Timu nane Afrika hesabu zinakubali Kombe la Dunia
Muktasari:
- Katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu huko Marekani, Canada na Mexico, Afrika inawakilishwa na timu 10 ambazo ni Ivory Coast, Senegal, Morocco, Tunisia, Algeria, Misri, Afrika Kusini, Cape Verde, Ghana na DR Congo.
Wawakilishi nane wa Afrika kwenye Kombe la Dunia, wanaweza kutinga hatua ya mtoano ya 32 ikiwa mambo yatawanyookea katika mechi za mwisho za hatua ya makundi.
Timu hizo ni Morocco, DR Congo, Algeria, Ghana, Cape Verde, Misri, Afrika Kusini na Ivory Coast.
DR Congo ambayo kesho kuanzia saa 11:00 alfajiri kwa saa za Afrika Mashariki itakuwa na mchezo dhidi ya Colombia, inayo nafasi ya kwenda 32 bora moja kwa moja au kutegemea nafasi moja kwenye kundi la timu nane zinazofuzu kwa kuwa na matokeo bora zikiwa zimeshika nafasi ya tatu kwenye makundi.
Kabla ya mchezo dhidi ya Colombia, DR Congo iliyo katika kundi K, ina pointi moja.
Morocco inahitaji angalau sare tu katika mechi ya mwisho ya kundi C dhidi ya vibonde Haiti, iweze kusonga mbele kwani ina pointi nne hivi sasa huku Afrika Kusini ikiwa na kibarua cha kuichapa Korea Kusini katika mechi ya mwisho na kuombea Jamhuri ya Czech isipate ushindi dhidi ya vinara wa kundi A, Mexico.
Kama Czech itashinda, Afrika Kusini inaweza kupita kwa mgongo wa 'viti maalum' ikiwa itashinda dhidi ya Korea Kusini, kwani itafikisha pointi nne zinazoweza kuifanya iingie katika kundi la timu nane zilizofanya vizuri katika nafasi ya tatu.
Katika Kundi E, Ivory Coast itafuzu 32 bora ikiwa itaichapa, Curacao na ikitoka sare inaweza kusonga mbele kupitia mlango wa uwani wakati Misri inahitaji angalau sare tu katika mechi ya mwisho dhidi ya Iran ili ipenye kupitia kundi G kwa vile sasa inaongoza ikiwa na pointi nne.
Cape Verde ina nafasi ya kufuzu kupitia kundi H ikiwa itapata ushindi katika mechi ya mwisho dhidi ya Saudi Arabia ambapo itafikisha pointi tano na Algeria yenye pointi tatu, itafuzu ikiwa itaichapa Austria katika mechi ya mwisho ya kundi J.
Ghana ambayo leo itakabiliana na England, itafuzu kupitia kundi L iwapo itaibuka na ushindi leo au dhidi ya Croatia katika mechi ya mwisho.
Senegal iliyopoteza mechi mbili za mwanzo za kundi I dhidi ya Ufaransa na Norway, inategemea miujiza tu ya kupenya kupitia nafasi ya kundi la timu nane zenye matokeo mazuri katika nafasi ya tatu iwapo itashinda mechi ya mwisho dhidi ya Iraq na kuziombea mabaya timu za makundi mengine na Tunisia imeshaaga mashindano hayo.