Prime
Wagombea urais TFF walia kukosa udhamini
Muktasari:
- Katika uchaguzi huo wa TFF utakaofanyika Agosti 16 jijini Tanga, jumla ya nafasi saba zinawaniwa.
Ishu ya kuchukua na kurudisha fomu za kuwania nafasi katika Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imefungwa leo, huku wagombea wa Urais akiwamo Ally Mayay na Shija Richard wakilia faulo walizokutana nazo wakati wa kusaka wadhamini wa kuwaidhinisha.
Mayay na Shija ni kati ya wagombea wanne wa Urais waliorudisha fomu wakiwania nafasi hiyo akiwamo Dk Mshindo Msolla na Wallace Karia anayetetea kiti chake kwa mara ya tatu, lakini wagombea hao wamelia kukosa wadhamini wanaotakiwa kuwaidhinisha ili kukidhi kanuni za uchaguzi wa TFF za mwaka 2021 zinazotaka wapate wajumbe wa Mkutano Mkuu si chini ya wadhamini watano kati ya 47 waliopo.
"Hakuna mtu hata mmoja aliyepata udhamini, nakwambia ukweli zote zimechukuliwa na mtu mmoja, na hata akipata haziwezi kufika tano zinazotakiwa," kilisema chanzo kutoka ndani ya mmoja wa mgombea jana.
Katika uchaguzi huo wa TFF utakaofanyika Agosti 16 jijini Tanga, jumla ya nafasi saba zinawaniwa, ikiwamo moja ya Urais na nyingine sita za Wajumbe wa Kamati ya Utendaji na jana ilikuwa mwisho wa kurudisha fomu baada ya zoezi na uchukuliwaji wa fomu hizo kuanza tangu Jumatatu (Juni 16).
Kipengele cha suala la Udhamini wa wagombea (endorsement), kimelalamikiwa na nahodha wa zamani wa Yanga Mayay na Shija sambamba na Ally Msigwa nyota wa zamani pia wa Yanga, kwa kukosa watu wa kuwadhamini.
Kanuni hizi hapa
Kanuni ya Uchaguzi ya Mwaka 2021 Ibara ya 10 (3 -4) kinaeleza kuwa Mgombea wa Urais wa TFF lazima awe na barua tano za udhamini kutoka kwa wanachama wa TFF, huku kwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji kutoka kanda, lazima awe na barua ya udhamini kutoka Chama cha Soka cha Mkoa husika.
na Mwanachama hapaswi kumdhamini mgombea zaidi ya mmoja kwa nafasi moja vinginevyo udhamini wote utakuwa batili.
Kwa mujibu wa orodha hiyo ya wanaotoa uidhinishaji (endorsement), kwa wagombea wa TFF ni 47 ambao mchangnuo wake upo hivi; Vyama vya Soka vya Mikoa (FA) yenye wajumbe 26, Klabu za Ligi Kuu (16) huku Chama wa Waamuzi Tanzania (FRAT), Chama cha Makocha Tanzania (TAFCA), Chama cha Madaktari wa Michezo (TSMA), Chama cha Wachezaji (SPUTANZA) na Chama cha Soka la Wanawake (TWFA) kila moja ikiwa na mjumbe mmoja.
Hata hivyo, Mayay amerudisha fomu ya kugombea nafasi hiyo akiambata na rafiki yake, Dominic Salamba na kufunguka kwamba amekamilisha hatua ya awali ya mchakato huo kwa kuchukua na kurudisha fomu.
"Hatua ya kwanza ilikuwa kuchukua fomu na nawashukuru rafiki zangu kina Kiemba (Amri) waliniwakilisha kwenye kuchukua fomu. Sikuwepo nilikuwa kwenye kumalizia msiba wa mzee wangu," alisema Mayay ambaye aligombea tena kipindi kilichopita na kuongeza;
"Nimerudi jana (juzi) na leo (jana) nikasema nirudishe fomu hizi kwa kuwa leo ndio mwisho wa hatua hii ya kuchukua nakurudisha fomu."
Akizungumzia juu ya uidhinishwaji kupitia wajumbe wa uchaguzi huo kwa wagombea, Mayay alisema; "Zipo changamoto nimekutana nazo na unajua changamoto ni sehemu ya maisha yetu. Zamani hizi endorsement ilikuwa moja unaweza kumpa mgombea zaidi ya mmoja, lakini nyakati zimebadilika. Mimi nimeona nirudishe fomu haya mengine yataendelea baadaye."
Kwa upande wa Shija, alisema licha ya kurudisha fomu lakini changamoto ileile ya kukosa uidhinishwaji kutoka kwa wajumbe wa mkutano mkuu na mtumishi huyo wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) alifafanua anakusudia kufungua mashtaka kwa Kamati mbili za TFF ya Maadili na ile ya Rufani ya Uchaguzi.
"Nimerudisha fomu mama mnavyoona lakini niungane na wengine ambao wameonyesha kukosa hizi endorsement (uidhinishwaji). Mimi ni mzoefu wa uchaguzi wa TFF na nimewahi hadi kufikia hatua ya kupigiwa kura," alisema Shija na kuongeza;
"Kila unayemgusa katika watu 47 unaambiwa zimeshatoka, sasa kila mmoja analia hizi zimekwenda wapi, nilichokuja kugundua ni kuwa, kuna mgombea mwenzetu mmoja amezichukua zote. Hatuwezi kuwa na uchaguzi wa huru kwa njia kama hii, binafsi nasema najipanga kwenda kushtaki haya Kamati ya Maadili kwa kuwa uidhinishwaji ulitakiwa kufanyika kuanzia ile siku ya kuchukua fomu ilipoanza.
"Nitapeleka pia malalamiko Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF, ili kupinga mambo haya hakuna usawa lakini pia nitakwenda mpaka Baraza la Michezo Tanzania (BMT) ambao TFF ipo chini ya chombo hicho."
Wakati Mayay na Shija wakilia, kwa upande wa Dk Msolla kupitia mwanaye, Msolla Mshindo alisema kila kitu kipo sawa na yeye alipata waidhinishwaji ingawa baadaye chanzo kilisema naye hajakidhidi idadi inayotakiwa, huku Msigwa anayewania nafasi ya Ujumbe akilia kukosa wadhamini.
"Dk Msolla ni mwanamichezo mbobevu wa mambo ya michezo. Kila kitu kipo sawasawa kwake na kama mnavyoona amerudisha fomu," alisema mtoto wa Msolla, lakini mgombea nafasi ya Ujumbe, Ally Msigwa alisema amekumbana na changamoto ya watu wa kumuidhinisha na amerudisha fomu hivyo hivyo kwa vile hata asingerudishwa tayari alishaliwa Sh 200,000 za kununua fomu hiyo.
"Nimerudisha fomu lakini kitu kimeniumiza ni kukosa uidhinishwaji kwa wajumbe wa mkutano mkuu, nilianza mapema tu wakati mchakato wa uchaguzi ulipoanza lakini sijazipata," alisema Msigwa