Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Prisons, Fountain mmoja anabaki

Muktasari:

  • Mechi hii itakuwa ya nne kwa timu hizi kukutana, ambapo mbili ni za Ligi Kuu Bara na mbili ni za play-off, ambapo kati ya hizo zote hakuna iliyoibuka mbabe zaidi ya mwenzake, jambo linalosubiriwa kwa hamu kuona na leo ni kipi kitachojiri.

Kitendawili cha kujua ni timu gani kati ya maafande wa Tanzania Prisons dhidi ya Fountain Gate cha kubakia Ligi Kuu Bara msimu ujao, kitateguliwa leo saa 10:00 jioni, wakati miamba hiyo itakapochuana kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Mechi hiyo ni ya marudiano ya play-off, ili kusaka nafasi ya kubakia baada ya ile ya kwanza iliyopigwa Juni 26, 2025, kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo mjini Babati, mkoani Manyara, timu hizo kutoka sare ya kufungana kwa bao 1-1.

Katika mechi hiyo, Fountain ilipata bao la utangulizi la mshambuliaji nyota wa kikosi hicho, Edgar William dakika ya 39, kabla ya maafande wa Prisons kujibu mapigo kipindi cha pili na kulisawazisha dakika ya 62, likifungwa na Oscar Mwajanga.

Timu hizo zinakutana leo Jumatatu baada ya Fountain kumaliza nafasi ya 14 na pointi 29, ikishinda mechi nane, sare tano na kupoteza 17, huku Prisons ikimaliza ya 13 na pointi 31, kufuatia kushinda minane, ikitoka sare saba na kupoteza 15.

Fountain ilihitimisha msimu huu wa 2024-2025 Juni 22 kwa kuchapa mabao 3-2, ikicheza nyumbani dhidi ya matajiri wa Jiji la Dar es Salaam Azam FC, huku kwa upande wa Prisons ikitoka sare ya kufungana mabao 3-3, mbele ya Singida Black Stars.

Mechi hii itakuwa ya nne kwa timu hizi kukutana, ambapo mbili ni za Ligi Kuu Bara na mbili ni za play-off, ambapo kati ya hizo zote hakuna iliyoibuka mbabe zaidi ya mwenzake, jambo linalosubiriwa kwa hamu kuona na leo ni kipi kitachojiri.

Katika mechi za Ligi Kuu msimu huu, timu hizi zilianza kukutana Oktoba 1, 2024, kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, ambapo Prisons ilishinda mabao 3-2, yaliyofungwa na Nurdin Chona kwa penalti, Ezekia Mwashilindi na Vedastus Mwihambi.

Kwa upande wa mabao ya Fountain katika pambano hilo, yalifungwa na Seleman Mwalimu 'Gomez' anayeichezea kwa sasa Wydad Casablanca ya Morocco aliyojiunga nayo dirisha dogo la Januari 2025 na Abalkassim Suleiman aliyehamia pia Pamba Jiji.

Mechi ya mwisho ya Ligi Kuu baina ya timu hizo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Februari 26, 2025, Fountain ilishinda bao 1-0, lililokuwa la mkwaju wa penalti, lililofungwa na beki wa kikosi hicho, Amos Kadikilo dakika ya 28.

Kwa maana hiyo, katika Ligi Kuu Bara kila timu imeshinda nyumbani kwake, japo sare ya bao 1-1, katika mechi ya kwanza ya mtoano kusaka tiketi ya kubaki kwa msimu ujao, inaonyesha wazi pambano hili litakuwa ni gumu na lenye kuvutia mashabiki.

Kocha wa Prisons, Amani Josiah alisema nidhamu ya kujilinda na kutumia pia vyema nafasi za kufunga ndizo zitakazowabeba, huku Kocha wa Fountain, Mohamed Ismail 'Laizer', akiamini nafasi bado ipo ya kubaki, licha ya ugumu uliopo ugenini.

Mshindi kati ya Prisons au Fountain Gate, itabakia Ligi Kuu Bara msimu ujao, ingawa itakayopoteza itaenda kucheza tena mechi ya play-off dhidi ya Stand United inayoshiriki Ligi ya Championship, iliyoitoa Geita Gold kwa jumla ya mabao 4-2.

Mechi ya play-off kati ya Stand iliyomaliza ya tatu na pointi zake 61, katika Ligi ya Championship msimu wa 2024-2025 na kupata nafasi hiyo, itacheza na Prisons au Fountain Julai 3, huku marudiano yakitarajiwa kupigwa Julai 7, 2025.

Kama timu ya Ligi Kuu itashinda itasalia katika ligi hiyo kwa msimu ujao na kuizuia Stand kupanda daraja, lakini kama Chama la Wana itashinda itapanda daraja kuzifuata Mtibwa Sugar na Mbeya City na timu ya Ligi Kuu itashuka kuungana na KenGold na Kagera Sugar zilizotangulia mapema.