Rais wa soka Afrika afungiwa miaka mitano

Monday November 23 2020
is pic
By Mwandishi Wetu

Lausanne, Uswisi (AFP)
Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Ahmad Ahmad amefungiwa kwa miaka mitano na Fifa kutokana na rushwa, chombo hicho kinachoendesha mpira wa miguu duniani kimesema leo Jumatatu (Novemba 23).
Ahmad, kutoka Madagascar, amekuwa rais wa CAF tangu Machi 2017 na alikuwa anawania tena nafasi hiyo kabla ya Fifa kumzuia kushiriki "katika masuala ya uongozi".
Katika taarifa yake, Fifa imesema Ahmad alikiuka jukumu lake la utii, kutoa zawadi na upendeleo mwingine, ubadhirifu wa fedha na kutumia vibaya nafasi yake kama rais wa CAF.
Ahmad pia amepigwa faini ya dola 220,000 za Marekani (sawa na zaidi ya Sh450 milioni za Kitanzania) na Fifa kwa vitendo hivyo, ambavyo vinahusiana na "kuandaa na kugharimia mahujaji wa Umrah kwenda Makka" na kuhusika kwake katika kwake katika mkataba wa CAF na kampuni ya kutengeneza vifaa vya michezo.
Hata kabla ya watu kujitokeza kutangaza nia ya kuwania urais wa CAF, nchi 46 ziliandika barua za kuonyesha zinamuunga mkono Ahmad kuendelea na wadhifa huo aliouchukua kutoka kwa kiongozi wa muda mrefu, Issa Hayatou.

Advertisement