Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

GGML ni kampuni inayotekeleza miradi mingi ya kijamii Geita

Muonekano wa mzunguko wa barabara (round about) uliojengwa na kampuni ya GGML kupitia fedha za CSR.


Muktasari:

Kwa mujibu wa sheria mpya ya madini ya mwaka 2017 kifungu cha 105(1) kinazielekeza kampuni zote za uchimbaji wa madini kuandaa mpango wa matumizi ya fedha za huduma kwa kushirikiana na Halmashauri husika kabla ya kuanzisha miradi yoyote ya maendeleo.

Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) ni Mgodi mkubwa zaidi nchini na kwa mujibu wa takwimu mbalimbali za TRA na TEITI (Tanzania Extractive Industry Transparency Initiative) zinaonyesha mgodi huo ndio unaolipa mapato makubwa  kwa Serikali ikilinganishwa na migodi mingine.

Kama ilivyo kinara kwa ulipaji kodi za Serikali, mgodi wa GGML ndio mgodi mkubwa kwa Mkoa wa Geita na ndio unaolipa mapato makubwa yatokanayo na kodi ya huduma pamoja na utekelezaji wa miradi ya kijamii (CSR) ikiwa ni huduma kwa wananchi wanaozunguka mgodi huo.

Kwa mujibu wa sheria mpya ya madini ya mwaka 2017 kifungu cha 105(1) kinazielekeza kampuni zote za uchimbaji wa madini kuandaa mpango wa matumizi ya fedha za huduma kwa kushirikiana na Halmashauri husika kabla ya kuanzisha miradi yoyote ya maendeleo.

Kufuatia mabadiliko ya sheria hiyo, Mkoa wa Geita unaendelea kunufaika na uwepo wa Mgodi wa GGML na tayari utekelezaji wa sheria hiyo ulianza na miradi ya kimkakati imeanza kutekelezwa kwa fedha za CSR.

Wafanyakazi wa mgodi wa dhahabu wa GGM wakishusha miche kwa ajili ya kupanda katika eneo la msitu wa Geita ulioko ndani ya leseni ya kampuni hiyo.

Meneja Mawasiliano kutoka Mgodi wa GGML, Tenga Tenga akizungumzia jinsi kampuni hiyo inavyowajibika katika shughuli za uwekezaji nchini alisema GGML ni kampuni yenye uwekezaji wenye tija katika Mkoa wa Geita na Tanzania kwa ujumla.

Tenga anasema uwekezaji kupitia utaratibu wa Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (Corporate Social Responsibility) ni moja ya uthibitisho wa kuendesha shughuli zao katika njia yenye maadili kwa kufanya kazi na kushirikiana na Serikali na jamii inayowazunguka ili kuleta mabadiliko chanya ya kijamii, kiuchumi, miundombinu na mazingira.

Anasema katika miaka 10 iliyopita kampuni ya GGML imewekeza dola za kimarekani 25 milioni ambazo ni sawa na Sh 56 Bilioni katika miradi mbalimbali ya kijamii yaani CSR.

Kwa mujibu wa Tenga, kwa mwaka 2018 pekee kampuni hiyo iliwekeza Sh 9.2 Bilioni ambazo zimetekeleza miradi katika Halmashauri ya Mji Geita, Halmashauri ya Wilaya Geita na kiasi cha bajeti hiyo kilipelekwa katika Wilaya za Chato, Bukombe na Mbogwe.

Licha ya kampuni hii kuwa katika Wilaya ya Geita, lakini hutoa huduma ya miradi kwenye Halmashauri zote inapowezekana na kuwezesha Mkoa wa Geita kusonga mbele kiuchumi.

Muonekano wa jengo la soko la kisasa linalojengwa mjini Geita kupitia fedha za Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR) kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML). Jengo hilo litakalokuwa na vibanda 80 linatarajiwa kuongeza mapato ya Halmashauri ya mji wa Geita na kukuza uchumi wa wananchi .

