Simba yalala kwa Esperance ikitegemea miujiza robo fainali
Muktasari:
- Simba imefunga bao moja tu katika mechi tatu za mwanzo za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Dar es Salaam. Matumaini ya Simba kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu yamezidi kuwa magumu baada ya leo kupokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Esperance katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Olimpiki wa Rades, Tunisia.
Kichapo hicho kimeifanya Simba izidi kushika mkia katika msimamo wa kundi D ikiwa haina pointi huku Esperance ikifikisha pointi tano zilizoisogeza hadi nafasi ya kwanza.
Bao pekee la Esperance katika mchezo wa leo limepachikwa na Jack Diarra katika dakika ya 21 akimalizia pasi ya Ben Hamida.
Matokeo hayo yanaifanya Simba sasa kutegemea miujiza ili itinge hatua ya robo fainali kwani inatakiwa angalau kuibuka na ushindi katika mechi zake tatu zilizobakia kwenye kundi hilo na pia kuombea matokeo ya mechi nyingine zitakazohusisha timu za Esperance, Stade Malien na Petro Luanda yawe yenye faida kwa upande wao.
Mbali na matokeo hayo kuiweka rehani ndoto ya Simba kucheza robo fainali, yameifanya pia iandike rekodi mbaya ya kucheza mechi tatu mfululizo za hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika bila kupata pointi.
Simba imevunja rekodi yake yenyewe ya msimu wa 2022/2023 ambapo katika mechi tatu za mwanzo za hatua ya makundi, ilipoteza mbili na kushinda moja.
Katika mchezo wa leo, Simba iliwaanzisha nyota wake wawili ambao imewasajili katika dirisha dogo la usajili, Nickson Kibabage na Mahamadou Tanja waliochukua nafasi za Anthony Mligo na Hussein Abel.
Baada ya mchezo wa leo, timu hizo zinatarajiwa kurudiana Dar es Salaam katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Februari Mosi mwaka huu.