Simba yaichapa Coastal Union, yakaa nafasi ya pili
Winga wa kulia wa Simba, Libase Gueye wakati akijaribu kumtoka mchezaji wa Coastal Union katika mechi ya Ligi Kuu iliopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Simba ikishinda 2-0 Aprili 2, 2026. Picha na Simba
Muktasari:
- Simba inajiandaa na mchezo ujao wa Dabi ya Mzizima dhidi ya Azam utakaopigwa Jumapili ujao kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Dar es Salaam. Simba imefanikiwa kusogea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kuibuka na uahindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union.
Huu ulikuwa mchezo wa kwanza kwa timu hizo msimu huu, lakini ikiwa mechi muhimu kwa timu zote mbili zikiwa na malengo tofauti, Simba ikijipanga kuwania ubingwa huku Coastal ikipambana kutoka mkiani.
Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Meja Isamuhyo, Simba ilifanikiwa kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao mawili.
Mabao ya Simba yaliwekwa kimiani na mshambuliaji Seleman Mwalimu pamoja na beki wa kati Toure likiwa ni la kwanza kwake tangu ajiunge na timu hiyo.
Mshambuliaji wa Simba, Seleman Mwalimu wakati akifunga bao la kuongoza katika ushindi wa 2-0 iliopata Simba dhidi ya Coastal Union katika mechi ya Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, Aprili 2, 2026. Picha na Simba
Hili ni bao la sita kwa Mwalimu msimu huu akifunga kwenye michezo miwili mfululizo.
Ushindi huu umeifanya Simba kusogea hadi nafasi ya pili ikiwa na pointi 34 iko pointi nne dhidi ya vinara Yanga lakini yenyewe ikiwa na faida ya mchezo mmoja.
Kwa upande wa Coastal mambo kwao siyo mazuri msimu huu ikiwa na pointi 15 baada ya michezo 17, ikiwa nafasi ya 13 kwenye msimamo.
Sasa Simba inajiandaa na mchezo ujao wa Dabi ya Mzizima dhidi ya Azam utakaopigwa Jumapili ujao kwenye Uwanja wa Azam Complex.