Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanroads yaweka mbele ulinzi  wa mazingira na jamii Dira 2050

Meneja wa Mazingira na Jamii wa Tanroads, Zafarani Madayi

Wakati Tanzania ikiendelea kuwekeza mabilioni ya shilingi katika ujenzi na uboreshaji wa barabara, madaraja na vituo vya mizani, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeeleza mafanikio ya miradi hiyo hayaangaliwi tu kwa kiwango cha miundombinu inayojengwa, bali pia kwa namna inavyolinda mazingira, kunufaisha jamii na kuchangia maendeleo ya uchumi.

Ili kuhakikisha hilo linafanikiwa, TANROADS imekuwa ikifanya tathmini za athari za mazingira na jamii kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi yake mbalimbali nchini.

Meneja wa Mazingira na Jamii wa TANROADS, Zafarani Madayi anasema kila mradi mkubwa wa miundombinu, iwe ni barabara, daraja au kituo cha mizani, hutakiwa kupitia mchakato wa tathmini ya athari kwa mazingira na jamii kabla ya kuanza kutekelezwa.

Tathmini hiyo huangalia athari zinazoweza kujitokeza katika mazingira ya eneo husika kwa wananchi wanaoishi karibu na mradi, pamoja na athari za kiuchumi kwa jamii na taifa kwa ujumla.

“Tathmini hizo hufanyika kwa kuzingatia sheria za Tanzania pamoja na miongozo ya kimataifa inayotumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo,”anasema Zafarani.

Anasema kwa kawaida, kazi hiyo hufanywa na wataalamu washauri wa mazingira ambao hukusanya taarifa mbalimbali, kufanya tafiti na kushirikisha wadau wa maeneo husika ili kupata maoni yao kuhusu mradi unaotarajiwa kutekelezwa.


Ripoti ya tathmini ya mazingira

Anasema baada ya kukamilika kwa mchakato huo, huandaliwa taarifa maalumu inayojulikana kama Taarifa ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (Environmental Impact Assessment Report – EIA Report). Taarifa hiyo ndiyo msingi wa kufanya uamuzi kuhusu namna mradi utakavyotekelezwa bila kuathiri mazingira na jamii.

Sambamba na hilo, huandaliwa pia Mpango wa Usimamizi wa Mazingira (Environmental Management Plan – EMP) ambao huainisha hatua za kuchukua ili kudhibiti changamoto zinazoweza kujitokeza na kuboresha faida zinazotokana na mradi.

Kwa mujibu wa meneja huyo, mpango huo hufafanua kwa kina majukumu ya kila mdau katika kusimamia masuala ya mazingira wakati wa utekelezaji wa mradi.

Mpaka sasa TANROADS ina jumla ya Hati 93 za mazingira (EIA certificate s) kutoka NEMC na miradi 96 imesajiliwa NEMC kwa ajili ya utekelezaji wa miradi yake.


Mikakati ya kudhibiti athari za mazingira

Anasema endapo tathmini itaonesha shughuli za ujenzi zitasababisha vumbi kutokana na uchimbaji wa udongo na upitishaji wa magari makubwa, mkandarasi hupewa maelekezo ya kumwagilia maji mara kwa mara katika maeneo hayo ili kupunguza kiwango cha vumbi kinachoweza kuathiri wananchi na mazingira.

“Ikiwa tathmini itaonesha uwezekano wa kuongezeka kwa kelele kutokana na matumizi ya mitambo ya ujenzi, mkandarasi hulazimika kufanya matengenezo ya mara kwa mara ya vifaa vyake pamoja na kutumia mashine zinazokidhi viwango vya uhifadhi wa mazingira ili kupunguza usumbufu kwa wananchi wanaoishi karibu na eneo la mradi,”anasema Zafarani.

Hatua hizo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa usimamizi wa mazingira unaolenga kuhakikisha changamoto zote zilizobainishwa zinadhibitiwa kwa wakati.


Miradi kuibua ajira na fursa za biashara

Mbali na kudhibiti athari hasi, TANROADS huweka mikakati ya kuhakikisha manufaa ya miradi hiyo yanafika kwa wananchi wa maeneo husika.

Zafarani anasema moja ya maeneo yanayopewa kipaumbele ni utoaji wa ajira, katika utekelezaji wa miradi mingi, wananchi wanaoishi kandokando ya maeneo ya mradi hupewa nafasi ya kwanza katika ajira zinazohitaji nguvu kazi za kawaida na huduma nyingine zinazohusiana na utekelezaji wa mradi.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha jamii zinazopokea miradi zinanufaika moja kwa moja na uwekezaji unaofanyika katika maeneo yao.

