia yanayoendelea huko Marekani. Brazil ilipeleka timu nne kwenye mashindano hayo na zote zilifuzu hatua ya 16 bora.

Palmeiras waliokuwa kundi A sambamba na Inter Miami ya Messi, Porto na Al Ahly ya Afrika, walimaliza vinara na tayari wamefuzu robo fainali, kumbuka hawa ndiyo jezi yao inavaliwa sana hapa nchini ikiwa na wadhamini Grefisa.

Botafogo waliokuwa kundi B sambamba na PSG, Atletico Madrid na Seattles Sounders ya Marekani, walimaliza katika nafasi ya pili lakini wakilingana alama na vinara PSG huku wakifanya maajabu ya kuwafunga mabingwa hao wa Ulaya, ingawa wameshatolewa lakini historia inabaki.

Flamengo walikuwa kundi D sambamba na Chelsea, Esperance ya Tunisia na Los Angeles FC ya Marekani, wakaongoza kundi.

Fluminense walikuwa kundi F sambamba na Dortmund, Mamelodi Sundowns na Ulsan ya Korea, wakamaliza wa pili. Zaidi tu ya kufuzu hatua ya 16 bora, timu hizi zilionesha uwezo mkubwa huku zikitambulisha mbinu kadhaa ambazo hazikuwa kuonekana kabla.

Kwa mfano, Fluminense walitambulisha aina mpya ya kupanga ukuta dhidi ya mikwaju ya adhabu ndogo. Badala ya watu kusimama upande mmoja wa goli na kumuachia kipa upande mwingine wa goli, waliugawa ukuta mara mbili, watu wanne wanne. Katikati wakamuachia kipa, hii iliwapa tabu sana hata mafundi wa mikwaju ya aina hiyo.

Hiki ambacho timu hizi imekionesha kwenye mashindano kimekuja kutoa majibu juu ya swali la muda mrefu kuhusu uhodari wa Pele.

Nyota huyo wa zamani wa klabu ya Santos ya Brazil na timu ya taifa ni binadamu pekee kushinda Kombe la Dunia mara tatu.

Simulizi nyingi zinazomhusu zinamtaja kama mchezaji bora zaidi kuwahi kutokea. Lakini kuna watu wengi hawampi hiyo heshima wakisema alionekana bora sana kwa sababu alicheza Brazil, angecheza Ulaya asingefanya hata nusu ya alichofanya.

Kwamba ligi ya Brazil haikuwa ngumu kama ligi za Ulaya kwa hiyo alicheza kwenye ligi nyepesi dhidi ya timu nyepesi. Wanasahau kwamba alikutana na timu za Ulaya kwenye Kombe la Dunia na alizinyanyasa alivyotaka.

Hata kwenye ngazi ya vilabu, japo hakukuwa na mashindano makubwa kama sasa ya kukutanisha timu za Ulaya za Brazil kama sasa, lakini bado zilikutana kwenye mashindano maalumu au mechi za kirafiki, na alizinyanyasa.

Kwa mfano, mwaka 1962 Santos ya Pele ilienda Ulaya kucheza na mabingwa wa Ulaya, Benfica ya Ureno kwenye kombe la mabara la vilabu. Benfica wakafungwa 5-2 huku Pele akiubonda mwingi mno na kuishangaza Ulaya.

Kabla ya hapo, mwaka 1959 Santos na Pele walifanya ziara maalumu Ulaya na kucheza na vilabu kadhaa. Wakaifunga Inter Milan 7-1, Pele akifunga mabao manne, na pia wakaifunga Barcelona 5-1, Pele akifunga mabao mawili.

Kwa jumla Pele alicheza mechi zaidi ya 200 dhidi ya timu za Ulaya na akafunga mabao 200. Lakini kwa kuwa watu wengi huishia kuangalia ligi za Ulaya tu na kudhani ndio zina kila kitu, ndio maana humvunjia heshima Pele.

Lakini huu uwezo ambao timu za Brazil zinauonesha kwenye mashindano yanayoendelea nchini Marekani, unatudhihirishia ugumu wa ligi yao na uwezo wa Pele.

Kama Pele alicheza kwenye ligi yenye timu bora kama hizi, ilikuwa lazima awe bora kama anavyotajwa. Hata hivyo, sio kwamba Pele hakucheza Ulaya kwa sababu alikosa timu au hakuwa na uwezo, hapana.

Serikali ya Brazil ilitunga sheria kabisa ya kumzuia Pele kucheza nje ya nchi yao. Sheria hiyo ilimtaja Pele kama nyara ya taifa kwa hiyo hatakiwi kutolewa. Yaani kwa kifupi Pele alitajwa na sheria kama mlima, au mbuga ya wanyama au kitu chochote ambacho ni nyara.

Timu kubwa za Ulaya kama Real Madrid, Barcelona, na Milan, zilituma ofa ya kumnunua lakini haikuwezekana kwa sababu alikuwa hazina ya taifa alikuwa nyara ya taifa alikuwa hauzwi. Kwa hiyo Pele alicheza Brazil hadi akastaafu mpira mwaka 1974.

Mwaka 1975, klabu ya New York Cosmos ya Marekani ikamfuata na kumsaini akiwa ameshastaafu takribani mwaka mzima...ili akawasaidie kuujenga mpira nchini humo.


Pele ni kama Papa

New York Cosmos ilitaka kumsaini Pele tangu mwaka 1970 lakini haikuwezekana hadi alipostaafu mwaka 1974.

Lakini klabu hiyo iliamini kwamba Pele licha ya kustaafu bado ana kitu cha kuwasaidia uwanjani na nje ya uwanja endapo watamshawishi kurudi dimbani.

CEO wa klabu hiyo, Clive Toye akaenda kumshawishi CEO wa kampuni kubwa ya burudani ya Warner Bros, Steve Ross, ambayo ilikuwa inamiliki studio kubwa za muziki za Warner Studios na vyombo vya habari na mawasiliano kama TV.

Kampuni hii ndio ilikuwa wadhamini wakubwa wa klabu ya New York Cosmos. Lakini bahati mbaya Ross hakuwa akimfahamu kabisa Pele hivyo akasita.

Toye akamwambia, "Pele ninayemzungumzia ni mtu mkubwa sana kwenye mpira. Kama alivyo baba mtakatifu Papa kwa Wakristo ndivyo alivyo Pele kwenye mpira".

Ross aliposikia hivyo, akatoa pesa ndefu kumrudisha Pele uwanjani.

Mwaka 1975, Pele akaibukia Marekani kuichezea New York Cosmos.

Pele akaenda Marekani na akafanya mabalaa makubwa na kuufanya mpira ufuatiliwe sana nchini humo.

Na sasa vilabu vinne vya Brazil vipo katika ardhi ile ile iliyomrudisha Pele dimbani baada ya kustaafu. Na vinatukumbusha kwamba Pele hakucheza ligi dhaifu ndio maana alionekana bora, alionekana bora kwa sababu alikuwa bora!