Akizungumzia muonekano wa Geita mpya inayoonekana kutokana na miradi mikubwa inayofanywa na fedha za CSR, Tenga alisema GGML imekuwa ikiwekeza katika jamii kwa kuzingatia mijadala inayofanyika na kukubaliana na wananchi na uongozi wa sehemu husika moja kwa moja na Serikali.

Anasema mabadiliko ya sheria mpya ya madini ya mwaka 2017 inahitaji mwekezaji atayarishe mpango kazi wa CSR (CSR plan) ambayo inajadiliwa kwa pamoja na halmashauri husika na kukubaliana vipaumbele kwa mwaka huo.

Anasema kwa mwaka 2018 vipaumbele vilikuwa katika miradi ya Miundombinu kama taa za barabarani, round about, ujenzi wa soko la kisasa  ambapo pia fedha hizo zilielekezwa katika ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa majengo katika nyanja za elimu na afya.

Tenga anasema kama ilivyokuwa mwaka 2018 na sasa wapo kwenye mchakato wa kutengeneza mpango kazi wa CSR kwa mwaka 2019 na utakapokamilika GGML itaendelea kuwa kampuni kinara katika uwekezaji wa miradi inayonufaisha jamii inayowazunguka.

Tenga anasema uwekezaji wa kampuni katika jamii ya Geita unakwenda sambamba na ulipaji kodi unaoongoza nchini katika sekta nzima ya uchimbaji madini, mafuta na gesi.

Anasema katika Ripoti mpya ya Tanzania Extractive Industry Transparency Initiative (TEITI) kwa mwaka 2015/16 katika jumla ya mapato yaliyopatikana katika sekta nzima serikalini, asilimia 47%ya mapato yote kwa jumla yalitolewa na GGML.

Kwa mujibu wa Tenga, GGML imechangia zaidi ya Sh 203 Bilioni serikalini kwa kipindi cha mwaka 2015/16.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel anasema kutekelezwa kwa Sheria mpya ya madini ya mwaka 2017 kutakuwa na mafanikio hasa kwenye fedha zitakazokusanywa ambazo sasa zinaijenga Geita mpya.

Gabriel anasema mabadiliko ya sheria yamewezesha wananchi wanaozunguka migodi kunufaika kwa miradi mikubwa inayotekelezwa kwa fedha hizo.

Anasema Mkoa umeweka vipaumbele kwenye miradi ya kimkakati itakayoonyesha Geita ni mkoa wa Dhahabu kwa kuwa hali ya sasa ya umaskini uliopo haiendani na rasilimali zilizopo.

Anasema fedha za CSR zilikuwa zikitolewa kila mwaka lakini umaskini uliendelea kuwepo kutokana na watumishi wasio waaminifu waliokuwa wakifuja fedha hizo kwa matakwa binafsi.

Gabriel anasema  unapozungumzia maendeleo lazima uwe na msingi wa kusimamia na msingi wa kwanza ni kupambana na rushwa  na mpigaji anayesababisha fedha zinazotolewa zisiwanufaishe wananchi.

 “Kwa sasa tumekubaliana na GGM kukaa meza moja kufanya miradi ya pamoja, nia yao ni njema tatizo lilikuwa kwa watumishi wetu na tayari nimeziagiza halmashauri kuachana na watumishi wanaosababisha wananchi wasinufaike na fedha zinazotolewa kutekeleza miradi,”alisema Gabriel.

Mkuu wa Mkoa alisema GGML katika mwaka 2018 imetoa Sh 9.2 Bilioni ikiwa ni mchango wa kampuni katika kusaidia jamii inayozunguka Mgodi, ni kodi ya huduma kwa mwaka 2018 na mgodi huo ndio ulikuwa mgodi wa kwanza kutekeleza mabadiliko ya sheria mpya.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Modest Apolnary anasema jengo la kwanza la soko kuu la Mkoa ndio ujenzi uko kwa asilimia 50 na kwamba litakapokamilika halmashauri itaingiza mapato ya Sh 100 milioni kwa mwaka.

Anasema miradi hiyo ni mikubwa na ni uwekezaji utakaosaidia halmashauri kujitegemea na kujiendesha kwa shughuli za maendeleo ya wananchi.

