Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Benki ya CRDB inavyochangia kuboresha elimu kupitia Keti Jifunze

Maofisa wa Benki ya CRDB wakiwa katika picha ya pamoja na uongozi na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mahutanga iliyopo Halmashauri ya Mji wa Ifakara, mkoani Morogoro baada ya kugawa meza na viti katika shule hiyo kupitia programu yao ya Keti Jifunze.

Akiwa ofisini kwake, katika ghorofa ya tano ya jengo la makao makuu ya Benki ya CRDB, TullyEsther Mwambapa ambaye ni Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation anatizama kwa utulivu foleni kubwa ya magari yaliyopo kwenye mataa ya Daraja la Salender akifikiri ni kwa namna gani atafika nyumbani kwake baada ya kukaa ofisini humo tangu saa 12:15 asubuhi.

Kwa tabasamu lenye mchanganyiko wa tafakuri nyingi, mkurugenzi huyu wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation anasema: “Tanzania yetu ni nchi iliyobarikiwa sana. Kuna vitu vingi vya kuvutia na changamoto kadhaa za kushughulikia ili kuboresha maisha yetu.”

Maofisa wa Benki ya CRDB wakiwa katika picha ya pamoja na uongozi na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Rukwa iliyopo Halmashauri ya Wilaya wa Sumbawanga, mkoani Rukwa baada ya kugawa meza na viti katika shule hiyo kupitia programu yao ya Keti Jifunze.

Tully anasema haya baada ya kufunga kompyuta yake akiwa amemaliza kuipitia ripoti ya Uwekezaji kwa Jamii ya Benki ya CRDB kwa mwaka 2025 inayoonyesha kuwa miezi hiyo 12, Benki imeshiriki kwa kiasi chake kusaidia kupunguza uhaba wa madawati kwa shule za msingi nchini na viti na meza kwa sekondari zinazowapika viongozi, wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania ya leo na kesho.

Katika ripoti hiyo, inadhihirika kwamba Benki ya CRDB imetumia zaidi ya Sh 253 milioni kutengeneza madawati 515 pamoja na viti na meza  2,346, samani zilizosambazwa katika shule mbalimbali nchini kote kupitia Programu ya Keti Jifunze.

Kinachomfurahisha Tully ni juhudi iliyowekwa kwenye mchakato mzima wa utengenezaji na usambazaji wa samani hizo ambazo ni muhimu katika safari ya mwanafunzi kusoma kwa utulivu, usafi wa mwili na mavazi pamoja na kuongeza umakini na usikivu wa mwanafunzi.

“Ulikuwa ni mwaka wa hekaheka kwani hatukulala. Tulilazimika kuwepo kila mahali kuhakikisha wanafunzi wanaketi na kujifunza kuanzia kule Mbinga Mjini mpaka Nguruka pale Uvinza. Tulifika Mbulu, Muleba hadi Mafia huko kote tulikuta wanafunzi wenye ari ya kujifunza na kusoma kwa bidii licha ya changamoto zilizokuwepo. Kwa madawati, viti na meza tulizokabidhi, tuliacha tabasamu la matumaini kwa wanafunzi wengi,” anakumbuka Tully. 

Maofisa wa Benki ya CRDB wakikabidhi meza na viti kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Dovya iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa programu yao ya Keti Jifunze kwa shule mbalimbali nchini.

Katika safari hizo za kuwafuata wanafunzi na kuwapa samani za darasani, Tully anasema yapo maeneo mnasafiri kwa kilomita nyingi bila kupishana na gari hivyo kutoa nafasi ya kufurahia mandhari yenye uoto wa asili, wanyamapori pamoja na milima na misitu ya kuvutia.

Ukiliangalia tabasamu lake pindi akieleza haya, unayaona madaraja makubwa yaliyojengwa na Serikali katika mito kadhaa inayounganisha maeneo tofauti na nchi yetu kuanzia Daraja la Mkapa lililojengwa katika Mto Rufiji likiunganisha mikoa ya kusini, Daraja la Wami linalotumiwa zaidi na watu wa mikoa ya kaskazini pamoja Daraja la Ruvu kwa wanaotoka na kuingia Dar es Salaam kutokea Barabara ya Morogoro.

