Yanga yaipa Tabora United Sh20 milioni
Muktasari:
- Hii ni mara ya kwanza timu hiyo inafanikiwa kuichapa Yanga katika historia yao kuanzia zimeanza kukutana.
Tabora. Baada ya Klabu ya Yanga kupokea kichapo kizito cha mabao 3-1 kutoka kwa Tabora United kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Chamazi Complex jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Paul Chacha, amesema ataizawadia timu hiyo Sh20 milioni baada ya kuifunga Yanga.
Hii ni mara ya kwanza timu hiyo inafanikiwa kuichapa Yanga katika historia yao kuanzia zimeanza kukutana.
Bosi huyo wa mkoa amesema timu ikiwasili fedha hizo atazikabidhi kwa wachezaji kama motisha kwao kwa ushindi walioupata.
Aidha Chacha amesema awali waliahidi timu hiyo ikishinda mchezo wowote wa Ligi Kuu ikiwa ugenini itapewa bonasi ya Sh10 milioni lakini kwa kuifunga Yanga dau limepanda na sasa watapewa Sh20 milioni kama zawadi ya kutikisa nchi.
Akizungumza na Mwananchi Chacha amesema mpango wa timu hiyo ni kwamba kila atakayekanyaga Uwanja wa Al Hassani Mwinyi afungwe ili timu hiyo imalize ligi kwenye nafasi za juu.
"Tumejipanga kwamba kila atakayekuja hapa tumfunge bao za kutosha na uwezo huo tunao kwakua tangu tunafanya usajili tulihakikisha kwamba tunasajili wachezaji bora ambao wanaweza kucheza na kutupa matokeo hivyo wapinzani wajipange," alisema Chacha.
Baadhi ya mashabiki wa Tabora United wakiwakilishwa na Emmanuel Vedastus wamesema hawakutegemea timu yao kuishangaza Yanga kutokana na ubora ambao wapinzani wao hao wamekuwa nao tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi.
"Tunawapongeza wachezaji kwa kujitoa na kutupa ushindi kwa tulivyocheza mechi mbili hapa nyumbani mwanga ulionekana wa kuifunga Yanga japokuwa hatukuwa tukijua kama tutafunga mabao mengi kiasi hiki ila tumeandika historia kama Tabora kuwa timu ya kwanza kuifunga Yanga idadi hii," alisema.
Baada ya mchezo huo, Yanga imeendelea kusalia nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu bara baada ya michezo 10 wakikusanya alama 24 huku Tabora United wenyewe wakifikisha alama 17 baada ya mechi 11 na kupaa hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi kuu.