Simba, Azam mechi za kimtego makundi CAF
Muktasari:
- Azam ambayo ipo kwenye Kombe la Shirikisho, yenyewe inaanzia hatua ya makundi ikiwa ugenini dhidi ya Maniema kwenye Uwanja wa Stade des Martyrs jijini Kinshasa, DR Congo.
Dar es Salaam. Wawakilishi wawili wa Tanzania kwenye Mashindano ya Klabu Afrika, Simba na Azam leo wanaanza kibarua cha hatua ya makundi ya mashindano hayo katika mechi zitakazochezwa katika viwanja na nchi tofauti leo.
Mechi zote mbili zimepangwa kuanza saa 10:00 ambapo Simba itakuwa mwenyeji wa Petro Luanda ya Angola katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Azam ambayo ipo kwenye Kombe la Shirikisho, yenyewe inaanzia hatua ya makundi ikiwa ugenini dhidi ya Maniema kwenye Uwanja wa Stade des Martyrs jijini Kinshasa, DR Congo.
Simba inaingia katika mchezo wa leo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kupata ushindi katika mechi kama ya leo ya ufunguzi wa hatua ya makundi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita dhidi ya Onze Bravos ya Angola.
Miongoni mwa wachezaji ambao waliunda kikosi cha Bravos, alikuwa Jo Paciencia ambaye kwa sasa yupo katika kikosi cha Petro Luanda na amekuja nacho hapa nchini kwa ajili ya mechi ya leo.
Simba inaingia katika mchezo huo ikiwa na historia ya kufanya vizuri katika mechi za kwanza za hatua ya makundi ambazo inacheza nyumbani ambapo imepoteza mara moja tu kati ya mara saba ambayo ilicheza hatua hiyo, ikishinda mara tano na kutoka sare moja.
Kocha wa Simba, Selemani Matola amesema kuwa pamoja na ugumu na ubora wa wapinzani wao, wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi leo.
"Malengo yetu msimu huu ni kufika nusu fainali lakini haitokuwa rahisi kwa sababu ya ushindani wa timu tulizonazo. Naamini silaha yetu muhimu ni kutumia vyema mechi za nyumbani na hiyo ndio njia pekee na bora itakayotubeba kufanikisha hilo," alisema Matola.
Jijini Kinshasa, DR Congo, wawakilishi wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC watakuwa na kibarua kizito mbele ya wenyeji wao Maniema.
Hii ni mara ya kwanza kwa Azam FC kushiriki hatua hiyo na hapana shaka inahitajika kuanza vizuri hasa kutokana na ugumu wa mchezo unaofuata ambao itacheza na Wydad AC ya Morocco.