Vigogo warejea Ligi Kuu Bara
Muktasari:
- Mechi za mwisho za viporo, zitapigwa Jumanne, Januari 20, 2026, ambapo Azam itaikaribisha Fountain Gate kwenye Uwanja wa Azam Complex saa 10:00 jioni, huku Singida Black Stars ikicheza na JKT Tanzania saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa KMC.
Dar es Salaam. Timu nne zinazowakilisha Tanzania katika hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika, zitakuwa na siku 28 ngumu kuanzia kesho ambapo Ligi Kuu Tanzania Bara itakaporejea rasmi baada ya kusimama kwa muda.
Baada ya kusimama tangu Desemba 7, 2025, ligi hiyo inarejea kwa mechi za viporo zinazohusisha timu za Yanga, Simba, Singida Black Stars na Azam FC.
Kurejea kwa Ligi hiyo kesho, kutazifanya timu hizo nne kuwa na siku 28 za kuamua hatima ya timu hizo katika mashindano matatu tofauti zinazoshiriki msimu huu ambayo ni yale ya Klabu Afrika, Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho la CRDB.
Katika kipindi hicho cha siku 28, timu hizo kila moja inatarajiwa kucheza mechi takribani 10 ikiwa ni wastani wa mechi moja kila baada ya siku mbili.
Mabingwa wa Kombe la Mapinduzi 2026, Yanga wataanza kwa kufungua pazia la ligi kwa kucheza na maafande wa JKT Tanzania, ikiwa ni mechi ya kiporo itakayochezwa kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Yanga ndio timu ya mwisho kucheza Ligi Kuu Bara kabla ya kusimama na kupisha Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), ambapo ilishinda bao 1-0, dhidi ya Coastal Union katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma, Desemba 7, 2025.
Mechi nyingine itakayochezwa kesho saa 1:00 usiku, itakuwa baina ya Dodoma Jiji inayoshika nafasi ya 15 na pointi sita, ikiikaribisha Singida Black Stars, kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Ligi hiyo itaendelea tena Jumamosi, wakati Azam iliyokosa taji la Mapinduzi kwa kuchapwa na Yanga kwa penalti 5-4, itakapoikaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa Azam Complex kuanzia saa 1:00 usiku.
Kocha wa Simba, Steven Barker, ataanza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar Jumapili saa 10:00 jioni, kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni.
Simba iliyopo nafasi ya tano na pointi 12, inaingia ikiwa na kumbukumbu mbaya baada ya mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, kuchapwa mabao 2-0, dhidi ya Azam, Desemba 7, 2025.
Jumatatu Januari 19, 2026, Ligi hiyo itaendelea tena ambapo Yanga itakuwa kwenye Uwanja wa KMC Complex Mwenge, Dar es Salaam kucheza dhidi ya maafande wa Mashujaa kutoka Kigoma, mechi itakayopigwa kuanzia saa 10:00 za jioni.
Mechi za mwisho za viporo, zitapigwa Jumanne, Januari 20, 2026, ambapo Azam itaikaribisha Fountain Gate kwenye Uwanja wa Azam Complex saa 10:00 jioni, huku Singida Black Stars ikicheza na JKT Tanzania saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa KMC.
Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza amesema kuwa wapo tayari kwa urejeo wa ligi.
"Tumeona ratiba na hapa tulipo ndio tumeanza safari ya kwenda Dodoma kuikabili Dodoma Jiji. Tulijiandaa na ratiba kama hii na kwetu tunaona itatusaidia katika maandalizi yetu kwa ajili ya mechi za kimataifa," alisema Massanza.