Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wazawa 10 wanaendelea kukimbiza

Muktasari:

  • Kibu yupo kwenye orodha ya wachezaji wenye nafasi ya kuwania ufungaji bora kwani amezidiwa mabao mawili na kinara Ismaïl Belkacemi wa USM Alger mwenye mabao matano.

Katika vitabu vya kumbukumbu za klabu kongwe hapa nchini, Simba na Yanga, kuna rekodi zinaonyesha timu hizo zimefika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mara moja kila upande.

Ilianza Yanga msimu wa 2022-2023 ambapo ilikwenda kupoteza mbele ya USM Alger ya Algeria kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla kuwa 2-2. Mechi ya kwanza iliyochezwa Mei 28, 2023 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Yanga ilipoteza kwa mabao 1-2.

Mechi ya marudiano ilipigwa Juni 3, 2023 nchini Algeria, Yanga ikashinda 0-1, matokeo ambayo hayakutosha kuifanya kutwaa ubingwa. Ikarejea nchini na medali ya nafasi ya pili.

Misimu miwili mbele kwa maana ya 2024-2025, watani zao wa jadi, Simba nayo imefuzu fainali ya michuano hiyo ikisubiri kukabiliana na RS Berkane, mechi ya kwanza imepangwa kuchezwa Mei 17, 2025 nchini Morocco, kisha marudiano ni Mei 25, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kwa misimu ya karibuni, Simba na Yanga zimekuwa na lundo kubwa la wachezaji wa kigeni inaowasajili kuongeza nguvu kwenye vikosi vya timu hizo, lakini licha ya hivyo, wazawa wameendelea kukomaa kupambania nafasi.

Ukiangalia vikosi vya Simba na Yanga, kila kimoja kina wachezaji 12 wa kimataifa lakini si wote wanaocheza, wapo wanaoishia benchi wakisubiri wazawa waanze jambo linalodhihirisha kwamba wazawa hawapo kinyonge wanapambania nafasi zao.

Wakati kikosi cha Yanga kinacheza mechi ya kwanza ya fainali Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023, kilianza na wazawa watano ambao ni Dickson Job, Kibwana Shomari, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Hamad 'Bacca', Mudathir Yahya, kisha Salum Abubakar 'Sure Boy' na Clement Mzize wakaingia kutokea benchi.

Wazawa ambao hawakucheza kabisa wakiishia benchi katika mechi hiyo ni Metacha Mnata, Farid Mussa na Zawadi Mauya.

Ile ya marudiano, pia wazawa watano walianza ambao ni Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca, Mudathir Yahya na Salum Abubakar 'Sure Boy', huku Farid Mussa na Clement Mzize wakiingia wakitokea benchi. Metacha Mnata, Kibwana Shomari na Zawadi Mauya hawakucheza kabisa wakiishia benchi.

Safari hii Simba katika mechi mbili za nusu fainali zilizowapa tiketi ya kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ilipocheza dhidi ya Stellenbosch, nayo imekuwa na nyota watano wa kikosi cha kwanza ambao ni Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Abdulrazack Hamza, Yusuph Kagoma na Kibu Denis.

Nyota hao walianza mechi ya kwanza iliyochezwa Aprili 20, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar wakati Simba ikishinda 1-0, kisha wakaanza tena ugenini nchini Afrika Kusini, matokeo yakiwa 0-0, Aprili 27, 2025.

Wazawa walioishia benchi mechi zote hizo ni Ally Salim, David Kameta, Awesu Awesu, Edwin Balua na Ladack Chasambi.

Ukiangalia katika wachezaji hao, safu ya ulinzi ndiyo imebeba wazawa waliokuwa panga pangua huku wakionekana kujenga ulinzi imara uliozifikisha timu hapo.

Msimu wa 2022-2023 kipindi ambacho Yanga inacheza fainali, kuanzia hatua ya makundi hadi fainali yenyewe, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job na Ibrahim Bacca, walikuwa wachezaji muhimu wa eneo la ulinzi na kuifanya timu hiyo kuruhusu mabao saba pekee. Manne hatua ya makundi, moja nusu fainali na mawili fainali.

Katika mabao ya kufunga, Yanga kuanzia makundi hadi fainali ilitikisa nyavu za wapinzani mara 17, wazawa wakifunga mawili kupitia Mudathir Yahya na Farid Mussa.

Kwa upande wa Simba, nahodha Mohamed Hussein, Shomari Kapombe na Abdulrazack Hamza, nao wamekuwa wachezaji muhimu wa eneo la ulinzi huku wakiruhusu mabao sita pekee kuanzia hatua ya makundi hadi nusu fainali. Mabao manne imeruhusu hatua ya makundi na mawili robo fainali, huku nusu fainali mechi zote mbili ikiondoka na clean sheet.

Mbali na kuzuia, pia katika kufunga, Simba hadi inatinga fainali imetikisa nyavu za wapinzani mara 11, huku wazawa waliocheka na nyavu ni Kibu Denis aliyefunga matatu na Mohamed Hussein moja.

Kumbuka Kibu yupo kwenye orodha ya wachezaji wenye nafasi ya kuwania ufungaji bora kwani amezidiwa mabao mawili tu na kinara Ismaïl Belkacemi wa USM Alger mwenye mabao matano.

Nahodha wa Simba, Mohamed Hussein, amezungumzia kutinga fainali kwa timu hiyo akisema: "Kufuzu fainali ni kitu ambacho Wanasimba walikuwa wakikisubiri kwa hamu, kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu tunakwenda kuchukua taji hili."