Meneja huyo anaeleza kuwa manufaa ya kiuchumi yanayotokana na miradi hiyo hayaishii kwa watu wanaoajiriwa moja kwa moja na wakandarasi. Shughuli za ujenzi huibua pia fursa nyingi za biashara kwa wananchi wa maeneo husika.

“Kwa mfano, kuwepo kwa wafanyakazi wengi katika eneo la mradi huongeza mahitaji ya chakula, huduma za malazi, usafiri na bidhaa mbalimbali.”

Anasema hali hiyo huwapa wananchi nafasi ya kuanzisha au kupanua biashara zao na hivyo kuongeza kipato cha familia na kuchochea uchumi wa eneo husika.

“Wapo wananchi wanaofungua migahawa midogo, kuuza vyakula, vinywaji na bidhaa mbalimbali kwa wafanyakazi wa miradi. Wengine hupangisha nyumba au vyumba kwa wataalamu na wafanyakazi wanaotoka nje ya eneo husika, huduma zote hizo huchangia kuunda ajira zisizo za moja kwa moja zinazotokana na uwepo wa mradi,”anasema.


Sheria na kanuni zinazoongoza utekelezaji

Katika kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo, anasema TANROADS huzingatia kikamilifu matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 pamoja na maboresho ya mwaka 2025.

Anasema taasisi hiyo huzingatia Kanuni za Tathmini na Ukaguzi wa Athari za Mazingira za mwaka 2005 zilizoboreshwa mwaka 2018.

“Mbali na sheria hizo, miradi ya miundombinu huzingatia pia sheria nyingine za kisekta zinazohusu misitu, madini, ardhi na rasilimali nyingine za asili ili kuhakikisha maendeleo yanafanyika bila kuharibu mazingira,”anasema.

Kadhalika, TANROADS huzingatia miongozo ya taasisi mbalimbali za kimataifa zinazofadhili miradi ya maendeleo. Taasisi hizo ni pamoja na Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na wadau wengine wa maendeleo ambao huhitaji tathmini za athari za mazingira na kijamii kufanyika kabla ya kutoa ufadhili wa miradi.


Kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Wakati huo huo, mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuwa moja ya changamoto kubwa zinazoathiri miundombinu ya usafiri duniani, ikiwemo Tanzania.

Kutokana na hali hiyo, TANROADS imeanza kuzingatia zaidi suala la kujenga miundombinu inayoweza kustahimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wa kihandisi, anasema usanifu wa barabara na madaraja umeboreshwa ili kuhimili mafuriko makubwa na hali nyingine za hewa zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Maboresho hayo yanahusisha kuongeza uimara wa miundombinu, kuongeza urefu wa madaraja katika maeneo hatarishi na kuweka nafasi kubwa zaidi kati ya nguzo za madaraja ili kuruhusu maji na takataka kupita kwa urahisi wakati wa mafuriko.


Upandaji miti kulinda miundombinu

Kwa upande wa mazingira, TANROADS imeendelea kutekeleza kampeni za upandaji miti katika hifadhi za barabara na maeneo mengine yanayozunguka miradi yake.

Zafarani anasema upandaji miti unalenga kupunguza mmomonyoko wa udongo, kuimarisha uoto wa asili na kusaidia kunyonya hewa ukaa ambayo ni moja ya vichocheo vya mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, uwepo wa miti na nyasi kandokando ya barabara husaidia kudhibiti kasi ya maji ya mvua na kupunguza uwezekano wa kutokea kwa mafuriko yanayoweza kuharibu miundombinu.


Dhamira ya maendeleo endelevu

Kupitia hatua hizo zote, TANROADS inaendelea kuhakikisha kuwa maendeleo ya miundombinu nchini yanaenda sambamba na ulinzi wa mazingira, ustawi wa jamii na ukuaji wa uchumi.

“Mtazamo huo unalenga kuhakikisha kuwa miradi inayotekelezwa leo inawanufaisha Watanzania wa sasa bila kuhatarisha uwezo wa vizazi vijavyo kufaidika na rasilimali za mazingira zilizopo.”


TANROADS yavuka lengo la upandaji miti

TANROADS imefanikiwa kuvuka lengo lake la upandaji miti baada ya kupanda zaidi ya miti 160,000 nchini, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa uhifadhi wa mazingira.

Awali, anasema ilikuwa imepanga kupanda miti 40,000 katika maeneo ya hifadhi ya barabara, lakini idadi hiyo imevukwa kwa zaidi ya mara nne kutokana na ushirikiano wa watendaji wake nchini.

Katika utekelezaji wa mpango huo, TANROADS imehusisha wananchi kupitia vikundi mbalimbali ikiwepo Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Makutupola na wananchi wa kawaida kwa kupewa jukumu la kupanda na kutunza miti katika maeneo ya miradi ya barabara.