Mkakati wa Serikali kujenga madaraja haya pamoja na kuimarisha mtandao wa barabara unaounganisha mkoa na mkoa kote nchini sio tu unakusudia kurahisisha usafirishaji wa huduma na bidhaa bali kuwaruhusu wananchi kutembea kutoka eneo moja kwenda jingine ikiwamo kufuata elimu.

Uamuzi wa serikali kufuta ada kuanzia shule za msingi mpaka sekondari tangu mwaka 2016 uliongeza udahili wa wanafunzi hivyo kuleta changamoto mpya ambayo ni upungufu wa madawati kwa wanafunzi wa shule za msingi pamoja na viti na meza kwa ajili ya sekondari.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Old Mapinduzi iliyopo Halmashauri ya Mji wa Handeni, mkoani Tanga wakiwa wameketi katika viti vilivyogawiwa na Benki ya CRDB ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa programu yao ya Keti Jifunze kwa shule mbalimbali nchini.

Mwaka 2024, kulikuwa na shule za msingi 20,533 zenye zaidi ya wanafunzi milioni 11.39 huku sekondari zikiwa 6,269 zinazowahudumia zaidi ya wanafunzi milioni 3.31. Takwimu za Serikali zinaonyesha kati ya mwaka 2020 na 2024 vyumba vya madarasa ya shule za msingi vimeongezeka kutoka 128,425 hadi 155,330 wakati vile vya sekondari vikitoka 46,928 hadi 81,052.

Uboreshaji huu wa miundombinu ya shule za serikali, Tully anasema:“Unahitaji ushirikiano wa kila mdau kuchangia kile anachoweza kuhakikisha watoto wote wanasoma katika mazingira bora. Benki ya CRDB itaendelea kuonyesha mfano katika hili kuhakikisha shule zote zinawavutia wanafunzi hivyo kupunguza utoro na idadi ya wanaokacha shule.”


Milima na mabonde kuwafikia wanafunzi

Katika kuhakikisha jamii inanufaika nchi nzima, mwaka 2025 kampeni ya Kiti Jifunze ya Benki ya CRDB ilipeleka madawati 50 katika Shule ya Msingi Jitegemee na Mlima Reli iliyopo Mbeya idadi sawa na viti na meza zilizopokelewa pia katika Sekondari ya Shewa.

Mwakilishi wa uongozi wa Shule za Sekondari za New Ukonga, Kigenzi Chini na Yongwe zilizopo Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam akizungumza na wanafunzi na wazazi baada ya kupokea msaada wa meza na viti kutoka Benki ya CRDB ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa programu yao ya Keti Jifunze kwa shule mbalimbali nchini.

Kutoka Mbeya, safari iliendelea katika mikoa mingine ya kanda ya nyanda za juu kwa kukabidhi viti na meza 55 kwa Shule ya Sekondari Kagunga Green ya wilayani Tanganyika na idadi kama hiyo kwa Shule ya Wasichana Katavi iliyopo Nsimbo. Wanafunzi wa Sekondari ya Usimbili katika Manispaa ya Mpanda wao walipata viti na meza 56 wakati Shule ya Sekondari ya Wasichana Rukwa iliyopo Sumbawanga ikipokea viti na meza 40. Safari iliishia Kyela katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Mbeya iliyokabidhiwa viti na meza 60.

Kwa kanda ya pwani, Benki ilikabidhi viti na meza 240 kwa sekondari saba ambazo ni Mabwe (Kinondoni), Dovya (Temeke), Viziwaziwa na Mwakamo Ruvu za Kibaha, Dondwe (Mkuranga), Joji Baki ya Mafia na Visiga ya Kisarawe pamoja na Shule ya Msingi Golden English Medium ya Bagamoyo. Shule hizi zote zilipata viti na meza 30 kila moja.

