Yanga, Simba zampasua kichwa Florent Ibenge
Muktasari:
- Azam FC inashika nafsi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC wakiwa na pointi 23 walizokusanya katika mechi 11.
Kocha Mkuu wa Azam Florent Ibenge amesema licha ya matokeo mazuri waliyonayo lakini hafurahii sana kwa kuwa pointi walizozidiwa na timu za Simba na Yanga kwenye msimamo wa Ligi zinawapa wakati mgumu katika kufikia malengo yao ya kutwaa ubingwa msimu huu.
Amesema kutokana na hali hiyo, anaendelea kuwaandaa vyema nyota wake kuhakikisha kila mchezo ulio mbele yao wanapata ushindi, ukiwemo dhidi ya Tanzania Prisons ugenini kesho, Alhamisi, Machi 5, 2026 katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Azam iliyopo nafasi ya tano kwa pointi 23, imezidiwa moja dhidi ya Simba waliopo nafasi ya tatu na pointi sita dhidi ya vinara wa Ligi Kuu, Yanga na kufanya vita ya ubingwa msimu huu kuwa nzito.
Akizungumza jijini Mbeya leo, Jumatano, Machi 4, Ibenge amesema matokeo waliyonayo si mabaya sana japokuwa hayamfurahishi kutokana na kuzidiwa pointi na Simba na Yanga, hali inayomfanya kupambana kuwashusha usukani.
Amesema timu hiyo inayo mikakati yake akieleza kuwa kinachompa matumaini zaidi ni namna nyota wake wanavyojituma ndani ya uwanja kusaka ushindi akieleza kuwa kiwango wanachoonesha kinampa nguvu.
“Kikubwa ni kupambana kuondoa pengo lililopo la pointi dhidi yetu, Simba na Yanga. Tunao mkakati wetu msimu huu katika kufanya vizuri na vijana wanapambana na wanaonesha soka safi,” amesema Ibenge.
Kuhusu mchezo wa kesho dhidi ya Tanzania Prisons, amekiri kutokuwa mwepesi akieleza kuwa watakuwa makini akibainisha kuwa kutokuwapo kwa baadhi ya wachezaji akiwamo Feisal Salum haitakuwa tatizo kwa kuwa anacho kikosi bora.
Kwa upande wake Nahodha wa timu hiyo, Lusajo Mwaikenda amesema mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na wapinzani nafasi waliyopo akieleza kuwa hawataki yawakute yaliyowatokea Liverpool mbele ya Wolves walipolala 2-1.
“Bado tuna ubora kwenye Ligi Kuu licha ya ratiba ngumu mfululizo Tunajua ugumu wa mchezo dhidi ya Prisons waliopo chini kwenye msimamo Kila mmoja aliona kilichowakuta Liverpool dhidi ya Wolves,” amesema Mwaikenda