Safari ya kujenga umakini, kumbukumbu na kujiamini kwa watoto jijini Tanga
Mtoto akipanga kwa umakini na vipande vya kuchezea vya rangi mbalimbali wakati wa zoezi la darasani, akionyesha umuhimu wa ujifunzaji kupitia michezo katika kukuza ubunifu, uwezo wa kutatua changamoto na maendeleo ya awali ya akili.
Clifford Singai, Ofisa Mawasiliano wa Programu ya TangaYetu
Kijiji cha Konazedi kipo umbali wa kilomita kumi na sita kutoka jijini Tanga ambacho barabara yake imekatisha kwenye mapango ya Amboni, ndipo binti mwenye umri wa miaka minne, Aisha anapoanzia siku yake.
Ili kufika Konazedi, utalazimika kupita Amboni na kuuacha nyuma msongamano na pilika pilika za mjini. Kadri unavyozidi kukikaribia kijiji hicho, maduka yaliyo kando ya barabara yanapungua, magari yanakuwa machache na mandhari ya kuvutia ya eneo hilo yanazidi kufunguka.
Konazedi, licha ya kuwa mbali na kitovu cha biashara, ni eneo lililozungukwa na shule nyingi binafsi za awali na ndipo Kituo cha Malezi ya Watoto cha Jamii cha Konazedi kilipo.
Kwa kawaida, Vituo vya Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (ECD) hupatikana maeneo ya mijini, karibu na ofisi na maeneo ya makazi. Kutokana na hilo, Konazedi inatufikirisha sana katika mazingira kiliyopo.
Saa mbili kamili asubuhi, Aisha anavua viatu vyake na kujiunga na wenzake ndani ya duara lililochorwa kwa chaki sakafuni katika darasa lao.
“Anza, njoo ndani, subiri... ndani, nje,” mlezi Madam Vick Mgonja anawaelekeza.
Aisha anainama, maelekezo yanabadilika kwa haraka. Anasimama kidogo, anasikiliza tena, kisha anaruka kuelekea upande sahihi. Mwanafunzi mwenzake anakosea mwelekeo na darasa lote linaangua kicheko.
“Mchezo huu humsaidia mtoto kuwa makini na kusikiliza kwa umakini maelekezo ya mwalimu,” anaeleza Mwalimu Vick.
Licha ya kuonekana kama mchezo wa kawaida tu, lakini ndani ya duara hilo, watoto wanajijengea uwezo wa kuzingatia wanachofundishwa, kudhibiti hisia na kuimarisha kumbukumbu zao.
Wanauzoesha ubongo wao utamaduni wa kusikiliza, kuchakata taarifa na kujibu kwa usahihi. Katika makuzi ya awali ya mtoto, stadi hizi hujenga msingi wa kila kitu kinachofuata.
Kabla ya uwepo wa mifumo rasmi ya kujifunza kwa watoto
Katika kijiji cha Konazedi na maeneo mengine yaliyopo pembezoni mwa miji, mara nyingi ukuaji wa watoto umeshuhudiwa kutokupitia mifumo sahihi ya kujifunza. Watoto wengi wanacheza nyumbani kwao huku wazazi wakiendelea na majukumu yao ya kila siku.
Mlezi Vicky Mgonja akizungumza na watoto wakati wa zoezi la ujifun zaji wa nje ya darasa, akionesha umuhimu wa ushiriki wa watu wazima na jamii katika kusaidia maendeleo ya awali ya mtoto.
Catherine Donato, mmoja wa wazazi katika jamii hiyo, anaelezea changamoto alizokutana nazo mototo wake kabla ya kujiunga na kituo hicho.
“Kabla mtoto wangu hajaanza kuja hapa, kulikuwa na makundi mengi ya watoto mitaani. Alikuwa akizunguka ovyo na kumfuatilia muda wote lilikuwa jambo gumu,” anasema.
Faida za kumleta mtoto kituoni hapo ni nyingi. Baadhi ya watoto wameweza kusoma namba lakini bado wana shida kwenye matumizi yake sahihi.