Katika mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara inayounda kanda ya kusini, Benki ilipeleka viti na meza 320 kwa sekondari nane zilizopata viti na meza 40 kila moja. Sekondari zilizonufaika ni Mbinga, Umoja ya Mtwara Mikindani, Chitekete ya Newala, Kiwalala ya Mtama, Mavuji ya Kilwa, Mtyangimbole ya Madaba pamoja na Chandarua na Namihoro za Songea.

Maofisa wa Benki ya CRDB wakiwa katika picha ya pamoja na uongozi na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mbinga iliyopo Halmashauri ya Mji wa Mbinga, mkoani Ruvuma baada ya kugawa meza na viti katika shule hiyo kupitia programu yao ya Keti Jifunze.

Kwa kanda ya magharibi inayojumuisha mikoa ya Kigoma, Tabora, Geita na Shinyanga, Benki ilikabidhi madawati 120 kwa shule tatu za msingi ambazo ni Mkuyuni iliyopo Chato, Ngilimba ya Ushetu na Hanihani ya Igunga pamoja na viti na meza 80 kwa kila sekondari ikiwamo Ugansa ya Kaliua, Nguruka ya Uvinza na Idete ya Uyui pamoja na Ikinda ya Msalala.

Wanafunzi wengine waliokarishwa kwenye samani bora ni wa kanda ya kaskazini ambako madawati 185 yalikabidhiwa kwa shule tano za msingi na viti na meza 250 kwa sekondari tatu. Shule za msingi zilizonufaika ni Mahinge ya Mbulu, Mriti ya Mwanga, Azimio ya Moshi, Emaoi ya Arusha na Uswaa ya Hai. Sekondari ya Wavulana Manyara iliyopo Babati pamoja na Old Mapinduzi ya Handeni na Prof. Adolf Mkenda ya Rombo zilipata viti na meza.

Kutoka Mwanza, Kagera, Simiyu mpaka Mara katika kanda ya ziwa, yalitolewa jumla ya madawati 160 kwa shule nne za msingi na viti na meza 180 kwa shule sita za sekondari. Shule za msingi zilipokea madawati hayo ni Massanga ya Meatu, Kaigara ya Muleba, Igegu ya na Kibimba ya Kyerwa. Kwa sekondari ilikuwa Buhangaza ya Muleba, Kaitoro (Bukoba), Weigita (Tarime), Manchimweru (Bunda), Nyongo (Maswa) na Bulale ya Mwanza.

Maofisa wa Benki ya CRDB wakiwa katika picha ya pamoja na uongozi na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Idete iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, mkoani Tabora baada ya kugawa meza na viti katika shule hiyo kupitia programu yao ya Keti Jifunze.

Katika kanda ya Dar es Salaam, jumla ya viti na meza 350 vilitolewa kwa sekondari za King’azi na Goba Kulangwa za Ubungo wakati Ilala ni Kigenzi, Yongwe na New Ukonga pamoja na sekondari ambazo ni Vumilia Ukooni, Mkamba na Mbutu Mkwajuni.

Ndani ya mikoa inayounda kanda ya kati ambayo ni Dodoma, Singida, Iringa na Morogoro, kulikuwa na viti na meza 370 zilizopelekwa Shule ya Msingi Chemba pamoja na sekondari saba ambazo ni Ikokoto ya Kilolo, Solya ya Manyoni, Bolisa ya Kondoa na Malimbika iliyopo Gairo. Sekondari nyingine ni Kweuma ya Mvomero, Mahutanga ya Ifakara na Mkundi Mlimani ya Morogoro Mjini.

“Tumefika huko kote. Ninafarijika zaidi nikitambua kwamba katika shule tuliyoenda, iwe ya msingi au sekondari, tulikutana na wanafunzi wenye shauku ya kujifunza na kuzipambania ndoto zao, wazazi wenye moyo wa kuwaunga mkono watoto wao na walimu walio tayari kutoa maarifa yao kwa faida ya jamii nzima,”anasema Tully.