Ufaransa, Senegal vita ya heshima Kombe la Dunia
New York, Marekani. Unakumbuka wakati Senegal ilipowashangaza mabingwa wa dunia watetezi, Ufaransa? Ni ile mechi ya Ufaransa 0-1 Senegal ya mwaka 2002. Inarudiwa tena leo. Ikiwa ni zaidi ya miongo miwili tangu ushindi maarufu wa Senegal dhidi ya Ufaransa huko Seoul, Korea Kusini, mataifa hayo mawili yanakutana tena katika Kombe la Dunia huku ushindani ukiendelea kuathiriwa na mshtuko ule wa mchezo wa ufunguzi.
Wakati Ufaransa na Senegal zitakapokutana tena leo katika mchezo wao wa ufunguzi wa Kundi I kwenye Kombe la Dunia la 2026, mida ile ya saa 4:00 usiku itakuwa mara ya kwanza kukutana tangu moja ya mishtuko ya kukumbukwa zaidi katika michezo ya ufunguzi ya mashindano hayo. Ni ushindani ambao bado unaonekana kutokamilika zaidi ya miongo miwili baadaye.
Timu hizo mbili zilikutana Mei 31, huko Seoul, katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Dunia 2002. Kwa namna nyingi, tofauti kati yao ilikuwa kubwa sana. Ufaransa walifika kama mabingwa watetezi wa dunia na Ulaya, wakiwa na moja ya safu za ushambuliaji zilizoogopwa zaidi katika soka la kimataifa.
Kikosi cha kocha wa wakati huo, Roger Lemerre, kilijumuisha wafungaji bora kutoka ligi kubwa tatu za Ulaya wakiongozwa na Thierry Henry aliyekuwa amefunga mabao 24 ya ligi akiwa Arsenal msimu huo, David Trezeguet alikuwa amefikia idadi hiyohiyo akiwa Juventus, huku Djibril Cisse akifunga mabao 22 akiwa Auxerre.
Senegal, kwa upande mwingine walikuwa wanashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza na dakika 90 baadaye wageni hao walikuwa wamepata ushindi maarufu wa bao 1-0, na utetezi wa taji la Ufaransa ulikuwa tayari umeanza kuyumba.
Kulikuwa na ishara za tahadhari kwa Ufaransa hata kabla ya mchezo kuanza, kwani Zinedine Zidane ambaye alikuwa moyo wa ubunifu wa timu hiyo alipata majeraha katika mchezo wa kirafiki kabla ya mashindano na akaikosa mechi hiyo. Robert Pires, ambaye bila shaka alikuwa mchezaji bora wa Ufaransa katika msimu wa klabu wa 2001-02, pia hakuwepo.
Senegal, kwa upande wao, huenda walikuwa wageni katika Kombe la Dunia, lakini hawakuwa timu isiyojulikana. Wachezaji 21 kati ya 23 wa kikosi chao walikuwa wakicheza soka nchini Ufaransa. Kwa namna fulani, mchezo huo ulionekana zaidi kama kusanyiko la ajabu la mastaa waliokuwa wakikipiga Ligi Kuu Ufaransa (Ligue 1) kuliko mechi ya kimataifa.
Wachezaji wanne wa kikosi cha Senegal walikuwa wamemaliza msimu wakiisaidia Lens kushika nafasi ya pili katika Ligue 1, akiwemo El Hadji Diouf na Papa Bouba Diop. Wote wawili walikuwa na mchango mkubwa huko Seoul.
Ufaransa walimiliki mpira kwa kiasi kikubwa katika hatua za mwanzo za mchezo, lakini udhibiti wao haukuzalisha nafasi nyingi za wazi. Walikuwa na umiliki wa mpira wa asilimia 65 katika kipindi cha kwanza, lakini walizalisha mabao yanayotarajiwa wastani wa 0.56 pekee.
