Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga yamkomalia refa wa CAF

Dar es Salaam. Uongozi wa Yanga umeandika barua kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ikimlalamikia refa Ibrahim Mutaz kutoka Libya ikidai hakuchezesha kwa haki mechi yao ya ugenini ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Medeama ya Ghana, Ijumaa, Desemba 8.

Mjumbe wa bodi ya wakurugenzi ya Yanga na mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya timu hiyo, Rodgers Gumbo aliliambia gazeti hili kuwa lengo la kuiandikia CAF barua hiyo ya malalamiko ni kuiomba ifanye tathmini kwa marefa ili wazitafsiri vyema sheria 17 za mpira wa miguu.

Gumbo alisema kuwa uchezeshaji usioridhisha wa refa Mutaz ulichangia kwa kiasi kikubwa kuifanya Yanga isipate ushindi katika mchezo huo ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 na kuinufaisha Medeama ambayo ilikuwa nyumbani.

“Ni kweli tumepeleka barua ya malalamiko kwa CAF tukimlalamikia mwamuzi (Mutaz) kwa kuonyesha upendeleo katika mechi yetu ya ugenini dhidi ya Medeama. Na matukio tuliyoyaainisha ni mawili ambayo la kwanza ni rafu ambayo mchezaji wetu Nickson Kibabge alichezewa na mchezaji wa Medeama ambaye alistahili kuonyeshwa kadi nyekundu lakini refa hakufanya hivyo.

“Lakini pia kuna tukio la bao letu halali ambalo Kibabage alifunga lakini refa akalikataa.

“Tumewaandikia ili wajue nini cha kufanya kwa sababu matukio kama yale yananyima timu haki ya kupata ushindi na kuipa nyingine matokeo ambayo haijastahili,” alisema Gumbo.

Tukio la rafu dhidi ya Kibabage linalolalamikiwa na Yanga ni lile la dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza ambapo beki Kwadwo Amoako alimrukia kwa miguu miwili nyota huyo wa Yanga ambapo kwa mujibu wa sheria ya faulo na utovu wa nidhamu, adhabu yake ni kadi nyekundu ya moja kwa moja ingawa refa Mutaz alionyesha kadi ya njano.

Lakini pia katika kipindi cha pili cha mchezo, bao la Kibabage lilikataliwa kwa kile kilichodaiwa kuwa aliotea kabla ya kufunga lakini picha za marudio ya luninga zilionyesha kuwa Kibabage hakuwa ameotea wakati akifunga bao hilo.

Sare hiyo ya bao 1-1 ugenini iliifanya Yanga ifikishe pointi mbili na kuendelea kukaa mikiani mwa kundi D linaloongozwa na Al Ahly iliyo na pointi tano huku Medeama na CR Belouizdad kila moja ikiwa na pointi nne.

Kwa nafasi iliyopo sasa, Yanga inahitajika kuibuka na ushindi katika mechi zake tatu zinazofuata dhidi ya Medeama na Belouizdad nyumbani na nyingine ya ugenini dhidi ya Al Ahly ili iweze kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga haijwahi kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo tangu mfumo wake ulipobadilishwa rasmi mwaka 1998.