Simba Queens kibabe Kariakoo Dabi, Yanga Princess chalii
Muktasari:
- Simba Queens inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake ikiwa na pointi 46 huku Yanga na JKT Queens zikifuata kila moja ikiwa na pointi 39.
Dar es Salaam. Simba Queens imezidi kujisafishia njia ya ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara msimu huu baada ya leo, Ijumaa, Mei 15, 2026 kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Watani wao wa Jadi, Yanga katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salam.
Mabao mawili ya mshambuliaji wa Simba Queens, Jentrix Shikangwa yametosha kuipa ushindi huo dhidi ya Yanga Princess ulioifanya iendelee kuusogelea ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake msimu huu ikifikisha pointi 46.
Pointi hizo ni saba zaidi ya zile za Yanga Princess iliyo katika nafasi ya pili na JKT Queens iliyopo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Shikangwa aliandika bao la kwanza katika dakika ya 19 akitumia vyema nafasi iliyotengenezwa na Vivian Corazone kabla ya kuongeza la pili katika dakika ya 37 na kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Yanga Princess walirejea kipindi cha pili wakionyesha mabadiliko ya kiuchezaji huku benchi la ufundi likifanya mabadiliko ya mapema kwa kumtoa Aregash Kalsa dakika ya 45 na kumuingiza Diana Mnally.
Dakika ya 49 Lydia Akoth naye aliingia kuchukua nafasi ya Asha Djafar katika jitihada za kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji.
Mabadiliko hayo yaliwapa uhai Yanga Princess na dakika ya 57 wakapata bao kupitia kwa Ritticia Nabbosa.
Licha ya Yanga kucheza vizuri kipindi cha pili na kupeleka presha langoni mwa wapinzani wao, Simba walisimama imara na kufanikiwa kuondoka na pointi tatu muhimu zilizoendelea kuwaweka kileleni.
Katika mchezo huo Simba Queens ilianza na Ruth Aturo, Zanga Brice, Ruth Ingosi, Fasila Adhiambo, Zainah Nandede, Elizabeth John, Asha Omary, Elizabeth Wambui, Vivian Corazone, Aisha Mnunka na Jentrix Shikangwa.
Yanga Princess ilianza na Rita Akarekor, Igwe Uzoamaka, Jeaninne Mukandayisenga, Aregash Kalsa, Wincate Kaari, Ester Akudo, Precious Christopher, Agnes Pallangyo, Ester Mabanza, Asha Djafar na Ritticia Nabbosa