Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau watoa ya moyoni bajeti ya AFCON, CHAN

Muktasari:

  • Katika AFCON, Mwigulu amesema bajeti ya Sh 179.8 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya mpira wa miguu.

Dar es Salaam. Wakati maandalizi ya viwanja kwa ajili ya fainali za mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 ikiwa ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali katika bajeti kuu ya mwaka wa fedha 2025/26, wadau wa michezo wamepongeza.

Akiwasilisha bajeti hiyo jana Juni 12, 2025 Bungeni mjini Dodoma, Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amesema Serikali imeweka kipaumbele ugharamiaji wa deni la Serikali, mishahara na stahiki za watumishi wa umma, ujenzi na ukarabati wa viwanja vya michezo kwa ajili ya AFCON 2027 na uchaguzi mkuu.

Katika AFCON, Mwigulu amesema bajeti ya Sh 179.8 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya mpira wa miguu.

Awali akizungumza na waandishi wa habari Juni 11, 2025, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa alisema bajeti ya zaidi ya Sh Sh1trilioni imetengwa kwa ajili ya maandalizi ya mashindanbo hayo na yale ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).

Alisema kwa nchi ya Tanzania kutakuwa na viwanja viwili vitakavyotumika katika mashindano ya CHAN ambavyo ni Zanzibar na Benjamin Mkapa.

Alisema kwa upande wa AFCON, viwanja vitakavyotumika ni Amaan, Benjamin Mkapa na Arusha ambacho hadi Juni 11, 2025, alipozungumza na waandishi wa habari, ujenzi wake ulikuwa umefikia asilimia 45 ukitarajiwa kugharimu zaidi Sh286 bilioni.

Alisema uwanja huo wa Arusha hadi ifikapo Aprili mwakani utakuwa umekamilika huku ule wa Dodoma alisema tayari mkandarasi yuko katika hatua za mwisho za kukusanya vifaa ili aanze ujenzi wake.

Mashindano ya CHAN yatafanyika Agosti 2 hadi 28 mwaka 2025 wakati yale ya AFCON yakifanyika 2027, nchi za Tanzania, Kenya na Uganda zikishirikiana kuandaa.


Wadau watoa maoni

Wakiichambua bajeti hiyo, wadau wa michezo nchini wamekuwa na mitazamano tofauti, licha ya kuipongeza Serikali kwenye miundombinu.

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali Mstaafu Iddi Kipingu amesema kikubwa katika bajeti hiyo ni ujenzi wa viwanja.

"Kikubwa kwenye AFCON na CHAN ni kutengeneza viwanja na hoteli na kuandaa timu yetu, bajeti inakidhi.

"Ambacho Watanzania tuko vizuri ni kupokea wageni, hata bajeti imetazama tabia yetu ya kutengeneza mazingira ya kuvutia kupokea wageni," amesema Kipingu.

Mwanariadha nyota wa zamani, Suleiman Nyambui amekuwa tofauti akieleza bajeti imelenga zaidi tukio la AFCON na CHAN na si kwa ajili ya kuinua michezo nchini.

"Wameweka kipaumbele kwenye tukio lijalo, hawajatenga kwa ajili ya kuinua michezo nchini, baada ya mashindano haya (CHAN 2025 na AFCON 2027), waangalie kuendeleza michezo.

"Mfano Serikali imekuwa ikiitaja michezo ya Umisseta na Umitashumta kwamba ni kwa ajili ya kuendeleza vipaji, lakini tujiulize vile vipaji vinavyoibuliwa huko vinaendelezwa?," amehoji Nyambui aliyewahi pia kuwa katibu mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania.

Amesema bajeti ni nzuri katika tukio la CHAN na AFCON, lakini haijajikita katika kuinua na kuendeleza michezo nchini.

Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Dk Devotha Marwa amesema bajeti hiyo imemaanisha ongezeko katika sekta ya michezo.

"Uboreshaji na ujenzi wa viwanja kwa ajili ya AFCON ni maendeleo ya michezo, kwani hata baada ya Afcon viwanja hivyo vitaendelea kutumika si kwenye soka peee, na michezo mingine na kutoa mwaya kuendesha mashindano ya kimataifa," amesema.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa kwa upande wake amesema Serikali kupanga bajeti kubwa kwenye michezo hususani katika ujenzi wa viwanja ni jambo zuri kwani ni mara ya kwanza kufanyika jambo hilo.

“Ujenzi wa viwanja vya kisasa unaoendelea nchini ni uthibitisho kuwa nchi ipo makini katika kuendeleza soka, huku akitoa wito kwa Watanzania kujiandaa na mageuzi makubwa kwenye mchezo huo,”amesema Mwesigwa.

Mwesigwa alisema kuwa ingawa miradi ya viwanja hivyo inatumia fedha nyingi, maandalizi yanayoambatana nayo yanaonyesha dhahiri dhamira ya kweli ya Serikali na wadau kuwekeza katika michezo kwa manufaa ya taifa.