“Vikundi hivyo vinashiriki moja kwa moja katika utekelezaji wa miradi ili kuhakikisha jamii inanufaika kiuchumi na pia kushiriki katika utunzaji wa mazingira,”anasema.


Miradi ya kijani Dodoma na Pangani–Tanga

TANROADS inatekeleza miradi maalumu ya kijani katika barabara kubwa ikiwemo Dodoma Outer Ring Road na Pangani–Tanga, ambapo wananchi wanashiriki katika upandaji na umwagiliaji wa miti.

Kila mradi wa barabara unahusisha kipengele cha upandaji miti na utunzaji wa mazingira ndani ya mkataba wake.

Shughuli mbalimbali za ujenzi kama uchimbaji wa changarawe, mchanga, vifusi na maeneo ya kukusanyia maji husababisha athari katika mazingira.

Anasema ili kukabiliana na athari hizo, huweka gharama maalumu katika mikataba ya ujenzi kwa ajili ya kurejesha maeneo yaliyoharibiwa kwa kupanda miti, kuyasawazisha na kuyaboresha ili yabaki katika hali nzuri na salama.

“Katika kila mkataba kuna kipengele cha mazingira chenye bajeti yake. Fedha hizo hutumika kupanda miti, kufanya landscaping na kurejesha maeneo yaliyoharibiwa wakati wa ujenzi,” anasema.

Pia, anasema kila mkandarasi anatakiwa kuwa na mtaalamu wa mazingira na mtaalamu wa masuala ya jamii watakaohakikisha masharti yote ya mazingira na kijamii yaliyowekwa katika mkataba yanatekelezwa ipasavyo.

Anasema mikataba yote ya ujenzi ina kanuni za maadili na utendaji (Code of Conduct) zinazohusu mazingira, afya, usalama mahali pa kazi na masuala ya kijamii ambazo wafanyakazi wote wanapaswa kuzifuata.

“Kila mfanyakazi anatakiwa kusaini kanuni hizi, hii ni kunamaanisha ameonyesha dhamira ya kuzitekeleza, akishindwa kufanya hivyo atakuwa amekiuka masharti ya kazi,” anaesema.

Kwa mujibu wa meneja huyo, hatua zinazoweza kuchukuliwa kwa mkandarasi anayekiuka masharti ya mazingira ni pamoja na kusimamishwa kwa kazi, kukatwa sehemu ya malipo au hata kuzuiwa kushiriki miradi mingine nchini endapo ukiukwaji huo utajirudia.

Mbali na usimamizi wa mazingira katika miradi ya kawaida ya barabara, anasema TANROADS pia inatekeleza miradi maalumu ya uhifadhi wa mazingira kupitia Mradi wa Barabara ya Mzunguko wa Nje wa Jiji la Dodoma (Dodoma Outer Ring Road).

Mradi huo unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kushirikiana na Global Environment Facility (GEF), ambao unalenga kuimarisha mazingira sambamba na maendeleo ya miundombinu ya usafiri.

Katika utekelezaji wake, anasema mradi huo unahusisha wadau mbalimbali wakiwamo Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Wizara ya Ujenzi, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa (TMA), NCC na TAFORI.

Kwa upande wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, anasema imepewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa baadhi ya shughuli za mazingira zikiwamo bustani ya mimea ya asili (Botanical Garden) na utungaji wa kanuni ndogo za usimamizi wa mazingira jijini humo.

Kwa upande wa TMA, anasema taasisi hiyo inasaidia masuala ya hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi, huku NCC ikipewa jukumu la kuandaa miongozo ya ujenzi itakayosaidia kuimarisha mipango ya makazi na miundombinu nchini.

“TAFORI imepewa jukumu la kufanya tafiti za aina za miti inayoweza kustawi katika mazingira ya Dodoma na kushiriki katika shughuli za kijani zinazolenga kuongeza uoto wa asili katika jiji hilo,”anasema.

Kwa ujumla, anasema ushirikiano wa taasisi hizo una lengo la kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa kuzingatia misingi ya uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.


Malengo mwaka 2026/27

Baada ya mafanikio ya kupanda zaidi ya miti 160,000 katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha, TANROADS imejiwekea lengo jipya la kupanda miti milioni mbili kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Taasisi hiyo imesema itaendelea kuboresha mikakati yake ili kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa kupitia miradi ya barabara inayoendelea nchini.


Mandhari ya kisasa kwenye barabara za mijini

Katika maeneo ya mijini, inaendelea kuboresha mandhari (landscaping) kwenye barabara mbalimbali, hususani njia za mabasi yaendayo haraka (BRT) jijini Dar es Salaam.

