TCAA CCC kuzindua kampeni kubwa ya msaada wa kisheria kwa watumiaji wa huduma za usafiri wa anga
Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa (kushoto) akisalimiana na Katibu Mtendaji wa TCAA CCC, Innocent Kyara (kulia) katika moja ya mikutano wa tathmini ya sekta ya uchukuzi.
Katika kipindi ambacho usafiri wa anga unaendelea kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi nchini, umuhimu wa kulinda haki, usalama na ustawi wa watumiaji umeongezeka kwa kasi na kuwa ajenda muhimu katika sera za kitaifa.
Dira ya Maendeleo 2050 na Ilani ya CCM 2025–2030 zinatambua kuwa ulinzi wa mtumiaji ni sehemu muhimu ya mageuzi ya sekta ya huduma, hivyo kutoa msingi thabiti wa ubora, ushindani na uwazi katika usafiri wa anga.
Wakili Karen Luoga (kulia) na Rashid Mngoya (katikati) kutoka kitengo cha malalamiko (CCU) wakimskiliza raia wa kigeni alipotembelea dawati la TCAA CCC kwa maelezo na msaada wa kisheria.
Kwa kutambua umuhimu huo, Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Anga (TCAA CCC), kuanzia Januari 2026, limejipanga kuzindua kampeni kubwa ya utoaji wa msaada wa kisheria kwa abiria wa usafiri wa anga. Hatua hii inaashiria mwelekeo mpya na wa kimkakati katika kulinda maslahi ya mtumiaji wa huduma za usafiri wa anga nchini.
Kampeni hii imejengwa juu ya ukweli kwamba abiria wengi wanakumbana na changamoto kama ucheleweshaji au kufutwa kwa safari, kupotea kwa mizigo, na huduma zenye ubora hafifu lakini wanashindwa kuchukua hatua stahili ya kulinda maslahi yao kutokana na kutofahamu haki zao na utaratibu wa kudai haki zao pindi changamoto husika zinapotokea.
Takwimu za IATA zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 25 ya abiria hupitia matatizo yanayohitaji ufafanuzi wa kisheria, lakini chini ya asilimia 10 tu ndiyo huutafuta au kuupata.
Hivyo, TCAA CCC inalenga kupanua wigo wa haki, uwazi na uwajibikaji katika sekta, huku ikipunguza pengo la uelewa na kuwawezesha abiria kuchukua hatua sahihi wanapokutana na usumbufu.
Katika mahojiano maalumu na Gazeti hili, Katibu Mtendaji wa TCAA CCC, Innocent Kyara, alisema msaada wa kisheria utaanza kutolewa mara tu baada ya kukamilika kwa mafunzo ya maafisa wa msaada wa kisheria na kufunguliwa kwa madawati na vituo maalumu vya utoaji wa msaada wa kisheria katika viwanja vya ndege, pamoja na njia za ushauri mtandaoni.
“Katika mwezi wake wa kwanza wa utekelezaji wa kampeni hii, Baraza linalenga kutoa huduma kwa watumiaji zaidi ya 1,500, na ndani ya mwaka mmoja kufikia zaidi ya watumiaji 20,000 kupitia mawasiliano ya ana kwa ana pamoja na mifumo ya kidijitali,” amesema Kyara.
Kupitia madawati ya utoaji wa msaada wa kisheria, wataalamu wa sheria na haki za watumiaji wa usafiri wa anga watatoa mwongozo wa papo kwa papo bila malipo yoyote kwa abiria.
Huduma hizi zitawekwa karibu na wananchi kupitia viwanja vya ndege na majukwaa ya mtandaoni ili kuhakikisha kila abiria anapata usaidizi sahihi kwa haraka.
Kyara amebainisha kuwa madawati haya yataongeza uelewa wa haki, kupunguza maumivu ya kimya kimya na kuwasaidia abiria kujua hatua za kuchukua wanapopata usumbufu. Kampeni pia itahusisha utetezi wa kimkakati (strategic litigation) kwa kesi zenye maslahi mapana ya umma.
Amesema “Kwa sasa tunapitia Sheria na Kanuni zote zinazotumika katika utoaji wa huduma ya usafiri wa anga, ikiwemo mikataba ya usafirishaji (conditions of carriage) ya watoa huduma (mashirika ya ndege) ili kubaini vifungu vinavyo mkandamiza mtumiaji wa huduma ya usafiri wa anga.”
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Abdul Athumani Mombokaleo (kushoto) akizungumza na baadhi ya watumishi wa TCAA CCC, Bi. Debora Mligo (katikati) na Bi Lucy Shayo (kulia) katika dawati maalumu la utoaji wa elimu kwa umma.