“Kwa namna moja au nyingine, japo ni gharama, lakini maandalizi haya yanaonyesha tuko 'serious'. Nimefuatilia hata mataifa ya jirani kama Kenya na Uganda, nao wameweka mkazo mkubwa katika suala la viwanja,” alisema Mwesigwa.

 Kwa mujibu wa Mwesigwa, kukamilika kwa viwanja hivyo kutatoa fursa kwa mechi kubwa kama fainali za Kombe la FA, Ligi Kuu na hata mechi za kimataifa kuchezwa katika mikoa mbalimbali nchini, badala ya kuangukia kwenye viwanja vichache kama vile Taifa (Mkapa), Amaan na Arusha pekee.

Alitolea mfano wa hali ilivyokuwa wakati wa fainali ya Kombe la FA, ambapo kutokana na changamoto za viwanja vingine, fainali ilihamishiwa Zanzibar kwenye Uwanja wa Amaan. Alisema hali kama hiyo inaweza kuepukika iwapo kutakuwa na viwanja vya kisasa katika kila kanda au mkoa.

“Ujenzi wa viwanja si tu unatoa burudani kwa wananchi, bali pia unasaidia kupunguza gharama na usumbufu wa timu kusafiri mikoa mingi. Pia utaongeza ushiriki wa mashabiki na kukuza vipato vya maeneo hayo,” amesema.


Simba yapongezwa, yapigwa dongo

Akiwasilisha bajeti hiyo, Mwigulu pia aliipongeza timu ya Simba kwa kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa mara nyingine tangu mwaka 1993.

"Mafanikio ya Simba yanatokana na juhudi kubwa ya uwekezaji inayofanywa na rais wa

heshima wa timu hiyo, Mohamed Dewji (MO), hii si tu inatoa heshima kwa timu hiyo, bali pia

inaitangaza nchi yetu katika ramani ya soka la kimataifa.

Kusema ukweli, Simba ya mwaka huu imepambana sana hasa ukizingatia kuwa kocha bado anaijenga timu anayoitaka. Hivyo, nitoe pongezi kwa menejimenti ya timu pamoja na mashabiki wa Simba ambao wanaendelea kuwa mashabiki bora kabisa wakiongozwa na meneja

wangu mimi (Striker), maarufu kama Semaji la CAF," amesema Mwigulu.

Mwigulu alitoa dongo kwa Simba akiwataka wasibweteke na kudai mafanikio ambayo timu hiyo inajivunia sasa sio mapya kwa watani zao Yanga ambayo ilifika hatua kama hiyo mwaka juzi akitaja mafanikio hayo ya Yanga kuchangiwa na  uwekezaji wa Ghalib Said Mohamed (GSM).

Mwigulu aliwashauri Yanga kwamba wanapoandaa ramani ya ujenzi wa uwanja mpya, wasisahau kuweka sanamu ya GSM na kutoa rai kwa klabu nyingine kuiga hatua za Simba na Yanga kwa manufaa ya soka la Tanzania huku akimpongeza pia Said Salim Bakhresa kwa uwekezaji katika tasnia ya michezo.


Kwenye burudani

Katika bajeti hiyo, Mwigulu aligusia pia upande wa burudani na kutaja mapendekezo mapya kwa huduma zinazotolewa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) ambayo imetaka wasimamizi wa wasanii (mameneja) kulipia ada.

Kada hiyo na ile ya prodyuza italipia Sh 60, 000 kila mmoja ambayo ni ada ya usajili Sh 10,000 na kibali Sh 50,000 kila mwaka hii.

"Hii ni kwa ajili ya kuongeza mapato ya Serikali na kurasimisha kazi zao, itawawezesha kupata mikopo ya Serikali kupitia mfuko wa Utamaduni na Sanaa," amesema.

Pia wapigapicha za mnato wa kazi za sanaa, wabunifu wa picha, wabunifu wa mavazi, wasanifu wa picha na matangazo, saluni za kike na kiume, wapambaji katika sherehe na matukio, wapambaji wa keki watalipia ada ya Sh 10,000 kila mmoja.

Upande wa vibali,  makundi hayo yametofautiana gharama, wapambaji wakitakiwa kulipa Sh 20,000 huku wasanii binafsi ambao walikuwa wakilipia Sh 50,000 kama kibali kwenda nje ya nchi ikifutwa ili kuhamasisha wasanii wazawa kwenda nje ya nchi kufanya shughuli za sanaa.

Wizara ya Habari. Utamaduni. Sanaa na Michezo imeongezea maradufu bajeti mwaka ujao wa fedha 2025/26  kutoka Sh 285.3 bilioni  za mwaka 2024/25 hadi Sh519.6 bilioni kwa mwaka ujao wa fedha.