Samatta astaafu kuitumikia Taifa Stars baada ya miaka 15
Nahodha wa muda mrefu wa Taifa Stars, Mbwana Samatta. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Samatta amebainisha kuwa, uamuzi huo umekuja baada ya kutafakari kwa kina na anaamini sasa ni wakati wa kutoa nafasi kwa vipaji vipya kuifikisha timu katika hatua za juu zaidi.
Nahodha wa muda mrefu wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ametangaza rasmi kustaafu kuitumikia timu hiyo, akihitimisha safari ya takribani miaka 15 aliyosema imejaa mafanikio, changamoto na kumbukumbu zisizosahaulika.
Katika taarifa aliyotoa leo Jumanne Julai 7, 2026, Samatta amesema amefikia uamuzi huo baada ya kutafakari kwa kina, akieleza kuwa amejivunia kuitumikia Tanzania kwa kipindi chote alichokuwa sehemu ya kikosi cha Taifa Stars.
Amesema moja ya mafanikio makubwa aliyoyapata ni kuiongoza timu hiyo kwa miaka 10 akiwa nahodha, huku akishuhudia Taifa Stars ikifuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mara tatu na kuweka historia ya kufuzu hatua ya 16 bora kwa mara ya kwanza.
Nahodha wa muda mrefu wa Taifa Stars, Mbwana Samatta. Picha na Mtandao
"Ulikuwa wakati mzuri na wa kipekee katika maisha yangu kuwa mchezaji wa Timu ya Taifa kwa takribani miaka 15 na najisikia fahari kusema nashukuru kwa nafasi hii.
"Miaka 10 ya kuwaongoza wachezaji wenzangu kama nahodha wa Taifa Stars imekuwa yenye alama kubwa katika maisha yangu ikiwemo kufuzu fainali za AFCON mara tatu (3) na kutimiza ndoto ya muda mrefu ya kuweka historia ya kuingia hatua ya 16 bora kwa mara ya kwanza. Naamini huu ni wakati wa vipaji vipya kupewa nafasi ya kutufikisha kwenye hatua za juu zaidi.
"Ilikuwa safari njema iliyojaa nyakati zisizosahaulika na zenye hisia mchanganyiko, naishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) kwa kuhakikisha timu ya taifa ya Tanzania inakuwa tamanio na ndoto ya kila mchezaji.
"Shukrani za kipekee pia ziende kwa familia yangu, wachezaji wenzangu, rafiki zangu, wadau wa Taifa Stars na Watanzania wenzangu kwa kunionesha upendo na kuiunga mkono timu hii katika nyakati zote za furaha na huzuni.
"Nikijivunia Utanzania wangu, naahidi kuendelea kutoa mchango wangu kwa timu ya Taifa katika maeneo mengine yaliyo ndani ya uwezo na uzoefu wangu," amesema Samatta.
Moja ya mafanikio makubwa ya Samatta katika kuiongoza Taifa Stars ni kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mara tatu, pamoja na kuweka historia ya kuifikisha timu hiyo hatua ya 16 bora kwa mara ya kwanza AFCON 2025.
Nahodha wa muda mrefu wa Taifa Stars, Mbwana Samatta (kushoto). Picha na Mtandao
Samatta alianza kuitumikia Taifa Stars mwaka 2011, hadi anatangaza kustaafu kuitumikia timu hiyo, amefunga mabao 22 katika mechi 87.
Bao lake la kwanza alifunga Machi 26, 2011 katika mechi ya kufuzu AFCON 2012 dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, iliyochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, huku pia bao la 22 akilifunga dhidi ya mpinzani huyo uwanjani hapo tena mwezi kama ule, tofauti tarehe na mwaka. Safari hii ilikuwa Machi 23, 2022 ikiwa mechi ya kirafiki.
Nyota huyo anayeitumikia klabu Le Havre inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa, amekuwa mchezaji anayetazamwa zaidi na wanasoka wengi wa Kitanzania kutokana na safari yake kuanzia Tanzania hadi barani Ulaya.
Samatta aliyeanza kucheza Ligi Kuu Bara katika kikosi cha African Lyon kisha Simba SC zote za Dar es Salaam, 2011 alihamia TP Mazembe ya DR Congo ambayo ilimfungulia milango ya kwenda Ulaya mwaka 2016 akitua Ubelgiji akijiunga na KRC Genk. Pia amecheza Royal Antwerp ya hapo Ubelgiji.
Mwaka 2020, aliweka historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya England aliposajiliwa na Aston Villa. Pia amecheza Fenerbahçe ya Uturuki na PAOK ya Ugiriki kabla ya 2025 kusajiliwa Le Havre.
Samatta amechukua uamuzi huo mwaka mmoja kabla ya Tanzania kuwa mwenyeji wa AFCON, fainali zitakazofanyika Juni 2027, kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.
Nahodha wa muda mrefu wa Taifa Stars, Mbwana Samatta. Picha na Mtandao
Uamuzi huo wa Samatta umekuja baada ya Juni 6, 2024 Mwanaspoti kuripoti kwamba TFF ilimkaushia mshambuliaji huyo katika ombi lake la kujiweka kando kufuatia barua aliyoiwasilisha katika shirikisho hilo.
Samatta ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa mchango wao katika maendeleo ya soka nchini na kuhakikisha Taifa Stars inakuwa timu yenye matumaini kwa wachezaji na mashabiki.