Mpango huo unahusisha upandaji wa miti, nyasi, maua na vichaka kwa lengo la kupendezesha miji na kuboresha mazingira.


Mizani yachangia uhifadhi wa mazingira

Anasema usimamizi wa vituo vya mizani unachangia katika uhifadhi wa mazingira, sambamba na jukumu la kulinda miundombinu ya barabara.

Kwa mujibu wa taasisi hiyo, magari yanayobeba mizigo kupita kiasi hutumia mafuta mengi zaidi na kuongeza uzalishaji wa hewa ukaa, hali inayochangia mabadiliko ya tabianchi.

Udhibiti wa uzito wa magari unasaidia kupunguza matumizi ya mafuta na hivyo kupunguza uchafuzi wa mazingira.


Usalama na afya mahali pa kazi

Katika utekelezaji wa miradi tumeweka mpango na bajeti kwa ajili ya Afya na usalama mahali pa kazi. Kila mradi unawekewa bajeti ya kukabiliana na kuenea kwa magonjwa ambukizi na yasiyoambukiza na hasa UKIMWI, magonjwa ya zinaa, Kifua kikuu, korona nk kwa kutoa elimu, kuhamasisha kuhusu kujilinda, kupima kwa hiyari na kugawa Kondom kwa wafanyakazi wa mradi na wanajamii karibu na mradi husika.

Aidha, mkandarasi ana jukumu la kuimarisha usalama mahali pa kazi kwa kugawa vifaa kinga (PPE) kama kofia ngumu, viatu, barakoa nk.

Mkandarasi anatakiwa kuweka mazingira ya kazi na Kambi safi na salama wakati wote kwa kuweka sehemu za kukusanya taka ngumu, vizima moto, alama sehemu hatarishi, nk.


Changamoto zinazowakabili na utatuzi

TANROADS inaendelea kutekeleza majukumu ya kuhifadhi na kuboresha mazingira katika hifadhi za barabara kupitia upandaji wa miti, nyasi na vichaka pamoja na matengenezo ya miundombinu ya mazingira ya barabara. Hata hivyo, utekelezaji wa shughuli hizi unakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazochangia kudhoofisha juhudi hizo.

Zafarani anasema miongoni mwa changamoto ni uelewa mdogo wa baadhi ya wananchi kuhusu umuhimu wa upandaji wa miti, nyasi na vichaka katika hifadhi za barabara.

“Katika baadhi ya maeneo, mimea inayopandwa huharibiwa na mifugo inayolishwa ndani ya hifadhi za barabara, hali inayosababisha kupungua kwa idadi ya miti inayotarajiwa kukua na kufikia malengo yaliyowekwa ya uhifadhi wa mazingira,”anasema.

Changamoto nyingine anasema uchomaji moto katika maeneo ya hifadhi za barabara ambao huathiri nyasi, vichaka na miti iliyopandwa, hivyo kupunguza mafanikio ya juhudi za kuboresha mazingira.

Hali hii husababisha baadhi ya maeneo yaliyoboreshwa kurejea katika hali ya awali kutokana na uharibifu unaotokana na moto. TANROADS inakabiliwa na changamoto ya ukataji wa miti katika maeneo ya hifadhi za barabara, baadhi ya miti iliyopandwa au iliyopo katika maeneo hayo hukatwa bila idhini, jambo linalopunguza mchango wa miti katika kuboresha mazingira na mandhari ya barabara.

Mbali na hilo anasema katika usimamizi wa miundombinu ya mazingira ya barabara, changamoto kubwa imekuwa utupaji holela wa taka katika mitaro, makalvati na madaraja.

“Taka za majumbani, kilimo na shughuli nyingine za kibinadamu hutupwa katika miundombinu na kusababisha kuziba kwa njia za maji. Matokeo yake ni kuongezeka kwa mafuriko na uharibifu wa miundombinu ya barabara wakati wa mvua kubwa,”anasema Zafarani.

Pia, anasema kumekuwapo na changamoto ya shughuli zisizoidhinishwa ndani ya hifadhi za barabara, ikiwemo uchimbaji wa udongo, uwekaji wa vifaa mbalimbali na matumizi mengine yasiyozingatia taratibu zilizowekwa.

Shughuli hizo huathiri usalama wa miundombinu ya barabara na mazingira yake. Licha ya changamoto hizo, anasema TANROADS imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira ya barabara na kushirikisha vikundi vya vijana na wanawake katika shughuli za upandaji miti na usafi wa mazingira.

“Ushirikiano wa wananchi umeonekana kuwa nyenzo muhimu katika kuhakikisha mazingira ya barabara yanabaki salama, safi na endelevu kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla,”anasema.