Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TEN/MET inavyojenga mustakabali wa mtoto wa Kitanzania kupitia elimu jumuishi na mazingira salama ya kujifunzia

Mgeni rasmi Kaimu Katibu Mkuu – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ephreim Simbeye akizungumza wakati akifunga rasmi Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa (GAWE) 2026 yaliyofanyika Halmashauri ya Momba, mkoani Songwe.

Kila mwaka ifikapo Juni 16, nchi za Afrika huadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika kwa kutafakari maendeleo, changamoto na fursa zinazohusu ustawi wa mtoto. Mwaka 2026, maadhimisho hayo yanabeba kaulimbiu ya "Kuhakikisha kila mtoto barani Afrika anapata huduma za maji safi, usafi na mazingira salama ya kujisitiri (WASH)." Kaulimbiu hii inatukumbusha kuwa haki ya elimu haiwezi kutenganishwa na haki ya mtoto kupata maji safi, vyoo salama na mazingira yanayomwezesha kujifunza kwa afya na heshima.

Nchini Tanzania, siku hii imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuangazia mchango wa wadau mbalimbali katika kuboresha elimu, sekta ambayo ndiyo msingi wa maendeleo ya mtoto na taifa kwa ujumla. Miongoni mwa wadau hao ni Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), unaojumuisha wanachama zaidi ya 265 kutoka asasi za kiraia nchini na ambao kwa miaka mingi umeendelea kutetea elimu bora, jumuishi na inayomfikia kila mtoto bila ubaguzi.


Elimu jumuishi haiwezi kutenganishwa na miundombinu ya maji, vyoo na usafi wa mazingira (WASH)

Tafiti na mipango ya Serikali zinaonyesha kuwa mazingira bora, ikiwemomo miundombinu ya maji, vyoo na usafi wa mazingira shuleni yana mchango mkubwa katika kuongeza mahudhurio ya wanafunzi, kupunguza magonjwa na kuboresha matokeo ya ujifunzaji. Shule zenye huduma duni za WASH huathiri zaidi watoto wa kike, watoto wenye ulemavu na wanafunzi wa maeneo ya vijijini.

Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Maji Awamu ya Tatu (WSDP III), takribani asilimia 67 ya shule nchini zina huduma za msingi za maji ya kunywa, asilimia 88 zina huduma za usafi zilizoboreshwa, lakini ni asilimia 32 pekee zina vituo vinavyofanya kazi vya kunawia mikono na asilimia 12 tu zina vyoo vinavyoweza kutumiwa kwa urahisi na watoto wenye ulemavu. Aidha, ni karibu asilimia 28 tu ya shule zinazokidhi viwango vya kitaifa vya uwiano wa wanafunzi kwa tundu la choo. Hali hii inaonesha kuwa bado kuna safari ndefu kuelekea mazingira jumuishi na salama ya kujifunzia kwa kila mtoto licha ya hatua endelevu zilizopigwa.

Serikali kupitia WSDP III imeendelea kuongeza uwekezaji katika WASH shuleni kwa kulenga kuongeza upatikanaji wa maji, vyoo bora na vituo vya kunawia mikono katika maelfu ya shule za msingi na sekondari nchini, hatua inayochangia kupunguza utoro na kuongeza usalama wa watoto shuleni.


TEN/MET na uwekezaji katika mazingira bora ya kujifunzia

Mbali na utetezi wa sera na haki ya elimu, TEN/MET imeendelea kuwekeza katika miradi inayoboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto.

Wanafunzi wa shule mbalimbali wakiwa wakipita mbele ya mgeni rasmi wakibeba mabango yenye jumbe mbalimbali wakati wa Maadhimisho ya Juma la Elimu (GAWE) 2026, yaliyofanyika katika Halmashauri ya Momba, mkoani Songwe.

Katika Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa (GAWE) 2026 yaliyofanyika mkoani Songwe chini ya kaulimbiu ya "Ugemaji wa Rasilimali za Ndani kwa Elimu Jumuishi, Bora na Inayozingatia Mahitaji Maalum," TEN/MET ilitoa zaidi ya Shilingi milioni 53 kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za elimu katika shule za mkoa huo.

Fedha hizo zitasaidia kukamilisha ujenzi wa madarasa mawili na ofisi ya walimu katika Shule ya Msingi Maalum ya Ndalambo, kununua viti mwendo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, kukamilisha darasa katika Shule ya Msingi Chiwanda pamoja na kununua madawati katika Shule ya Msingi Msia.

Uwekezaji huu unaenda sambamba na dhamira ya kuhakikisha watoto wanajifunza katika mazingira yanayolinda afya, usalama na utu wao.


