Okwa, Akpan ni Ihefu

NYOTA wawili wa Simba, Nelson Okwa na Victor Akpan waliosajiliwa kwenye dirisha kubwa la usajili msimu huu wamekubali kutolewa kwa mkopo kwenda Ihefu kwenye dirisha ambalo litafungwa kesho Januari 15.
Awali Okwa alikubali kutolewa kwa mkopo ila aliomba kwenye timu yenye mazingira mazuri iliyopo Tanzania wakati Akpan alikuwa amegomea maamuzi hayo kwa kuamini bado anaouwezo wa kuwania nafasi ya kucheza.
Baada ya majadiliano yaliyochukua siku mbili akiwa na wakala wake Akpan alikubali kutolewa kwa mkopo kama ilivyokuwa kwa Okwa na uongozi wa Simba tayari umewapatia timu ya kwenda kucheza.
Uongozi wa Simba umewaeleza Okwa na Akpan timu iliyopatikana ni Ihefu iliyokuwa tayari kuwachukua nyota hao wawili kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye kikosi chao haswa mzunguko huu wa lala salama.
Nyota hao wawili wameelezwa kama hawajaridhika na timu hiyo waliyopatiwa na mabosi wao wanaweza kueleza kuna nyingine waliyokubaliana nayo na wanataka kwenda na kama halitakuwepo siku si nyingi watatangazwa kama wachezaji wapya wa Ihefu.
Hadi sasa Ihefu tayari imenasa wachezaji wawili wazawa mshambuliaji, Adam Adam na beki wa kati, David Mwantika ambaye alikuwa mchezaji huru kwani mzunguko wa kwanza hakucheza timu yoyote ya Ligi Kuu Bara.
Alipotafutwa Okwa kuzungumzia hilo alisema kuna maamuzi yamefanyika kwa upande wake dhidi ya viongozi wa Simba na si vyema kulieleza wakati huu hadi hapo yatakapokuwa yamekamilika.
"Wakati huu sipo sawa naomba niwaachie viongozi wa Simba wao wanaweza kuzungumza ila nipo nyumbani hapa Dar es Salaam wala bado sijaenda mahala kokote," alisema Okwa aliyesajiliwa na Simba akitokea, Rivers United ya Nigeria.