Wengine wana changamoto ya misamiati au uwezo mdogo wa kuzingatia. Walipoanza shule ya msingi, walimu waliwakuta watoto hao katika viwango tofauti vya utayari wa kujifunza.
Dk Samwel Mtullu, Meneja Mradi wa Taasisi ya United Health for Tanzania Children (UHTC) ambayo ni mshirika wa utekelezaji wa programu ya TangaYetu anasema miaka hiyo ya awali ni muhimu sana kwa mtoto.
“Katika makuzi ya awali ya mtoto, tunajikita zaidi katika ukuaji wa uwezo wa kiakili,” anaeleza. Ananukuu tafiti zinazoonesha kasi kubwa ya ukuaji wa ubongo katika miaka ya mwanzo ya ukuaji wa mtoto.
“Ubongo huongezeka kwa asilimia 50 kufikia miezi 18 na huendelea kukua kwa kiwango kikubwa hadi mtoto anapofikisha miaka sita,” anasema.
Katika kipindi hicho, mazingira yanayochochea ujifunzaji husaidia kujenga miunganiko ya neva inayohusika na kumbukumbu, lugha, umakini na uwezo wa kufikiri.
Bila msukumo huo, watoto huweza kuanza elimu rasmi wakiwa tayari wamechelewa kujifunza mambo ya msingi katika makuzi yao.
Mradi wa Kuimarisha Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto katika Jiji la Tanga kupitia Miradi Inayosimamiwa na Jamii, unaotekelezwa chini ya programu ya TangaYetu, ulianzishwa mahsusi kuziba pengo hilo.
Kwa sasa, vituo tisa vya malezi ya watoto vya jamii na vituo tisa vya elimu ya awali vinafanya kazi katika kata nane za Jiji la Tanga, vikihudumia watoto 260 waliosajiliwa mwaka 2026. Kituo cha Konazedi ni ushahidi kwamba elimu bora ya awali si lazima ipatikane mijini pekee.
Kujifunza kupitia michezo yenye malengo mahsusi
Baada ya kumalizika kwa mchezo wa duara, Aisha anasogea kwenye bango ukutani lenye namba na picha mbalimbali.
“Mtoto anapokuja kwenye bango hili, anasema, ‘Hii ni namba moja na hapa kuna tembo,” anaeleza Mwalimu Vick.
Aisha anafuatilia namba kwa kidole chake na kutaja namba pamoja na mnyama husika. Hafanyi hayo kwa kukariri, bali anaunganisha alama na maana zake, jambo linaloimarisha kumbukumbu na kukuza msamiati wake.
Muda mfupi baadaye, mwalimu anabadilisha zoezi na kuhamia kwenye utambuzi wa wanyama.
“Mtoto, unaweza kuunguruma kama simba?” Mwalimu Vick anauliza.
Aisha anacheka na kuunguruma. Darasa linaendelea kujadili makazi ya wanyama mbalimbali. Pundamilia huishi porini. Sungura anaweza kufugwa nyumbani. Kupitia mazungumzo kama haya, watoto hujifunza kupanga taarifa katika makundi, kukumbuka na kutumia uwezo wa kufikiri.
Katika shughuli nyingine, mlezi Diana Sekinyashi anasimamia michezo ya ujenzi wa maumbo mbalimbali kwa kutumia vizibo maalum.
“Tunawapatia vifaa vya kujengea. Mmoja anajenga nyumba, mwingine anajenga gari,” anasema.
Aisha anapanga vipande kwa umakini. Umbo lake linaporomoka, anasimama, anachunguza na kujaribu tena. Huu ni mfano halisi wa kujifunza kutatua changamoto. Anajaribu, anarekebisha na kujifunza kutokana na matokeo.
Walimu hufuatilia kwa karibu maendeleo ya kila mtoto.
“Tunapowapa kazi na baadaye kuzisahihisha, tunapitia mtoto mmoja mmoja. Hivyo tunafahamu kiwango cha uelewa wa kila mtoto,” anaeleza Diana.