Anasema licha ya majengo hayo, pia CSR imefanya mengi katika sekta ya elimu na afya na kuwataka wananchi kuendelea kushirikiana na wawekezaji na Serikali ili kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika mji huo.

Anasema usimamizi usio sahihi ndio ulichangia wananchi kukata tamaa na kuchukia uwekezaji kutokana na usimamizi mbovu wa fedha na kwamba sasa furaha ipo kutokana na miradi kuonekana na inaendana na thamani ya fedha.

Taarifa mbalimbali zinaonyesha GGML tangu ilipoanza uwekezaji wake Tanzania imekuwa ikilipa kodi zote kwa mujibu wa sheria. Kwa mgodi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuangalia vipaumbele kwa pamoja, na kwa mwaka 2018 kuwekeza katika miundombinu ya halmashauri ya mji, muonekano wa mji wa Geita umebadilika kwa haraka.

Ipo miradi ya afya, elimu, miundombinu ya barabara na kilimo pamoja na miradi mikubwa iliyoifanya Geita kuwa mpya ukiwemo mradi wa taa za barabarani, round about ya kisasa yenye mnara  unaoonyesha rasilimali zinazopatikana kwenye mkoa huo.

Mradi Mwingine ni mradi wa majengo mawili ya ghorofa yatakayokuwa na maduka ya biashara yanayotarajiwa kuiwezesha halmashauri ya mji kukusanya mapato na kuongeza mapato ya ndani.

Majengo hayo yaliyobadili muonekano wa mji huo yanajengwa kwa gharama ya Sh 2.3 Bilioni ambazo ni fedha za CSR kutoka GGML

Mradi wa ujenzi wa mzunguko wa kisasa wa barabara (round about) uligharimu zaidi ya Sh, 300 Milioni, na uwekaji wa taa 150 za barabarani zilizogharimu Sh 70 Milioni na hii ni sehemu tu ya miradi mingi inayotekelezwa na fedha za CSR.

Wananchi wanazungumziaje miradi ya CSR kwa mji wa Geita?

Sagal Mganga mkazi wa mjini Geita anasema maendeleo yanayofanywa na kampuni ya GGML yamechangia mji kubadilika kimaendeleo na sasa unaweza kuufananisha na miji mingine mikubwa.

“Naweza kusema nimenufaika na mchango mkubwa wa GGML, ipo miradi mingi inatekelezwa hapa mjini na kila mradi ukiuliza unaona mkono wa GGML ndani yake,”alisema Mganga.

Gilbert George mkazi wa Magogo mjini hapa anasema uwekezaji uliofanywa na kampuni ya GGML umeleta mabadiliko makubwa katika mji huo ikiwa ni maendeleo ya kiuchumi na hata kuchangia ongezeko la watu katika mji huo.

Mradi wa round about unatangaza rasilimali inayopatikana katika Mkoa huo na umefanya mji wa Geita uonekane wa kisasa zaidi.

Gilbert anasema majengo ya ghorofa yatakayotumiwa na wafanyabiashara yataleta mkusanyiko wa wafanyabiashara na itavutia wawekezaji hata kutoka nje ya Mkoa na kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.

Raster Otto mkazi wa mtaa wa Miti mirefu anaipongeza kampuni ya GGML kwa kufanya uwekezaji wenye tija na manufaa kwa wananchi.

Otto anasema ili kazi inayofanywa na GGML ionekane hawana budi kusimamia fedha wanazozitoa ili thamani ya fedha iendane na mradi unaotekelezwa.

Magreth Masanja ni mkazi wa Nyamalembo mjini Geita anashauri Fedha za CSR zitakazotengwa kwa mwaka 2019 ziangalie zaidi mahitaji ya wananchi maskini kama maji safi na salama na miradi ya afya.

Masanja anasema ili mwananchi wa kipato cha chini aweze kuona manufaa ya uwekezaji, halmashauri haina budi kuwashirikisha kabla hawajaanza kutekeleza miradi hiyo.