Refa ambaye hakuona rafu mbaya Kombe la Dunia, afariki

Thursday November 12 2020
refa pic

The Hague, Uholanzi. Refa wa zamani, Charles Corver, ambaye alichezesha mechi ya nusu faina za Kombe la Dunia baina ya Ujerumani Magharibi na Ufaransa mwaka 1982, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 84, chama cha soka cha Uholanzi kimetangaza jana Jumatano (Novemba 11).
"Corver alifariki Jumanne jioni kwa ugonjwa," Shirikisho la Soka la Uholanzi (KNVB) limesema.
"Waamuzi wachache wa Uholanzi wamechezesha mechi muhimu za aina hiyo... na katika miaka ya sabini na themanini Corver alikuwa kileleni katika ulimwengu wa waamuzi."
Corver atakumbukwa kwa mechi ya nusu fainali baina ya Ujerumani Magharibi na Ufaransa aliyochezesha wakati wa fainali za Kombe la Dunia nchini Hispania.
Mdachi huyo hakuona rafu mbaya ambayo kipa wa Ujerumani, Harald "Toni" Schumacher alimchezea  beki wa Ufaransa, Patrick Battiston ambaye alilazimika kutoka.
Battiston alianguka chini na jino lake kung'oka, huku akiumia uti wa mgoongo. Madaktari wa dharura walilazimika kumuwekea hewa ya oksijeni uwanjani.
"Kwa kifupi, sikuliona (tukio hilo hadi nilipoangalia picha za marudiao siku mbili baadaye)," Corver aliliambia jarida la soka la Voetbal International katika mahojiano miaka sita iliyopita.
"FIFA haijawahi kuniadhibu na haijaniangusha."
Mbali na kuonekana katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1978 na 1982, Corver pia alichezesha mechi za fainali za Kombe la Uefa za mwaka 1977 na 1983 na klabu bingwa ya Ulaya mwaka 1978 baina ya Liverpool na Club Brugge.
Pia alipewa hadhi ya kifalme ya Uholanzi mwaka 2006.


Advertisement