Endapo vitabainika vipengele vinavyominya haki za abiria, Baraza litaishauri Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kuchukua hatua za kiudhibiti na inapobidi, kuomba tafsiri ya mahakama ili kupata maamuzi yatakayoboresha mfumo wa huduma na kuongeza uwajibikaji.
Njia hii imekuwa ikitumika duniani kuleta mageuzi makubwa kupitia kesi chache zenye uzito.
Katika upande wa elimu, kampeni itatumia warsha, vipindi vya televisheni na redio, mitandao ya kijamii na machapisho mahsusi kuongeza uelewa wa haki za abiria chini ya Sheria ya Usafiri wa Anga, Kanuni za Usafirishaji na Mikataba ya Kimataifa kama Montreal Convention.
Zaidi ya asilimia 60 ya abiria hawajui haki zao, jambo linalosababisha wengi kuathirika kimya kimya. Kupitia kampeni hii, mwamko unatarajiwa kuongezeka kwa kiwango kikubwa, hivyo kupunguza malalamiko yasiyozingatia taratibu na kuboresha mawasiliano kati ya abiria na watoa huduma.
Kwa upande wa mashirika ya ndege na sekta kwa ujumla, kampeni hii inaleta faida nyingi. Abiria wenye uelewa na mwongozo sahihi watatoa malalamiko kwa utaratibu unaotambulika, na hivyo kurahisisha utatuzi wa changamoto na kupunguza migogoro.
Wakati kampeni hii inaonekana kulenga watumiaji binafsi, ukweli ni kwamba faida zake ni za sekta nzima. Elimu na uwazi huongeza uaminifu wa abiria, jambo ambalo ni msingi wa ukuaji wa biashara za usafiri wa anga.
Mashirika ya ndege yanapowajibika, huongeza uwazi na kuzingatia viwango vilivyowekwa hivyo kuleta ushindani chanya unaochochea ubunifu, usalama, na ufanisi.
Aidha, kuwepo kwa mfumo madhubuti wa msaada wa kisheria kunasaidia kutatua malalamiko kwa wakati, kupunguza migogoro, na kusaidia mashirika ya anga kupata mrejesho wa kuboresha huduma.
Utapenda kufahamu kuwa, mrejesho wenye msukumo wa kisheria kutoka kwa Watumiaji utawasaidia watoa huduma kuboresha mifumo yao, hivyo kuinua ubora wa huduma kwa wasafiri, hali inayoweza kuongeza idadi ya abiria wanaotumia usafiri wa anga na hivyo kuchangia ukuaji wa kiuchumi katika nchi.
Kwa ujumla, kampeni hii inabeba ujumbe muhimu kwa abiria kutambua nafasi yao kwamba wao ni wadau wenye thamani katika sekta ya anga. Kupitia elimu, sheria na utetezi, watumiaji watapata nafasi ya kusikilizwa na kulindwa ipasavyo.
Hii ni hatua muhimu katika kujenga sekta ya usafiri wa anga yenye usawa, haki na ustawi kwa wote, hususan katika enzi ya usafiri unaovuka mipaka na unaohitaji mifumo madhubuti ya usimamizi na ulinzi wa haki.
Baraza linatoa wito kwa watumiaji wote kujitokeza na kutumia huduma hizi za msaada wa kisheria badala ya kukaa kimya wanapokutana na usumbufu unaoathiri haki zao.
Vilevile, mashirika ya ndege na watoa huduma wanahimizwa kushirikiana, kuongeza uwazi na kuzingatia sheria na viwango vya huduma, pamoja na kuboresha mifumo yao pale panapobainika changamoto.
Kampeni hii inalenga kuimarisha sekta ambayo inatambua kuwa ustawi wa mtumiaji ndiyo msingi wa maendeleo endelevu na ukuaji wa usafiri wa anga nchini.
Kwa mawasiliano na elimu zaidi, wananchi wote wanaweza kutembelea tovuti yetu (www.tcaa-ccc.go.tz) au kuwasiliana nasi kupitia mitandao yetu ya kijamii ya Instagram (@tcaa_ccc), Mtandao X (@ tcaa_ccc1), YouTube (@tcaa_consumerconsultativecouncil) au kupiga simu ya bure 0800 110 190 au kuwasiliana nasi kupitia anuani iliyoainishwa hapa chini;-
Katibu Mtendaji,
Baraza la Ushauri la Watumiaji Huduma za Usafiri wa Anga
(TCAA CCC),
Majengo ya TBA Na. L1,
Kiwanja Na. 6/2,
Mtaa wa Kilimani, Barabara ya Ali Hassan Mwinyi,
S.L.P. 12242,
14110 DAR ES SALAAM.