SIO ZENGWE: Mameneja wa Fei Toto hawastahili malipo

NI kitu kibaya sana kwangu kuzungumzia sakata moja kwa wiki mbili mfululizo, lakini nimelazimika kufanya hivyo kutokana na umuhimu wake.
Hakuna siri kwamba sakata la Feisal Salum 'Fei Toto' ni moja ya matukio makubwa yatakayokumbukwa mwaka huu, na kama ingekuwa ni nchi za wenzetu, lingeangaliwa kwa mapana yake na marefu ili kuboresha zaidi kanuni za mikataba ya wachezaji ya ndani ya nchi na ingepewa jina la Kanuni ya Fei Toto.
Ni kweli Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) lina muongozo wake wa sheria ya wachezaji unaohusu maslahi yake na uhamisho wake, lakini hiyo haimaanishi kuwa nchi isiwe na sheria zake kulingana na mazingira yake.
Mfano ni suala la mchezaji kununua mkataba. Wakati Fifa imeweka vipengele vya kuzingatia kabla ya mchezaji kuvunja mkataba kwa kulipa malipo yalioainishwa, nchini Hispania klabu inayomtaka mchezaji inapeleka malipo hayo yaliyoanishwa kwenye mkataba, kwa La Liga ambao baadaye huitaarifu klabu inayommiliki mchezaji kwamba ameshalipiwa malipo ya kumnunua mchezaji na hivyo yuko huru kuanza mazungumzo binafsi.
Hii inatokana na sheria za mikataba ya kazi za Hispania.
Ni dhahiri kwamba hata La Liga wana vipengele kadhaa vya kuvikidhi kabla ya klabu inayomhitaji mchezaji kufikia uamuzi wa kupeleka malipo yake La Liga. Ndivyo ilivyofanyika kwa Thomas Partey wakati Arsenal ilipomnunuia, lakini ikashindikana kwa Luis Suarez wakatui Arsenal ilipotaka kulipia buy out clause wakati akiwa Liverpool. Kwa kifupi suala hilo limekuwa na changamoto nchini England.
Kwa hiyo, suala la Fei Toto linaweza kuibua mengi kuhusu mikataba ya wachezaji kama vyombo husika havitaishia kuliona limepita na kusubiri mengine mapya yatokee ili yazungumzwe juujuu kabla ya kuchukuliwa na wimbi la upepo na kupotea.
Umuhimu mwingine naouona hapa ni jinsi wachezaji wanavyoweza kufanya kazi na wawakilishi wao au mameneja. Kwa kawaida mameneja ndio wanaotakiwa kufanya kazi yote ya kujadiliana mikataba ya wachezaji, maslahi yao, maisha yao, uhamisho na utatuzi wa migogoro baina ya wachezaji na klabu.
HJii huwafanya wachezaji waendelee kuweka akili yote katika kazi yake ya kucheza mpira hadi makubaliano yanapofikiwa. Mwisho mwa msimu uliopita, Real Madrid ilikuwa inakaribia kunasa saini ya mshambuliaji wa Real Madrid, Kylian Mbappe, ambaye alikuwa anasemekana kuwa ndoto yake siku moja na kuchezea vigogo hao wa Hispania.
Karibu kila sentensi ya Mbappe ilihjusishwa na mpango huo, lakini haikuwa kauli yake ya moja kwa moja kwamba ameamua kwenda Real Madrid. Hali ilikuwa hivyo hadi iliposemekana kuwa amebadili uamuzi na anabakia Paris Saint Germain (PSG).
Kama Mbappe angenukuliwa akisema kwamba hafurahii maisha yake PSG na kwamba anataka kwenda Real Madrid ambako angecheza kwa dhati ya moyo wake, leo hii angekuwa anaangaliwa vibaya PSG. Kila kosa ambalo angefanya lingetafsiriwa kuwa lilitokana na kutocheza kwa dhati ya moyo wake.
Ndio maana wachezaji hujizuia kutoa matamko yoyote kuhusu usajili wao hadi pale unapokamilika na kusaini mkataba na klabu nyiongine. Kazi ya kujadiliana maslahi na kuangalia sehemu nyingine anayoweza kwenda yanabakia kuwa kwa meneja wake. Na hata meneja wake huwa hatoi kauli yoyote.
Kinachoripotiwa na vyombo vya habari kuhusu matamanio ya mchezaji ni kauli ambazo aliwahi kutoa katika mahojiano kwamba siku moja angefurahia kuchezea klabu fulani, au mazungumzo na rafiki zake kuhusu maisha yake ya baadaye.
