Sekta ya kilimo Zanzibar iko kwenye muelekeo mzuri chini ya Idara ya Mipango, Sera na Utafiti
Sekta ya kilimo imeendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Zanzibar, ikiwezesha ajira kwa wananchi wengi na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika usalama wa chakula na maendeleo ya kijamii.
Serikali imeendelea kuweka mikakati madhubuti kuhakikisha sekta hiyo inaimarika na kuwa na mchango mkubwa zaidi katika uchumi.
Ndani ya jitihada hizo, Wizara ya Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo imekuwa na mifumo ya kitaasisi inayohakikisha mipango na sera za kilimo zinatekelezwa kwa ufanisi. Moja ya idara muhimu inayosimamia kazi hiyo ni Idara ya Mipango, Sera na Utafiti.
Idara hii imekuwa kiungo muhimu katika kubuni, kuratibu na kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya kilimo ili kuhakikisha malengo ya Serikali katika sekta hiyo yanafikiwa.
Kupitia mahojiano maalum na Mkurugenzi wa Idara ya Mipango, Sera na Utafiti katika Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Makame Kitwana Makame imebainika kuwa idara hiyo ina nafasi ya kipekee katika kuhakikisha maendeleo ya sekta ya kilimo yanaendeshwa kwa misingi ya mipango na sera zilizo thabiti.
Kuhusu Idara ya Mipango, Sera na Utafiti
Kwa mujibu wa Makame, Idara ya Mipango, Sera na Utafiti ni moja ya idara za msingi ndani ya Wizara ya Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo yenye jukumu la kuhakikisha kuwa shughuli zote za maendeleo ya kilimo zinapangwa, zinatekelezwa na kufuatiliwa kwa ufanisi.
Idara imegawanyika katika divisheni kuu tatu ambazo ni; Divisheni ya Mipango, Divisheni ya Sera na Divisheni ya Utafiti, Ufuatiliaji, Tathmini na Takwimu. Anasema idara hiyo ndiyo kitovu cha uratibu wa mipango ya wizara, kwani ina jukumu la kusimamia utekelezaji mipango ya muda mfupi, wa kati na wa muda mrefu ambayo inaongoza utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo ya kilimo.
“Idara hii inahakikisha kwamba mipango yote ya wizara inaendana na malengo ya maendeleo ya Serikali pamoja na mahi-taji halisi ya wakulima na wadau wa sekta ya kilimo,” anasema Makame.
Anasisitiza kuwa, kupitia idara hiyo, wizara inakuwa na uwezo wa kupanga vipaumbele vya maendeleo, kufuatilia utekelezaji wa miradi na kufanya tathmini ili kubaini mafanikio na changamoto zinazojitokeza.
Majukumu na kazi za idara
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, Idara ya Mipango, Sera na Uta-fiti ina majukumu kadhaa muhimu ambayo yanachangia moja kwa moja katika maendeleo ya sekta ya kilimo Zanzibar.
Moja ya majukumu yake makuu ni kuandaa na kuratibu mipango ya maendeleo ya wizara. Hii inahusisha kuandaa bajeti za kila mwaka, mipango ya maendeleo pamoja na mikakati ya muda mrefu ya sekta ya kilimo. Pia, idara hiyo ina jukumu la kuandaa na kusimamia utekelezaji wa sera mbalimbali zinazohusu kilimo.
Sera hizi hutoa muelekeo wa maendeleo ya sekta ya kilimo na kuhakikisha kuwa shughuli zote za kilimo zinaendeshwa kwa kuzingatia miongozo ya Serikali. Aidha, idara hiyo hushiriki katika kuratibu tafiti mbalimbali zinazolenga kubaini changamoto na fursa zilizopo katika sekta ya kilimo. Tafiti hizi husaidia Serikali kufanya maamuzi sahihi kuhusu sera na mipango ya maendeleo.
Makame anaeleza kuwa idara hiyo pia inasimam-ia shughuli za ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo ya kilimo. “Tunafuatilia utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali za wizara ili kuhakikisha kuwa malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa na rasilimali zinazotumika zinaleta matokeo yaliyotarajiwa.”
Katika kuhakikisha malengo ya maendeleo ya kilimo yanafikiwa, Idara ya Mipango, Sera na Utafiti hufanya kazi kwa karibu na idara nyingine ndani ya Wizara ya Kilimo pamoja na taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi.
Makame anasema ushirikiano huo ni muhimu kwa sababu maendeleo ya kilimo yanahitaji juhudi za pamoja kutoka kwa wadau mbalimbali.
“Tunafanya kazi kwa karibu na idara zinazoshughulika na uzalishaji wa mazao, huduma za ugani, mifugo, misitu, umwagiliaji, utafiti wa kilimo na hata taasisi za fedha ili kuhakikisha mipango ya maendeleo ya kilimo inatekelezwa kwa ufanisi,” anasema.
Pia idara hiyo hushirikiana na wizara nyingine za Serikali, mashirika ya kimataifa pamoja na asasi za kiraia zinazojihusisha na maendeleo ya sekta ya kilimo. Kupitia ushirikiano huo, wizara imekuwa na uwezo wa kupata rasilimali, utaalamu na teknolojia zinazosaidia kuboresha sekta ya kilimo Zanzibar.
