Rekodi nne zambeba Morocco Stars
Muktasari:
- Taifa Stars imeweka rekodi ya kwanza ambayo ni kukusanya idadi kubwa ya pointi katika awamu moja ya Fainali za Afrika iwe kwa CHAN au zile za kawaida (AFCON) ikiwa chini ya Kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’.
Dar es Salaam. Rekodi nne tofauti zilizowekwa katika Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezali wa Ligi za Ndani (CHAN) 2024 zinazoendelea katika nchi za Kenya, Uganda na Tanzania, zinamfanya Hemed Suleiman ‘Morocco’ kuwa kocha aliyefanikiwa zaidi akiwa na kikosi cha Taifa Stars katika fainali za Afrika kuliko kocha mwingine yeyote.
Ushindi wa mabao 2-1 ambao Taifa Stars iliupata dhidi ya Madagascar juzi, uliifanya Taifa Stars kufikisha pointi tisa na hivyo kujihakikishia rasmi uongozi wa kundi B la fainali za CHAN huku pia ikikata tiketi ya kucheza robo fainali.
Ikiwa chini ya Morocco, Taifa Stars imeweka rekodi ya kwanza ambayo ni kukusanya idadi kubwa ya pointi katika awamu moja ya Fainali za Afrika iwe kwa CHAN au zile za kawaida (AFCON).
Kabla ya CHAN mwaka huu, Marcio Maximo na Etienne Ndayiragije ndio walikuwa wanashikilia rekodi ya kuipa Taifa Stars pointi nyingi ambapo chini ya kila mmoja, timu hiyo ilivuna pointi nne, mara zote zikiwa ni katika fainali za CHAN, Maximo akifanya hivyo 2009 na Ndayiragije ni 2020.
Rekodi ya pili ambayo Morocco ameiweka ni kuiongoza Taifa Stars kumaliza ikiwa kinara ambapo kabla yake haijawahi hata kushika nafasi ya pili katika CHAN na AFCON.
Kwa kupata ushindi dhidi ya Madagascar, Taifa Stars imejihakikishia kumaliza ikiwa ya kwanza kwa vile ni Burkina Faso tu kwenye kundi lake inayoweza kufikia pointi tisa ilizonazo lakini ikiwa hivyo, Taifa Stars itabebwa na kanuni ya kwanza ya kuamua mshindi ambayo inatumika kwenye mashindano hayo iwapo timu mbili zinalingana pointi ambayo ni kuangalia matokeo ya mchezo baina ya timu mbili zilizofungana kwa pointi kwa vile ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso.
Morocco ameweka rekodi ya nne ambayo ni kuwa kocha wa kwanza kuiingiza Taifa Stars katika hatua ya mtoano ya mashindano ya Afrika.
Katika fainali za AFCON 1980, 2019 na 2023 na fainali za CHAN 2009 na 2020, Taifa Stars ilikwama katika hatua ya makundi.
Rekodi ya nne ambayo Morocco ameiweka ni kuiongoza Taifa Stars kupata ushindi katika idadi kubwa ya mechi mfululizo za mashindano rasmi.
Taifa Stars imepata ushindi katika mechi sita mfululizo za kimashindano ikianzia COSAFA ikaichapa Eswatini kwa mabao 2-1 kisha katika mashindano maalum ya kujiandaa na CHAN 2024, ikazifunga Uganda kwa bao 1-0 na baadaye Senegal kwa mabao 2-0.
Moto wa Taifa Stars ukaendelea katika CHAN ambapo ikazifunga Burkina Faso, Mauritania kwa bao 1-0 na kisha juzi ikaibamiza Madagascar.
Kocha Morocco alisema kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano ambao anaupata.
“Kikubwa ni sapoti tunayopata kutoka kwa Watanzania, mimi, wenzangu katika benchi la ufundi na wachezaji kiujumla. Inatupa nguvu na hamasa ya kujituma tukiamini nyuma yetu kuna kundi kubwa linatuunga mkono.
“Naamini kwa uwezo wa mwenyezi Mungu na sapoti hii ikaendelea kwa ukubwa zaidi, tutafanya vyema zaidi ya hapa. Tunawaomba Watanzania waendelee kutuunga mkono na kujitokeza kwa wingi uwanjani kutushangilia,” alisema Morocco.
Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije amempongeza Morocco na benchi lake la ufundi kwa mafanikio ambayo timu hiyo inayapata.
“Nampongeza kocha Morocco na wasaidizi wake kwa kazi nzuri wanayoifanya. Sio jambo rahisi lakini wanajitahidi kufanya vyema. Nawashauri Watanzania wasimame nao hasa kipindi kama hiki ambacho timu inaonyesha muelekeo mzuri,” alisema Ndayioragije.