Unaweza kusema ilikuwa ni zaidi ya burudani kwa Watanzania katika pambano la Knock Out ya Mama lililoanza usiku wa Desemba 26 na kufikia tamati saa 12 asubuhi ya Desemba 27, 2024 kwenye ukumbi wa The Super Dome, Masaki jijini hapa.
Pambano hilo lililowakutanisha mabondia kutoka Ufilipino, Burundi, Afrika Kusini, Nigeria na wenyeji Tanzania, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alikuwa mgeni rasmi.
Rais Samia Suluhu Hassan alinogesha pambano hilo kwa kutoa bonasi ya Sh10 milioni kwa Watanzania watakaoshinda mikanda ya ubingwa kwa Knock Out (KO) na Sh5 milioni kwa ushindi wa pointi na zawadi ya Boxing Day Sh1 milioni kwa mabondia waliocheza na wageni mapambano ya kimataifa yasiyokuwa ya ubingwa.