Udhaifu wa Jwaneng njia ya Simba Robo fainali

Muktasari:

  • Simba inayoshika nafasi ya pili kwenye kundi B, ikiwa na pointi sita, inahitaji ushindi katika mechi hiyo ili iweze kufuzu hatua ya robo fainali ya mashindano hayo na kuungana na Asec Mimosas ya Ivory Coast ambayo tayari imeshasonga mbele na kujihakikishia uongozi wa kundi hilo.

Udhaifu wa safu ya ulinzi na ubutu wa safu ya ushambuliaji ya Jwaneng Galaxy ni mambo mawili yanayoweza kuwa faida kwa Simba katika mechi baina yao, Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambayo itachezwa kuanzia saa 1:00 usiku.

Simba inayoshika nafasi ya pili kwenye kundi B, ikiwa na pointi sita, inahitaji ushindi katika mechi hiyo ili iweze kufuzu hatua ya robo fainali ya mashindano hayo na kuungana na Asec Mimosas ya Ivory Coast ambayo tayari imeshasonga mbele na kujihakikishia uongozi wa kundi hilo.

Jwaneng Galaxy inayoshika mkia katika kundi hilo ikiwa na pointi nne, imekuwa na safu dhaifu ya ulinzi ambayo katika mechi tatu zilizopita za hatua ya makundi imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita ikiwa ni wastani wa mabao mawili kwa kila mechi.

Licha ya kutoruhusu bao katika mechi mbili za mwanzo dhidi ya Wydad na Simba, ilijikuta ikifungwa mabao 2-0 nyumbani na Asec Mimosas kisha ziliporudiana ikafungwa mabao 3-0 na katika mechi ya juzi ikafungwa bao 1-0 na Wydad.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Jwaneng, Simba yenyewe safu yake ya ulinzi imeruhusu mabao mawili tu katika mechi tano za kundi hilo, ambapo bao la kwanza ilifungwa dhidi ya Asec Mimosas kwenye mechi ya kwanza na lingine ikafungwa dhidi ya Wydad kwenye mechi ya tatu.

Ubutu wa safu ya ushambuliaji ya Jwaneng Galaxy unaweza kuipa Simba tumaini lingine katika mechi hiyo ambayo ushindi wa aina yoyote utaifanya itinge hatua ya robo fainali pasipo kuathirika na matokeo ya mchezo baina ya Wydad na Asec Mimosas.

Katika mechi tano za hatua ya makundi, Jwaneng Galaxy imefunga bao moja tu ambalo ilipata katika mechi ya kwanza dhidi ya Wydad na baada ya hapo imecheza mechi nne mfululizo pasipo kufunga bao hivyo ina wastani wa bao 0.2 kwa mechi.

Simba nayo inaonekana kutokuwa tishio kwa ufungaji ingawa angalau ina namba nzuri kulinganisha na Jwaneng Galaxy kwani imefunga mabao matatu katika mechi tano ikiwa ni wastani wa bao 0.6 kwa mechi, mabao yote ikiwa imeyapata katika mechi ilizocheza uwanja wa nyumbani.

Kumbukumbu ya kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Simba ambao uliifanya Jwaneng Galaxy kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2021/2022 licha ya kufungwa mabao 2-0 kwao Botswana inaweza kuiongezea hali ya kujiamini kwenye mechi hiyo ya Jumamosi, lakini Simba nayo inajivunia historia nzuri ya kutamba kwenye mechi za mwisho za hatua ya makundi ambazo zinaamua hatima yake kwenye mashindano ya klabu Afrika.

Simba imeshinda mechi zote nne ambazo ilitakiwa ipate ushindi ili iweze kuingia hatua ya robo fainali, ikifunga mabao 17 sawa na wastani wa mabao 4.25 huku yenyewe ikiruhusu mabao mawili tu sawa na wastani wa bao 0.5.

Beki na nahodha msaidizi wa Simba, Mohamed Hussein 'Tshabalala' alisema kuwa mchezo wa mwisho umekaa kimtego kwao lakini wana imani watapata ushindi na kusonga mbele.

"Itakuwa ni mechi ngumu na itakuwa ni mechi ya kuamua hatima yetu katika michuano hii lakini uzuri ni kwamba katika hizi mechi za kuamua kwenda robo fainali mara nyingi tumekuwa tukifanya vizuri.

"Tutaendelea kuwasikiliza walimu wetu nini wanahitaji kuhakikisha kwamba mchezo huo tunashinda. Hiyo ni mechi yetu muhimu, hiyo ni mechi yetu sote, naamini mashabiki watajitokeza kwa wingi kuhakikisha kwamba tunafanya vizuri.

"Tunaingia katika mechi hiyo kwa tahadhari kuhakikisha tunafanya vizuri. Timu yoyote ikiwa ipo katika mechi hizi za Ligi ya Mabingwa ni nzuri na sisi tunawafahamu hivyo tutajipanga," alisema Tshabalala.

Kocha Abdelhak Benchikha alisema kuwa matokeo ya ushindi ndio wanayahitaji kwenye mechi ya mwisho kwa vile ndio yatawapeleka robo fainali.

"Tuna  njia moja tu ya kufanya ambayo ni kupata ushindi. Tutacheza kwa ajili ya kushinda na tunatuma ujumbe kwa mashabiki wetu waje uwanjani kutupa sapoti.

"Tumecheza mechi nzuri Ivory Coast. Tulipoteza nafasi moja nzuri ya kufunga hatukuitumia. Kwa sasa akili yetu tunaielekeza katika mechi inayofuata ambayo naamini tutapata ushindi.