Lakini mameneja, au mawakala au wawakilishi wa Fei Toto walijificha nhyuma yake. Badala ya wawakilishi hao kujihusisha na mazungumzo na klabu ya Yanga kuhusu kuboresha mkataba au ofa walizopata kutoka klabu nyingine zenye maslahi bopra zaidi, wao walijificha nyuma ya Fei Toto.
Walitaka Fei Toto ndio ajitoe muhanga. Anunue mkataba na kuandika barua kuwa anavunja mkataba na kuaga wana-Yanga kwa kutumia Instagram. Hawakuwa wamemuonyesha vikwazo vya kimkataba anavyoweza kukumbana navyo na jinsi ambavyo angeweza kuepuka.
Badala yake wakamuachia Fei Toto awe sterling wa filamu yake mwenyewe, acheze sehemu za hatari (stuns) kama za kuruka kutoka ghorofa refu, na awe promota wa filamnu hiyo.
Wao walienda getini kusubiri mapato ya filamu ambayo hawakuitunga, kushiriki kuchukua picha wala kuigiza. Walitaka kunufaika na donge nono la uhamisho bila ya kutoa jasho. Na mpango huo ungefanikiwa, vijiweni wangekuwa wanajisifu jinsi walivyomshauri kucheza filamu hadi sehemu za hatari.
Binafsi, nisingekuwa tayari kugawana malipo na mameneja wa aina hiyo. Mameneja waliotaka mchezaji apigane vita vyake mwenyewe na kuhatarisha maisha yake, huku wao wakisubiri donge nono la usajili ambalo wangepata katika mkataba mpya wa Fei Toto.
Hili ni suala ambalo wachezaji wengi hawana budi kuliangalia na kujifunza. Si kazi ya mchezaji kufanya mazungumzo na klabu yake kuhusu maslahi. Mambo hayo yalishapitwa na wakati. Ni suala la wawakilishi wake kufanya mazungumzo na klabu kwa kuzingatia vitu vingi kabla ya kusaini mkataba.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imesema inaonekana wachezaji wengi wanasaini mikataba bila ya kusoma vipengele vyote. Nadhani si rahisi mchezaji kusoma vipengele vyote vya mkataba, bali wasimamizi wake kuangalia kila kitu muhimu na kumuelewesha mchezaji kabla ya kusaini.
Kuna mchezaji aliwahi kuniomba niuangalie mkataba wake ulioandikwa Kifaransa. Nikamtafsiria kwa kuwa haukuwa umeandikwa kisheria. Mwishoni nilimsisitizia kipengele kimoja ambacho kingemuweka matatani na ndipo alipoamua kutokwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kujiunga na timu iliyokuwa inamtaka.
Kwa hiyo, wasimamizi wa wachezaji ndio wanaopaswa kufanya majadiliano na klabu na baadaye kumuelewesha mchezaji yaliyokubaliwa na ambayo yatakuwemo kwenye mkataba. Akisaini mkataba mbovu, tatizo kwa nje litaonekana la mchezaji, lakini kwa ndani itakuwa ni msimamizi wake au meneja au wakala.
Na tatizo likiwa ni msimamizi wa aina hiyo, kuna haja ya kumlipa? Hakuna. Na kama msimamizi huyo alitaka mchezaji ajitoe muhanga kulazimisha kuachwa na akafanikiwa na baadaye kusajiliwa klabu nyingine kwa donge nono, kuna haja ya kumlipa msimamizi kama picha yote kacheza mchezaji?
Ndio maana nasema kama suala la Fei Toto lilihusisha mwakilishi, wakala au meneja, basi hastahili malipo yoyote ya mkataba mpya wa mchezaji huyo kama atasalia Yanga au huko atakakokwenda.
Hii ni kwa sababu Fei Toto ndiye aliyeachwa aharibu, aliyeachwa amwage mboga, aliyeachwa ajizungumzie huku wengine wakisubiri mapato mlangoni.
Hii haifai na ni somo zuri kwa wachezaji kwamba kila wanapoona mameneja wao wanawasukuma wachukue hatua ngumu kulazimisha malipo bora, wajue kuwa hakuna meneja hapo.
Meneja wa kweli atamwambia mchezaji aendelee kufanya kazi yake, huku yeye akiendelea na mazungumzo hadi yuatakaposhindikana.