Watani wa Jadi na vita ya uamuzi Jeshini
Nyota wa Yanga, Pacome Zouzoua wakati akijaribu kumtoka Winga wa Simba, Libase Guey katika mechi ya fainali ya Kombe la Muungano iliyowakutanisha Watani wa Jadi visiwani Zanzibar, Aprili29, 2026. Picha na Yanga
Muktasari:
- Timu hizo zinakutana katika dakika 90 zenye presha kubwa, kila moja ikiwa na hesabu zake tofauti lakini zote zikilenga ubingwa.
Dar es Salaam. Mechi ya Dabi ya Kariakoo katika duru la pili la Ligi Kuu Bara, inapigwa leo Jumapili kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam, ambapo Simba itakuwa mwenyeji wa Yanga.
Mechi hiyo ina uamuzi ndani yake kwani yeyote atakayeshinda atakuwa mbabe msimu huu kwani Yanga ilianza kushinda Ngao ya Jamii 1-0, zikaja kutoka 0-0 mechi ya kwanza ya ligi, kisha Simba ikashinda 1-0 fainali ya Kombe la Muungano. Leo ni mechi ya nne kuzikutanisha timu hizo msimu huu, kila upande umeshinda mara moja, nyingine ikiwa sare.
Timu hizo zinakutana katika dakika 90 zenye presha kubwa, kila moja ikiwa na hesabu zake tofauti lakini zote zikilenga ubingwa.
Simba, ikiwa nyumbani, inalazimika kushinda ili kupunguza tofauti ya pointi dhidi ya Yanga kwani hivi sasa tofauti yao ni tano. Yanga inaongoza ligi kwa pointi 47, inafuatia Simba yenye 42.
Kushindwa kufanya hivyo kutamaanisha kuipa nafasi kubwa Yanga kuelekea kutetea ubingwa wa ligi hiyo.
Iwapo mchezo huo Simba itaambulia sare au kipigo, itakuwa pigo kwao ambayo inataka kukatisha ukame wa kutwaa taji la ligi, mara ya mwisho ilibeba msimu wa 2020-2021.
Simba inaingia kwenye dabi hiyo ikiwa na morali ya juu baada ya kushinda Fainali ya Kombe la Muungano Aprili 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kwa bao 1-0 dhidi ya Yanga.
Baada ya ushindi huo, wachezaji waliocheza fainali walirejeshwa haraka Dar es Salaam kwa ndege ili kupata mapumziko, huku wengine wakirejea na boti.
Hofu kubwa kwa Simba ni hali ya majeraha ya winga Anicet Oura aliyepata tatizo la misuli ya paja kwenye fainali hiyo na kutolewa dakika ya 26, ingawa juhudi zilikuwa zinafanyika awe fiti kwa mchezo wa leo huku taarifa zikibainisha hakuumia sana.
Pia, beki Ismael Toure alimaliza mechi hiyo akiwa na maumivu, lakini taarifa zinaeleza kuwa yuko tayari kwa mchezo huo.
Kwa upande wa Yanga, baada ya kupoteza fainali ya Muungano, ilibaki visiwani Zanzibar kwa maandalizi kabla ya kurejea Dar es Salaam kwa siri.
Yanga inahitaji ushindi kurejesha imani kwa mashabiki wake na kuonyesha kuwa imejirekebisha baada ya kupoteza taji hilo.
Ingawa imekuwa na rekodi nzuri dhidi ya Simba kwa kushinda mara sita mfululizo kabla ya kusimamishwa kwa sare na kipigo.
Yanga inahitaji ushindi au sare ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa tano mfululizo. Mabingwa hao watetezi bado hawajapoteza mechi yoyote ya ligi msimu huu, huku Simba ikiwa imepoteza mmoja.
Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves alifanya mazungumzo binafsi na baadhi ya wachezaji wake ili kuwaandaa kisaikolojia kabla ya mchezo huo.
Mechi hii Yanga itawakosa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kutokana na majeraha pamoja na kiungo Mudathir Yahya anayetumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu na Bodi ya Ligi Tanzania.
Hata hivyo, Chadrack Boka anatarajiwa kuendelea upande wa kushoto, huku Duke Abuya akitarajiwa kuanza eneo la kiungo wa kati baada ya kutokea benchi katika fainali ya Muungano.
Mechi hiyo itaamuliwa na waamuzi kutoka Morocco ambapo Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Karim Boimanda, alisema uamuzi wa kuwachagua waamuzi hao si pendekezo la klabu, bali ni muongozo wa kanuni za ligi hiyo.
"Waamuzi hawakuja kwa pendekezo la klabu, bali kanuni inaruhusu, kamati inapoona kuna umuhimu wa kutoa waamuzi kutoka ndani itafanya hivyo, kama itateuwa kutoka nje pia inaruhusiwa," alisema Boimanda.
Waamuzi waliochaguliwa kuchezesha mechi hiyo ni Hamza El Fareq (mwamuzi wa kati), Lahsen Agaou (mwamuzi msaidizi namba moja), Hamza Massiri (mwamuzi msaidizi namba mbili) na Mustapha Kechaf (mwamuzi wa nne wa mezani) ambao wote ni raia wa Morocco.
Kanuni ya 39 ya Ligi Kuu toleo la 2025 inayozungumzia waamuzi, imefafanua jambo hilo.
Kanuni hiyo ya 39 kifungu cha 7.1, inasema: "Kamati ya Waamuzi ya TFF inaweza kupanga mwamuzi/waamuzi kutoka nje ya Tanzania kwenye Michezo ya Ligi Kuu."
Hii itakuwa mara ya pili kwa Dabi ya Kariakoo ndani ya Ligi Kuu Bara kuamuliwa na waamuzi kutoka nje, ambapo msimu uliopita mchezo wa mwisho baina ya timu hizo uliochezwa Juni 25, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, uliamuliwa na waamuzi kutoka Misri na Yanga kushinda 2-0.
Mwamuzi wa kati alikuwa Amin Mohamed Amin Omar, huku Mahmoud Ahmed Abo El Regal akiwa mwamuzi msaidizi namba moja na Samir Gamal Saad Mohamed ni mwamuzi msaidizi namba mbili, Ahmed Mahrous alikuwa mwamuzi wa nne wa mezani, hawa wote kutoka Misri, huku mtathimini waamuzi akiwa Alli Mohamed wa Somalia.
Akizungumzia kuhusu utaratibu wa kuingia uwanjani, Boimanda alisema: "Mageti yatafunguliwa kuanzia saa 7 mchana, mashabiki wale wenye tiketi ndio wataruhusiwa kuingia, vinywaji havitaruhusiwa kesho."
Kocha wa Simba, Steve Barker, alisema: "Ili kushinda mechi ya kesho tunapaswa kufunga magoli na sio rahisi, tumekuwa na muendelezo mzuri hiyo inafanya mechi hiyo kuwa ngumu kutokana na ubora wa Yanga kwenye eneo la ulinzi.
"Kila mchezaji yuko sawa na wanashauku ya kutosha japo kushinda mechi dhidi ya Yanga ni ngumu na tunaelewa tukishinda kesho itakuwa tumepunguza gepu la pointi kubaki mbili dhidi ya Yanga, naamini itakuwa mechi ngumu kwa timu zote mbili."
Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, alisema: "Ni mashindano tofauti, tunajiamini vya kutosha na tunaamini tunaweza kucheza vizuri kesho (leo), tunaenda kucheza mechi na moja ya timu ngumu Tanzania na Afrika."