Usiku wa Ulaya warejea, Arsenal na Real Madrid dimbani leo
Muktasari:
- Bingwa mtetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ni PSG ambayo msimu uliopita ilichukua kombe kwa kuifunga Inter Milan mabao 5-0 katika fainali.
Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2025/2026 inaanza rasmi leo kwa uwepo wa mechi sita zitakazochezwa katika viwanja na miji tofauti barani Ulaya.
Ni mwanzo wa kibarua kigumu kwa timu 36 kusaka taji la mashindano hayo ambayo msimu uliopita bingwa wake alikuwa ni PSG iliyoifunga Inter Milan kwa mabao 5-0 katika mchezo wa fainali.
Kati ya timu hizo 36, nne zitakuwa zinashiriki kwa mara ya kwanza huku nyingine 32 zikiwa hazina ugeni wa mashindano hayo ambayo kwa Ulaya ndio yenye mvuto na thamani kubwa zaidi kwa ngazi ya klabu.
Timu hizo nne ambazo zinashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza ni
Bodø/Glimt ya Norway, Kairat Almaty ya Kazakhstan Pafos inayotokea Cyprus na Union Saint-Gilloise ya Ubelgiji.
Mchezo utakaofanyika katika Uwanja wa Allianz jijini Turin, Italia baina ya wenyeji Juventus dhidi ya Borussia Dortmund hapana shaka ndio utakaoteka hisia za mashabiki wengi wa soka ulimwenguni kati ya mechi sita zitakazochezwa leo.
Ni timu ambazo kila moja ina la kutamba dhidi ya mwenzake pindi zinapokutana leo kwa kukumbuka kilichowahi kutokea miaka ya nyuma pindi zilipokutana katika mashindano tofauti.
Wakati wenyeji Juventus wakijivunia utemi walionao dhidi ya timu hiyo ya Ujerumani ambapo katika mechi tisa walizowahi kukutana, wameshinda sita, sare na kupoteza moja, Borussia Dortmund inatambia historia yake ya kutwaa ubingwa wa mashindano hayo msimu wa 1996/1997 ilipoichapa miamba hiyo ya Italia katika mchezo wa fainali kwa mabao 3-1.
Refa Francois Letexier ndiye amepangwa kuchezesha mechi hiyo akisaidiwa na Wafaransa wenzake Cyril Mugnier na Mehdi Rahmouni.
Wana nusu fainali wa msimu uliopita, Arsenal wataanzia ugenini huko Hispania ambako watacheza na Athletic Bilbao katika Uwanja wa San Mames.
Mabingwa wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Real Madrid wao wataanzia nyumbani katika Uwanja wa Santiago Bernabeu kucheza na Marseille.
Mechi nyingine leo ni kati ya PSV na Union Saint-Gilloise, Benfica itakabiliana na Qarabag na Tottenham Hotspur itacheza na Villarreal.