Safari ya Gyokeres kwenda Arsenal yapigwa breki
Muktasari:
- Ripoti hiyo inasema kuwa bado milango ya mazungumzo iko wazi, lakini pia kuna hatari kubwa ya mazungumzo hayo kuvunjika kabisa.
Hatma ya mshambuliaji wa Kimataifa wa Sweden, Viktor Gyokeres, kujiunga na Arsenal ya England ipo njia panda, baada ya taarifa kutoka Ureno kudai kuwa mazungumzo kati ya klabu hiyo na Sporting Lisbon yameanza kukwama kuhusu makubaliano ya ada ya uhamisho na malipo ya nyongeza.
Kwa mujibu wa gazeti la Record nchini Ureno, kuna mvutano mkubwa juu ya bonasi ya kiasi cha Pauni milioni 8.7 (Sh28 bilioni) ambayo Sporting wanataka iwe sehemu ya dili hilo. Arsenal, kwa upande wao, wanasuasua kuongeza kiasi hicho juu ya Pauni milioni 62.4 (Sh206 bilioni) ambazo tayari wamekubali kulipa kama ada ya awali ya uhamisho.
Ripoti hiyo inasema kuwa bado milango ya mazungumzo iko wazi, lakini pia kuna hatari kubwa ya mazungumzo hayo kuvunjika kabisa, hali inayozua wasiwasi kwa mashabiki wa Arsenal waliokuwa wakisubiri kutangazwa rasmi kwa usajili wa mshambuliaji huyo hatari barani Ulaya.
Hii inajiri huku kocha Mikel Arteta akiwa tayari ameshakubali masharti binafsi na mchezaji huyo, huku taarifa zikieleza kuwa Gyokeres anataka kujiunga na Arsenal licha ya rais wa Sporting, Frederico Varandas, kuchelewesha makubaliano kwa matumaini ya kupata ofa za dakika za mwisho kutoka kwa klabu pinzani.
Inadaiwa kuwa Varandas alikataa ofa ya mwisho ya Arsenal ya Pauni milioni 60 kama malipo ya pamoja, na kuwaeleza wazi kuwa hawatampata Gyokeres bila kuongeza dau na malipo ya awali kuwa makubwa zaidi.
Kwa sasa, pande zote mbili zimeripotiwa kuwa karibu kufikia makubaliano ya Pauni milioni 55 (Sh192 bilioni) kama ada ya awali, pamoja na Pauni milioni 7.4 (Sh24 bilioni) kama bonasi, huku Gyokeres mwenyewe tayari akiwa amekubali mkataba wa miaka mitano.
Arsenal wanatarajia dili hilo kukamilika kabla ya mwishoni mwa wiki, ili mshambuliaji huyo aweze kusafiri na timu kwenda Asia kwa ziara ya maandalizi ya msimu mpya.
Katika usajili mwingine, Arsenal pia wameongeza kasi ya mazungumzo na Valencia kuhusu beki wa kati Cristhian Mosquera, huku wakitarajia pia kumalizana na kinda wao wa miaka 18, Ethan Nwaneri, kuhusu mkataba mpya.
Wakati huohuo, Noni Madueke alifanyiwa vipimo vya afya siku ya Jumatatu kwa ajili ya uhamisho wake wa Pauni milioni 52 kutoka Chelsea, huku Eberechi Eze wa Crystal Palace akitajwa kama usajili unaofuata kwa Arsenal.
Gyokeres ambaye msimu uliopita alifumania nyavu mara 54 akiwa na Sporting katika michuano yote, amekuwa mmoja wa washambuliaji hatari zaidi Ulaya. Tangu alipojiunga na Sporting kutoka Coventry kwa Pauni milioni 20 Sh66 bilioni) mwaka 2023, amefunga jumla ya mabao 97 katika mechi 102.
Kabla ya hapo, alifunga magoli 43 akiwa Coventry katika kipindi cha miaka miwili na nusu. Akiwa Brighton, alicheza mechi 8 tu na kufunga bao moja katika kipindi cha zaidi ya miaka mitatu.
Usajili wa Gyokeres unatazamwa kama sehemu muhimu ya juhudi za Arsenal kuhakikisha wanatwaa taji la Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2004. Tayari msimu huu wa kiangazi Arsenal wamefanikiwa kumsajili kiungo Martin Zubimendi kutoka Real Sociedad kwa Pauni milioni 60 (Sh200 bilioni) pamoja na kipa, Kepa Arrizabalaga na kiungo Christian Norgaard wa Denmark.