Prime
Tuzo Bara ni Ahoua, Pacome

Muktasari:
- Nyota hao wote ni raia wa Ivory Coast na huko walikotoka walifanikiwa kubeba Tuzo ya MVP kabla ya kutua Tanzania wakitokea klabu za nyumbani kwao.
Jana ilikuwa fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) iliyofanyika kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ambapo Yanga ilicheza dhidi ya Singida Black Stars.
Ni mchezo wa kufunga msimu wa 2024-2025 kwa timu hizo ambapo baada ya hapo kutakuwa na kipindi cha maandalizi kuelekea msimu ujao.
Wakati wa maandalizi ya kuelekea msimu ujao, hapo kati kutakuwa na mambo mengi ikiwemo michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (Chan) itakayofanyika Tanzania Kenya na Uganda.
Lakini usisahau kutakuwa na zoezi la utoaji Tuzo za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zikihusisha vipengele tofauti kuanzia Ligi Kuu Bara, Ligi Kuu Wanawake, Championship na Kombe la FA.
Upande wa Ligi Kuu Bara, msimu huu kumekuwa na mvutano mkubwa wa baadhi ya tuzo nani anastahili kuwa mshindi, huku zingine zikionekana wazi itabebwa na nani.
Mvutano mkubwa upo kwa Mchezaji Bora (MVP) wa Ligi Kuu Bara.
Majina yanayotajwa zaidi ni Pacome Zouzoua wa Yanga na Jean Charles Ahoua anayecheza Simba.
Nyota hao wote ni raia wa Ivory Coast na huko walikotoka walifanikiwa kubeba Tuzo ya MVP kabla ya kutua Tanzania wakitokea klabu za nyumbani kwao.
Pacome huu ni msimu wa pili anacheza Yanga, alitua 2023-2024 akitokea ASEC Mimosas wakati Ahoua aliyetokea Stella Club d'Adjamé, wote wamefanya vizuri kila mmoja kwa nafasi yake.
Ahoua ukiwa ni msimu wake wa kwanza, ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu akipachika mabao 16, pia ana asisti 9 hivyo amehusika kwenye mabao 25 kati ya 69 yaliyofungwa na Simba.
Pacome amefunga mabao 12 na asisti 10, amehusika kwenye mabao 22 kati ya 83 yaliyofungwa na Yanga kwenye ligi.
Mvutano wa nani MVP wa msimu huu kila mmoja anatoa vigezo vyake, lakini mwisho wa siku kamati ya Tuzo za TFF itamaliza utata huo.
Lakini wakati wengi wakimpigia chapuo Ahoua na Pacome katika suala la MVP, hali imekuwa tofauti kwa Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Masanza anayesema Jonathan Sowah anastahili kubeba tuzo hiyo.
Masanza anasema Sowah ambaye ametua Singida Black Stars kipindi cha dirisha dogo msimu huu, ndiye anayestahili kuwa MVP kutokana na kufanya mambo makubwa ndani ya muda mfupi.
Kuanzia Januari hadi Juni ligi ilipofikia tamati ambapo ni takribani miezi sita, mshambuliaji huyo raia wa Ghana amefunga mabao 13, akiwa matatu na mfungaji bora.
"Watu wanawataja Pacome na Ahoua, lakini binafsi namuona Sowah anastahili tuzo ya MVP kwa sababu ameingia dirisha dogo na amefanya mambo makubwa. Namba zake zinaongea," anasema Masanza.
Hata hivyo, Masanza hakusita kuukubali uwezo wa Pacome na Ahoua akiwataja katika nyota sita bora aliowaona wamefanya vizuri msimu huu.
"Namba moja ni Sowah ambaye anastahili kuwa MVP, kisha anafuatia Elvis Rupia, Pacome Zouzoua, Jean Charles Ahoua, Prince Dube na Feisal Salum," amesema Masanza.
Ukiweka kando hilo, tuzo zingine zinaonekana wazi ni ufungaji bora ambayo haina mpinzani, Ahoua anabeba kwa kumaliza na mabao 16, lakini kuna utata wa kipa bora, wanaosema anastahili Moussa Camara wa Simba wanaangalia kigezo cha clean sheet ambapo amemaliza na 19, wanaopinga hilo wanadai kipa bora asipimwe kwa clean sheet bali mchango wake katika kuisaidia timu kufanya vizuri.
Djigui Diarra wa Yanga amemaliza na clean sheet 17, huku akichangia ubingwa wa ligi uliobebwa na timu hiyo kwa msimu wa nne mfululizo.
Ukiangalia hadi hapo, tuzo zinazojadiliwa zaidi zinawahusu wachezaji wa kigeni, huku wazawa wakionekana kupigwa bao na hii imekuwa ikitokea msimu hadi msimu.
Katika misimu mitano iliyopita kuanzia 2019-2020 hadi 2023-2024, wageni wametawala zaidi kwenye Ufungaji Bora, MVP, Kiungo Bora, Kocha Bora na Kipa Bora.