Nafasi ya Idara katika kukuza sekta ya kilimo
Kwa mujibu wa Makame, Idara ya Mipango Sera na Utafiti ina nafasi muhimu katika kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa kwa kasi na kuleta manufaa kwa wananchi. Anasema kupitia mipango na sera zinazoandaliwa na kusimamiwa na idara hiyo, wakulima wanapata mazingira bora ya kufanya shu-ghuli zao za kilimo.
“Tunajitahidi kuhakikisha kuwa sera na mipango tunayoandaa inasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao, kuboresha masoko ya bidhaa za kilimo na kuongeza kipato cha wakulima,” anasema.
Pia idara hiyo inahakikisha kuwa sekta ya kilimo inaendeshwa kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia za kisasa na mbinu bora za kilimo ambazo zinaweza kuongeza tija katika uzalishaji.
Katika miaka ya karibuni, Idara ya Mipango, Sera na Utafiti Zanzibar imekuwa mstari wa mbele katika kusimamia utekelezaji wa mipango na sera mbalimbali za maendeleo ya kilimo Zanzibar.
Makame anataja baadhi ya mipango hiyo kuwa ni pamoja na mikakati ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula, kuimarisha huduma za ugani kwa wakulima pamoja na kuboresha miundombinu ya kilimo.
Pia idara hiyo imesimamia utekelezaji wa mipango inayolenga kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kupitia usindikaji na masoko. Kupitia sera na mipango hiyo, wakulima wengi Zanzibar wameweza kuongeza uzalishaji na kipato chao.
Mambo ambayo idara inajivuniaKwa mujibu wa Makame, Idara ya Mipango, Sera na Utafiti inajivunia mchango wake katika kuboresha mfumo wa upangaji na usimamizi wa maendeleo ya kilimo Zanzibar.
Anasema moja ya mafanikio makubwa ya idara hiyo ni kuimarika kwa mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya kilimo, jambo ambalo limeongeza uwazi na ufanisi katika matumizi ya rasilimali.
“Tunajivunia kuona kwamba mipango mingi ya maendeleo ya kilimo inayo-tekelezwa sasa ina matokeo chanya kwa wakulima na jamii kwa ujumla,” anasema.
Aidha, idara hiyo imefanikiwa kuimarisha ushirikiano kati ya wizara na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo, hali ambayo imeongeza uwekezaji katika sekta hiyo. Aidha, katika kipindi cha miaka ya karibuni, idara hiyo imepata mafanikio kad-haa yanayoonekana katika maendeleo ya sekta ya kilimo Zanzibar.
Miongoni mwa mafanikio hayo ni kuongezeka kwa uzalishaji wa baadhi ya mazao ya chakula, kuimarika kwa mifumo ya upangaji wa maendeleo ya kilimo pamoja na kuongezeka kwa miradi ya uwekezaji katika sekta hiyo.
Makame anasema mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano mzuri kati ya Serikali, wakulima na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Pamoja na mafanikio hayo, Makame anakiri kuwa bado kuna changamoto kadhaa zinazokabili idara hiyo katika utekelezaji wa majukumu yake. Moja ya changamoto kubwa ni upungufu wa rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza baadhi ya mipango ya maendeleo ya kilimo. Pia kuna changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaathiri uzalishaji wa mazao na hivyo kuhitaji mipango mipya ya kukabiliana nayo.
Aidha, ongezeko la mahitaji ya huduma za kilimo kutoka kwa wakulima linaweka shinikizo kubwa kwa wizara kuhakikisha huduma hizo zinapatikana kwa wakati. Ili kukabiliana na changamoto hizo, Idara ya Mipango, Sera na Utafiti imeweka mikakati mbalimbali inayolenga kuimarisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya kilimo.
Moja ya mikakati hiyo ni kuimarisha ushirikiano na wadau wa maendeleo ili kuongeza rasilimali kwa ajili ya miradi ya kilimo.
Pia idara hiyo inaendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za kilimo ili kusaidia katika kupanga mipango bora ya maendeleo.
Makame anasema wizara pia inaendelea kuweka mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuhamasisha matumizi ya mbegu bora na mbinu za kilimo zinazohimili ukame.
Anasema idara ya Mipango, Sera na Utafiti inaendelea kuwa mhimili muhimu katika kusimamia na kuongoza maendeleo ya sekta ya kilimo Zanzibar.
Kupitia mipango madhubuti, sera thabiti na ushirikiano na wadau mbalimbali, idara hiyo inaendelea kuhakikisha kwamba sekta ya kilimo inachangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi.
Kwa kuendelea kuimarisha mifumo ya upangaji na usimamizi wa maendeleo ya kilimo, Zanzibar itaweza kufikia malengo yake ya kuwa na sekta ya kilimo yenye tija, inayochangia kikamilifu katika usalama wa chakula na maendeleo ya uchumi wa visiwa hivyo.
“Lengo letu ni kuona sekta ya kilimo inakuwa ya kisasa, yenye tija na inayowanu-faisha wakulima pamoja na Taifa kwa ujumla,” anasisitiza Makame.