Ronaldo atupia mawili akiandika rekodi Kombe la Dunia
Muktasari:
- Ronaldo pia ameweka rekodi ya kuwa Mfungaji Bora wa muda wote wa Ureno katika Kombe la Dunia.
Houston, Marekani. Nahodha wa Ureno, Cristiano Ronaldo ameweka rekodi mbili katika ushindi wa mabao 5-0 ambao timu yake ya taifa ya Ureno imeupata dhidi ya Uzbekistan leo, Jumanne, Juni 23, 2026 Houston, Marekani.
Ronaldo ambaye amepachika mabao mawili katika mchezo huo, kwanza ameboresha rekodi yake ya kuwa mchezaji aliyefunga katika fainali nyingi tofauti za Kombe la Dunia, akifanya hivyo katika fainali sita.
Alianza kufunga katika fainali za Kombe la Dunia 2006 zilizofanyika Ujerumani, akafanya hivyo katika fainali zilizofanyika Afrika Kusini 2010.
Mwaka 2014, Ronaldo akafunga tena katika fainali zilizofanyika Brazil na kisha akafanya hivyo katika fainali za 2018 nchini Russia.
Fainali zilizopita ambazo zilifanyika Qatar mwaka 2022, Ronaldo alifunga tena na amefanya hivyo mwaka huu katika fainali zinazofanyika Marekani, Canada na Mexico.
Rekodi ya pili ambayo Ronaldo ameiweka ni kuwa Mfungaji Bora wa muda wote wa Ureno katika Kombe la Dunia.
Awali rekodi hiyo ilikuwa imeshikiliwa na Eusebio ambaye alikuwa amepachika mabao tisa na sasa Ronaldo ana mabao 10.
Katika mchezo wa leo, mabao mengine ya Ureno yamefungwa na Nuno Mendes, Rafael Leao na lingine moja la kujifunga la Abduvakhid Nematov.
Ureno sasa inaongoza msimamo wa kundi K ikiwa na pointi nne.