Taharuki yatanda tiketi zaibua mjadala
Muktasari:
- Licha ya changamoto hizo, Kombe la Dunia 2026 linatarajiwa kuchezwa kwa siku 38 likiwa na jumla ya mechi 104 kutokana na kuongezeka kwa timu kutoka 32 hadi 48.
Mexico City, Mexico. Mashindano ya Kombe la Dunia 2026 yanatarajiwa kuanza rasmi leo kwa mchezo wa ufunguzi kati ya Mexico na Afrika Kusini kwenye Uwanja wa Azteca jijini Mexico City, lakini maandalizi ya tukio hilo yamegubikwa na changamoto mbalimbali za kisiasa, kiusalama na kiutawala.
Katika mechi hiyo ambayo ni marudio ya mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia 2010, hamasa miongoni mwa mashabiki imekuwa kubwa, lakini mjadala mkubwa umekuwa ukihusu maandamano, gharama kubwa za tiketi na matatizo ya viza kwa baadhi ya mashabiki, waandishi wa habari na hata maofisa wa mashindano.
Mexico imeandika historia kwa kuwa taifa la kwanza duniani kuandaa mechi za Kombe la Dunia katika matoleo matatu tofauti baada ya kufanya hivyo mwaka 1970 na 1986. Hata hivyo, shamrashamra hizo zimekwenda sambamba na maandamano makubwa yanayoendelea jijini Mexico City.
Baadhi ya makazi ya muda 'Mahema' ambayo yamewekwa na waandamanaji Mexico City. Picha na Mtandao
Miongoni mwa wanaoandamana ni wanachama wa Chama cha Walimu cha Coordinadora Nacional de Trabajadores de la Educacion (CNTE), wanaopinga masuala ya mishahara, pensheni na mageuzi ya sheria za kazi.
Maelfu ya walimu hao wamekuwa wakifanya maandamano kwa zaidi ya wiki moja na kuweka makazi ya muda ‘mahema’ katika eneo ambalo limechukua sehemu kubwa jijini Mexico City na liko jirani na eneo rasmi la mashabiki wa Kombe la Dunia.
Waandamanaji hao wanadai Rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum, ameshindwa kutekeleza ahadi alizozitoa kwa walimu, hivyo wameamua kutumia jukwaa la Kombe la Dunia kuibua mjadala kuhusu changamoto zinazolikabili taifa hilo.
Kutokana na ukaribu wa eneo hilo na sehemu ya mashabiki, mamlaka zimeongeza ulinzi na kuweka vizuizi vya usalama.
Mbali na walimu, wakulima, wafanyakazi wa sekta ya usafiri pamoja na familia za watu waliopotea pia wamekuwa wakitumia mwangaza wa Kombe la Dunia kuwasilisha madai yao.
Makundi ya mazingira na haki za binadamu nayo yamefanya maandamano yakipinga athari za mazingira zinazotokana na mashindano hayo yanayofanyika katika miji 16 na nchi tatu tofauti.
Wakati huohuo, baadhi ya wananchi wa Mexico wameonyesha kutoridhishwa na gharama za kuandaa mashindano hayo, wakisema fedha hizo zingeweza kuelekezwa katika kutatua matatizo ya kijamii na kiuchumi yanayoikabili nchi hiyo.
Baadhi ya raia wa Mexico wakiwa katika mitaa ya jiji la Mexico City wakiikosoa Serikali. Picha na Mtandao
Gharama za tiketi zaibua mjadala mkubwa.
Licha ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kusisitiza kuwa mahitaji ya tiketi bado ni makubwa, taarifa zinaonyesha takribani tiketi 180,000 za hatua ya makundi bado hazijanunuliwa katika majukwaa rasmi ya mauzo.
Kwa mujibu wa Financial Times, tiketi 4,400 za mchezo wa kwanza wa Marekani dhidi ya Paraguay zilikuwa bado hazijauzwa, huku tiketi ya bei nafuu ikigharimu dola 1,120 za Marekani (Sh2.9 milioni).
Baadhi ya Askari Polisi jijini Mexico wakijaribu kuwatuliza waandamanaji waliojitokeza katika maeneo mbalimbali jijini humo. Picha na Mtandao
Mbali na gharama za tiketi, mashabiki wamekuwa wakilalamikia gharama za usafiri na malazi katika nchi tatu zinazoshiriki kuandaa mashindano hayo.
Changamoto nyingine imekuwa ni masuala ya viza na vibali vya kuingia Marekani, ambapo baadhi ya mashabiki, waandishi wa habari na maofisa wa mashindano wamekumbana na vikwazo mbalimbali.
Miongoni mwa walioathirika ni mwamuzi kutoka Somalia, Omar Artan, ambaye aliondolewa katika orodha ya waamuzi wa Kombe la Dunia baada ya kuzuiwa kuingia Marekani alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Miami.
Artan, anayehesabiwa miongoni mwa waamuzi bora barani Afrika, amesema amevunjika moyo kutokana na uamuzi huo.
Mwamuzi kutoka Somalia, Omar Artan, ambaye aliondolewa katika orodha ya waamuzi wa Kombe la Dunia
“Nilikuwa natimiza ndoto kubwa ya maisha yangu ya kushiriki Kombe la Dunia, lakini sasa nimeondolewa,” amesema mwamuzi huyo.
Mataifa kama Iran na Haiti pia yameathiriwa na vikwazo vya usafiri vya Marekani, huku Shirikisho la Soka la Iran likidai baadhi ya maofisa wake wamenyimwa viza na mgao wa tiketi kwa mashabiki wao kufutwa.
Kutokana na hali hiyo, Iran imelazimika kuhamisha kambi yake kutoka Arizona kwenda Mexico muda mfupi kabla ya kuanza kwa mashindano.
Hali hiyo imewafanya baadhi ya wachambuzi kuelezea Kombe la Dunia la 2026 kuwa miongoni mwa mashindano yenye mvutano mkubwa wa kisiasa katika historia yake.
Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino wakati akizungumzia bei za tiketi. Picha na Mtandao
Akizungumzia ukosoaji unaoendelea kuhusu viza, bei za tiketi na usalama, Rais wa FIFA, Gianni Infantino, amewataka wakosoaji kutulia na kueleza kuwa maamuzi ya uhamiaji yapo mikononi mwa serikali husika na si shirikisho hilo.
“Hatuishi mwezini, tunaishi duniani. FIFA si watawala wa dunia ambao wanaweza kuamuru serikali na vyombo vya usalama. Wakati mwingine ni muhimu kutulia na kupumzika, kwa sababu kelele pekee hazileti suluhisho,” amesema Infantino.
Licha ya changamoto hizo, Kombe la Dunia 2026 linatarajiwa kuchezwa kwa siku 38 likiwa na jumla ya mechi 104 kutokana na kuongezeka kwa timu kutoka 32 hadi 48.