Skudu Makudubela aagana na AS Vita

Muktasari:
- Skudu aliwahi kuitumikia Yanga akiweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Afrika Kusini kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mchezaji wa soka kutoka Afrika Kusini, Mahlatsi Makudubela, maarufu kama Skudu, ameagana rasmi na klabu ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, akifunga pazia la safari yake ya soka iliyosheheni uhamisho wa mara kwa mara.

Makudubela, ambaye ameshawahi kuchezea klabu 15 tofauti katika karia yake ya soka, sasa anakuwa mchezaji huru na tayari dalili zinaonesha kuwa anaweza kuhamia timu nyingine kuendelea na maisha yake ya soka.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Makudubela ameandika:
“Muda wangu na AS Vita umefikia tamati. Nina mengi ya kusema lakini nitaamua kusema machache. Napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru aliyekuwa Rais wa Klabu, Bwana Amadou Diaby.
“Kipindi kifupi nilichokaa Vita kimekuwa na mafunzo mengi... na mimi binafsi nimejifunza mambo mengi,” amesema Makudubela.

Akiwa na Vita, Makudubela alionesha ushindani mkubwa katika mechi alizocheza, na aliambulia tuzo mbalimbali za mchezaji bora wa mechi pamoja na kumbukumbu za kipekee kutoka vyumbani, uwanjani na hata akiwa safarini na kikosi cha timu hiyo kutokana na ucheshi wake.

Skudu ambaye aliwahi kuitumikia Yanga katika msimu wa 2023/2024 alitumika katika michezo kadhaa huko Jangwani ambapo aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Afrika Kusini kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara.

Alijiunga na Yanga akiwa mchezaji huru Julai 2023 akitokea Marumo Gallants ya Afrika Kusini na msimu huo aliisaidia timu yake kutetea ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la CRDB.