Maji na usafi shuleni ni kinga kwa mtoto wa kike

Moja ya changamoto kubwa inayowakabili watoto wa kike ni ukosefu wa huduma rafiki za maji,vyoo, vyumba vya kujisitiri na usafi wa mazingira, hususan wakati wa hedhi. Ukosefu wa vyoo salama, maji ya kutosha na sehemu za kujisitiri huchangia utoro na wakati mwingine kuacha shule kabisa.

TEN/MET inaamini kuwa shule jumuishi lazima ziwe na miundombinu ya WASH inayozingatia mahitaji ya watoto wote, wakiwemo watoto wenye ulemavu na wasichana wa rika balehe. Hili ni muhimu katika kuhakikisha hakuna mtoto anayekatishwa ndoto zake kutokana na changamoto zinazoweza kuzuilika.


Kulinda ndoto za mtoto kupitia mazingira salama

Mbali na changamoto za WASH, umbali mrefu kati ya makazi na shule unaendelea kuwa kikwazo kwa watoto wengi, hususan wasichana. TEN/MET imeendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine kuhimiza ujenzi wa mabweni na hosteli ili kupunguza safari ndefu, kuongeza usalama na kuboresha mahudhurio ya wanafunzi.

Juhudi hizi zinaendana na maono ya kuhakikisha kila mtoto, bila kujali eneo analoishi au hali yake, anapata nafasi sawa ya kupata elimu bora.


Kuandaa watoto kwa dunia ya kesho

Kadiri dunia inavyobadilika, elimu nayo inalazimika kuendana na mahitaji mapya ya soko la ajira. Kupitia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023), mkondo wa Amali unawajengea wanafunzi ujuzi wa vitendo unaowasaidia kujiajiri na kuajirika.

Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bi. Martha Makala akihutubia wadau wa elimu kwenye hafla ya kilele cha Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa (GAWE) 2026, yaliyofanyika kwenye Halmashauri ya Momba, mkoani Songwe.

TEN/MET imeendelea kufuatilia utekelezaji wa mkondo huo huku ikisisitiza kuwa mafanikio yake yanategemea pia uwepo wa mazingira bora ya kujifunzia yenye maji safi, usafi na afya bora kwa wanafunzi na walimu pampoja na vifaa vya kujifunzia.


Wito wa TEN/MET: Wekezeni katika WASH shuleni

Katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka huu, TEN/MET inatoa wito kwa Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa, sekta binafsi, washirika wa maendeleo na jamii kuongeza uwekezaji katika huduma za WASH shuleni kama sehemu ya utekelezaji wa haki ya msingi ya elimu kwa kila mtoto.

Mtandao huo unasisitiza kuwa:

  • Kila shule iwe na huduma endelevu ya maji safi na salama.
  • Kila shule iwe na vyoo vya kutosha, salama na vinavyozingatia mahitaji ya watoto wa kike na watoto wenye ulemavu.
  • Vituo vya kunawia mikono vyenye maji na sabuni viwe sehemu ya lazima katika shule zote.
  • Bajeti za elimu ziweke kipengele mahsusi cha WASH ili kuhakikisha miundombinu hiyo inajengwa na kutunzwa.
  • Ushirikishwaji wa jamii na kamati za shule uimarishwe ili kuhakikisha huduma za WASH zinadumu na zinatumika ipasavyo.


Kuendelea kuwekeza kwa mtoto

Siku ya Mtoto wa Afrika hutukumbusha kuwa jukumu la kumlea, kumlinda na kumwezesha mtoto si la Serikali pekee bali ni la jamii nzima. Elimu bora haiishii darasani; inahitaji pia maji safi, vyoo salama, mazingira rafiki ya kujisitiri na usafi wa mazingira unaolinda afya na utu wa mtoto.

Kutoka Ndalambo hadi Msangano, kutoka Songwe hadi maeneo mengine ya Tanzania, miradi inayoratibiwa na TEN/MET inaonesha kuwa pale jamii, Serikali na wadau wa maendeleo wanapounganisha nguvu zao, elimu jumuishi na bora inawezekana.

Katika maadhimisho haya ya Siku ya Mtoto wa Afrika 2026, ujumbe unabaki kuwa mmoja: hakuna elimu bora bila mazingira bora ya kujifunzia, na hakuna mtoto anayepaswa kubaki nyuma kwa sababu ya ukosefu wa maji safi, vyoo safi na salama na usafi wa mazingira ya shule. Kuwekeza katika WASH shuleni ni kuwekeza katika mustakabali wa Tanzania.