Lengo si kuwaharakisha watoto kufikia hatua zinazofuata, bali kuhakikisha wanaelewa kwa kina kila hatua ya maendeleo yao.
Mabadiliko yanayoonekana
Wazazi wanasema kituo hicho kimekuwa na manufaa makubwa kwenye maendeleo ya watoto hata wanapokuwa majumbani mwao.
“Mwanangu anaporudi nyumbani huanza kuniambia, ‘Mama, leo tumejifunza moja, mbili, tatu,’” anasema Catherine ambaye ameanza kuona mabadiliko ya motto wake. “Uelewa wake umeongezeka tofauti na zamani,” anaongeza.
Khadija Ibrahim Masimba naye anaelezea mabadiliko kama hayo. “Hakuwa anajua kuhesabu hapo awali. Sasa anajua kuhesabu,” anasema.
Pia ameona maendeleo katika matumizi ya lugha. “Anaweza kuzungumza Kiingereza na anaweza kuandika,” anaeleza.
Mabadiliko haya yanaonyesha ukuaji katika maeneo mbalimbali ya uwezo na akili. Watoto wanakumbuka masomo waliyojifunza, jambo linaloimarisha kumbukumbu. Wanatumia misamiati mipya, hivyo kukuza lugha. Wanashiriki michezo na shughuli za ujenzi zinazoboresha uwezo wao wa kutatua changamoto.
Catherine anasema motto wake humwambia kwa msisitizo: “Mama, nipeleke shule.” Shauku hiyo inaonyesha udadisi na kujiamini, sifa ambazo huwezi kuzipima kwa macho lakini zina mchango mkubwa katika ukuaji wa mtoto.
Mabadiliko kwa jamii nzima
Uwepo wa kituo cha ECD Konazedi unaashiria mabadiliko katika namna elimu ya awali inavyoeleweka. Unaonyesha kwamba maendeleo ya kiakili ya mtoto hayapaswi kutegemea ukaribu wa shule ilipo na mji au uwezo wa familia kulipia shule binafsi.
Kwa Dk Mtullu, uwekezaji huu una matokeo ya sasa na ya baadaye. “Tunaona matokeo sasa, lakini pia tunatarajia kuona matokeo makubwa zaidi siku zijazo,” anasema.
Jioni jua linapokuchwa, Aisha anakaa kwa utulivu darasani akisubiria kusimuliwa hadithi. “Mnyama gani anaishi porini?” mwalimu anauliza.
Aisha anainua mkono wake. “Punda milia,” anajibu kwa kujiamini. Ni jibu rahisi. Lakini ndani yake kuna mkusanyiko wa kumbukumbu, uelewa na ujasiri wa kujieleza.
Katika eneo ambalo vituo vya makuzi na maendeleo ya awali ya watoto vilikuwa vichache hapo awali, watoto sasa wanajifunza kusikiliza, kufikiri na kujieleza. Wanajenga msingi muhimu wa mafanikio shuleni na katika maisha yao ya baadaye.
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika
Wakati Afrika ikiadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka 2026 chini ya kaulimbiu isemayo “Kuhakikisha upatikanaji wa huduma za maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi kwa kila mtoto barani Afrika,” simulizi ya Aisha inatukumbusha kwamba watoto hustawi pale misingi ya maendeleo yao inapokuwa imara.
Sambamba na upatikanaji wa maji safi, huduma za usafi wa mazingira na usafi binafsi, fursa za elimu bora ya awali huwasaidia watoto kujenga stadi, kujiamini na kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto ili kufikia uwezo wao kamili.
Na katika nyakati hizo za kila siku, umbali kutoka mjini hauonekani tena kuwa muhimu kuliko mwelekeo wa mabadiliko yanayotokea.
Programu ya TangaYetu inafadhiliwa na Fondation Botnar na kusimamiwa na INNOVEX Development Consulting Limited kwa ushirikiano na Halmashauri ya Jiji la Tanga, kwa lengo la kuifanya Tanga kuwa jiji ambalo vijana wanastawi na kufikia uwezo wao kikamilifu.