Ipo hivi; Upande wa kipa bora, wageni wamechukua mara tatu dhidi ya mbili za wazawa ndani ya misimu hiyo mitano.
Tuzo ya Kocha Bora ndiyo balaa kwani mara zote tano imeenda kwa wageni, hii kwa kiasi kikubwa imechangiwa na wazawa kwa misimu ya karibuni kutopenya katika kuzinoa timu zinazomaliza nafasi za juu kwenye msimamo, Yanga, Simba na Azam.
Ukiangalia katika misimu hiyo mitano, Yanga na Simba pekee ndiyo zimetoa makocha bora.
Tuzo ya kiungo bora nayo imebebwa na wageni mara zote tano hizo.
Ufungaji bora ndani ya misimu mitano nyuma wageni wamechukua mara tatu, wazawa mbili, wakati ile ya kipa bora mzawa aliyeshinda mmoja pekee, ambaye ni Aishi Manula lakini amefanya hivyo mara mbili.
Wazawa wanatamba kwenye tuzo ya mchezaji chipukizi, hii inachangiwa zaidi na jinsi wageni wanaokuja kucheza soka Tanzania umri umesogea kidogo kulinganisha na chipukizi wetu.
Sehemu pekee wazawa wamefanya kweli misimu mitano ni upande wa tuzo ya beki bora, wamebeba tatu na wageni mbili.
Kwa msimu huu 2024-2025 hali itakuwaje kwa jumla. Ngoja tuone.
Tazama hapa ilivyokuwa misimu mitano ya Ligi Kuu Bara kuanzia 2019-2020 hadi 2023-2024 namna wazawa walivyopambana na wageni katika tuzo za TFF.
2023-2024
Mchezaji Bora
Stephane Aziz KI – Ivory Coast (Yanga)
Kiungo Bora
Stephane Aziz KI – Ivory Coast (Yanga)
Mfungaji Bora
Stephane Aziz KI – Ivory Coast (Yanga)
Beki Bora
Ibrahim Bacca – Tanzania (Yanga)
Kipa Bora
Ley Matampi – DR Congo (Coastal Union)
Mchezaji Chipukizi
Raheem Shomary – Tanzania (KMC)
Bao Bora
Kipre Junior – Ivory Coast (Azam)
Kocha Bora
Miguel Gamondi – Argentina (Yanga)
2022-2023
Mchezaji Bora
Fiston Mayele – DR Congo (Yanga)
Kiungo Bora
Saido Ntibazonkiza – Burundi (Simba)
Mfungaji Bora
Fiston Mayele & Saido Ntibazonkiza
Beki Bora
Dickson Job – Tanzania (Yanga)
Kipa Bora
Djigui Diarra – Mali (Yanga)
Mchezaji Chipukizi
Lameck Lawi – Tanzania (Costal Union)
Bao Bora
Fiston Mayele – DR Congo (Yanga)
Kocha Bora
Nasreddine Nabi – Tunisia (Yanga)
2021-2022
Mchezaji Bora
Yannick Bangala – DR Congo (Yanga)
Kiungo Bora
Yannick Bangala – DR Congo (Yanga)
Mfungaji Bora
George Mpole – Tanzania (Geita Gold)
Beki Bora
Henock Inonga Baka – DR Congo (Simba)
Kipa Bora
Djigui Diarra – Mali (Yanga)
Mchezaji Chipukizi
Dickson Mhilu – Tanzania (Kagera Sugar)
Bao Bora
Fiston Mayele – DR Congo (Yanga)
Kocha Bora
Nasreddine Nabi – Tunisia (Yanga)
2020-2021
Mchezaji Bora
John Bocco – Tanzania (Simba)
Kiungo Bora
Clatous Chama – Zambi (Simba)
Mfungaji Bora
John Bocco – Tanzania (Simba)
Beki Bora
Mohamed Hussein – Tanzania (Simba)
Kipa Bora
Aishi Manula – Tanzania (Simba)
Mchezaji Chipukizi
Abdul Sopu – Tanzania (Costal Union)
Bao Bora
Lambart Sabiyanka – Tanzania (Prisons)
Kocha Bora
Didier Gomes Da Rosa – Ufaransa (Simba)
2019-2020
Mchezaji Bora
Clatous Chama – Zambia (Simba)
Kiungo Bora
Clatous Chama – Zambia (Simba)
Mfungaji Bora
Meddie Kagere – Rwanda (Simba)
Beki Bora
Nicholas Wadada – Uganda (Azam)
Kipa Bora
Aishi Manula – Tanzania (Simba)
Mchezaji Chipukizi
Novatus Dismas – Tanzania (Biashara United)
Bao Bora
Patson Shigala – Tanzania (Mbeya City)
Kocha Bora
Sven Vandenbroeck – Ubelgiji (Simba)