Senegal, kwa upande mwingine walikuwa wenye nguvu na wenye malengo kila waliposhambulia. Diouf alikuwa kiini cha sehemu kubwa ya tishio hilo. Timu hiyo ilikamilisha mashambulizi hatari matatu katika mechi hiyo, na Diouf alihusika na mawili, huku mbio zake zikiiweka mara kwa mara safu ya ulinzi ya Ufaransa katika wakati mgumu.
Katikati ya kipindi cha kwanza, moja ya mashambulizi hayo lilizaa bao pekee la mchezo. kiungo wa Ufaransa, Youri Djorkaeff, alipoteza mpira katikati ya uwanja na Diouf akaambaa nao upande wa kushoto. Frank Leboeuf, kiungo na beki wa Ufaransa alikosea katika jaribio la kuzuia, jambo lililomruhusu Diouf kumpita na kuingia ndani ya eneo la hatari. Krosi yake iliyopata mwelekeo sahihi hatimaye ilimfikia Bouba Diop, ambaye aliusukuma mpira wavuni.
Halikuwa bao la kuvutia sana, lakini lilionyesha kikamilifu namna mchezo wa Senegal wa kushambulia moja kwa moja na kwa nguvu ulivyokuwa balaa. Baada ya mapumziko, Ufaransa waliongeza presha na mabingwa hao watetezi walishambulia bila kuchoka, wakiibana Senegal katika nusu ya uwanja.
Kwa mujibu wa takwimu, ilionekana kusawazisha ilikuwa suala la muda tu, lakini Ufaransa walimaliza mechi wakiwa na mashuti 24 dhidi ya matano ya Senegal ikiwa ni saba yaliyolenga lango, umiliki wa mpira wa asilimia 65 na miguso 30 ndani ya eneo la Senegal. Katika kipindi cha pili pekee, Ufaransa walipiga mashuti 15, lakini bao la kusawazisha halikuwahi kufika.
Katika mchezo huo ulinzi wa Senegal ulisimama imara. Ferdinand Coly aliingilia mpira mara tano, idadi kubwa zaidi katika mechi, huku Aliou Cisse akifanya nne, idadi ya pili kwa ubora. Omar Daf alifanya 'takolingi' tisa, nyingi kuliko mchezaji mwingine yeyote uwanjani. Mara kwa mara, kikosi hicho cha kocha hayati Bruno Metsu kilifanya takolingi, uingiliaji muvu ya mpira au kuzuia kabisa katika wakati sahihi kabisa.
Kwa Senegal, huo ulikuwa mwanzo wa mambo makubwa yaliyofuata, kwani walifika hadi robo fainali 2002 wakiichapa Sweden katika hatua ya 16 bora. Hadi leo, hayo ndiyo yamebaki kuwa mafanikio yao makubwa zaidi kuwahi kufikiwa, na wakati huo walikuwa timu ya pili kutoka Afrika kufika robo fainali.
Kwa Ufaransa mashindano yalikwenda upande tofauti kabisa. Sare ya bila kufungana dhidi ya Uruguay na kichapo kutoka kwa Denmark kiliwaondoa katika hatua ya makundi. Kikosi kilichokuwa na Henry, Trezeguet na Cisse kilimaliza mashindano bila kufunga hata bao moja katika mechi tatu. Ndiyo maana kukutana kwao tena 2026 kunabeba mvuto mkubwa. Ufaransa dhidi ya Senegal siyo ushindani uliojengwa juu ya historia ya miongo mingi, angalau si ndani ya uwanja. Badala yake, umejengwa juu ya mechi moja, bao moja na tukio moja.
Mwaka 2002, Senegal walikuwa wageni walioijua Ufaransa vya kutosha kuweza kuiumiza. Je? mwaka 2026 Ufaransa itakuwa inafahamu tishio hilo mapema hata kabla ya mechi kuanza ikizingatiwa kwamba kwa sasa ina vichwa kibao bora ikitokea kubeba ubingwa wa Afco 2025? Tusubiri na kuona kama kina Sadio Mane wataendeleza rekodi ya kina Diouf!