Rashford kurejea Man United wiki ijayo

Muktasari:
- Tayari anahusishwa na klabu mbalimbali barani Ulaya, zikiwemo Newcastle United na Barcelona timu anayoidai kuwa ndoto yake.
Birmingham, England. Mshambuliaji Marcus Rashford anatarajiwa kurejea kwenye mazoezi ya kikosi cha Manchester United wiki ijayo, lakini bado hatima yake ndani ya klabu hiyo inaonekana kutokuwa na uhakika, baada ya Aston Villa kuthibitisha kutotumia kipengele cha kumchukua kwa uhamisho wa kudumu kwa dau la Pauni milioni 40 (Sh135 bilioni).

Rashford, mwenye umri wa miaka 27, alikuwa amewekwa kando Old Trafford tangu Desemba mwaka jana kabla ya kupelekwa kwa mkopo Aston Villa katika dirisha dogo la usajili mwezi Februari. Akiwa Villa, alionyesha dalili za kuimarika kwa kucheza mechi 17, akifunga mabao manne na kusaidia mengine.

Hata hivyo, pamoja na mchango huo, kocha wa Aston Villa, Unai Emery hakuona sababu ya kuhalalisha mkataba wa kudumu, huku klabu ikitangaza rasmi kutotumia chaguo hilo. Kupitia taarifa ya klabu, Villa iliwashukuru wachezaji waliomaliza mikataba au mikopo yao, wakiwemo Rashford, Marco Asensio na Axel Disasi.

Rashford, ambaye amekuwa kwenye kikosi cha United tangu akiwa na umri wa miaka saba, analipwa Pauni 315,000 sawa na Sh1 bilioni kwa wiki na ikiwa ataendelea na mkataba huo hadi mwaka 2028, atakuwa amevuna zaidi ya Sh157 bilioni kwa kipindi hicho, kiwango ambacho kinaweza kuzuia vilabu vingine kumchukua kirahisi. Tayari anahusishwa na klabu mbalimbali barani Ulaya, zikiwemo Newcastle United na Barcelona timu anayoidai kuwa ndoto yake.
Katika mahojiano aliyofanya mapema mwaka huu, Rashford alieleza wazi kuwa yuko tayari kuanza maisha mapya: “Kwa upande wangu binafsi, nahisi niko tayari kwa changamoto mpya. Sitasema mabaya kuhusu Manchester United hiyo si tabia yangu. Wakati nitaondoka, nitatoa tamko la heshima na la upendo.”

Taarifa kutoka ndani ya Manchester United zinaonyesha kuwa Rashford yupo kwenye orodha ya wachezaji wasio kwenye mipango ya kocha Ruben Amorim, ambaye alimpiga chini kwa mara ya kwanza kwenye mchezo wa derby dhidi ya Man City mwezi Desemba. Baada ya hapo, Rashford hakuwahi tena kuvalishwa jezi ya United hadi alipohamia Villa siku ya mwisho ya dirisha la usajili.
Kwa sasa, Amorim tayari ameanza kujenga kikosi chake kwa kumsajili mshambuliaji Matheus Cunha kutoka Wolves na kuwania saini ya Bryan Mbeumo wa Brentford hatua inayoashiria wazi kuwa Rashford anazidi kusogezwa pembeni.

Kama Rashford hatapata klabu ya kujiunga nayo kabla ya dirisha kufungwa, atalazimika kurejea mazoezini Carrington japo kwa mazingira yanayoweza kuwa ya kukatisha tamaa, hasa ikizingatiwa kuwa Amorim ameshawahi kusema hadharani kuwa mchezaji huyo lazima ajibadili kama anataka nafasi kwenye kikosi chake.
Ikiwa Rashford atashindwa kuhamia kwingine, basi United inaweza kulazimika kukubali kupunguza thamani yake au kumtoa tena kwa mkopo hasa kwa klabu zinazoweza kuchukua mzigo wa mshahara wake mkubwa.