Simba yamcharukia Dejan kuvunja mkataba, yaahidi kumchukulia hatua

Simba yamcharukia Dejan kuvunja mkataba, yaahidi kumchukulia hatua

Muktasari:

  • BAADA ya aliyekuwa mshambuliaji wa Simba Mserbia Dejan Georgijevic jana Septemba 28, 2022 kutangaza kuvunja mkataba na klabu hiyo kwa kile alichodai kukiukwa kwa matakwa ya kimkataba, Uongozi wa timu hiyo umevunja ukimya na kueleza utamshughulikia.

BAADA ya aliyekuwa mshambuliaji wa Simba Mserbia Dejan Georgijevic jana Septemba 28, 2022 kutangaza kuvunja mkataba na klabu hiyo kwa kile alichodai kukiukwa kwa matakwa ya kimkataba, Uongozi wa timu hiyo umevunja ukimya na kueleza utamshughulikia.

Taarifa rasmi kutoka kwa Simba inaeleza kutofurahishwa na kitendo cha staa huyo kueleza kuvunja mkataba bila ya makubaliano ya pande zote mbili.

Simba imeandika; "Uongozi wa klabu ya Simba umepokea taarifa ya mchezaji Dejan ya kuvunja mkataba na klabu yetu.

Hata hivyo tumesikitishwa na kitendo cha Dejan kuandika taarifa ya kuvunja mkataba kupitia mitandao ya kijamii bila hata ya kufanya mazungumzo na waajili wake.

Uongozi utachukua hatua stahiki juu ya mchezaji huyo kufuatia kuvunja mkataba bila kufuata utaratibu maalumu," ilieleza taarifa ya Simba.

Simba leo itarejea Dar es Salaam ikitokea Zanzibar ilikoenda kucheza mechi mbili za kirafiki ikishida 1-0 dhidi ya Malindi na 3-0 mbele ya Kipanga, timu zote za Ligi Kuu Zanzibar.