Zanzibar inavyopaa katika sekta ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo
Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Suleiman Masoud Makame.
Sekta ya kilimo imeendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa Zanzibar, ikichangia ajira kwa idadi kubwa ya wananchi pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa chakula ambapo takwimu zinaonyesha kuwa takribani asilimia 70 ya Wazanzibar wapo kwenye sekta ya kilimo huku sekta hiyo kikichangia takribani asilimia 30 ya Pato la Taifa.
Katika miaka ya hivi karibuni, juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeelekezwa zaidi katika kuimarisha kilimo cha umwagiliaji kama suluhisho la changamoto za mabadiliko ya tabianchi na uzalishaji usiotabirika.
Kupitia mikakati mbalimbali ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mageuzi makubwa yanaendelea kufanyika, yakilenga kuongeza tija, kipato cha wakulima na usalama wa chakula.
Aidha, Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika miundombinu ya umwagiliaji, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa skimu za umwagiliaji katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.
Hatua hiyo imewezesha wakulima kulima mwaka mzima badala ya kutegemea mvua pekee, hali iliyoongeza uzalishaji wa mazao muhimu kama mpunga, mboga mboga na matunda.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Mhe. Suleiman Masoud Makame ameeleza dhamira ya Serikali kuibadilisha sekta ya kilimo kuwa mhimili mkuu wa uchumi kupitia uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji, matumizi ya teknolojia za kisasa na uimarishaji wa mnyororo wa thamani wa mazao ya kimkakati.
Amesema sekta ya kilimo inaendelea kuimarika na kubeba matumaini mapya kwa wananchi, hususan wakulima wadogo na vijana, huku Serikali ikiweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha inakuwa na tija zaidi kiuchumi.
Waziri huyo amesema moja ya maeneo yaliyopewa kipaumbele ni maendeleo ya kilimo cha umwagiliaji ambacho kimeonekana kuwa suluhisho la changamoto ya mabadiliko ya tabianchi na upatikanaji wa mvua zisizotabirika.
“Kilimo cha umwagiliaji kinatupa uhakika wa uzalishaji mwaka mzima. Hii si tu inaongeza mavuno bali pia inawawezesha wakulima kuwa na kipato cha uhakika,” amesema Mhe Makame. Kwa mujibu wa Mhe Makame, maeneo mbalimbali ya Zanzibar yameanza kunufaika na miradi ya umwagiliaji, hasa yale yenye miundombinu rafiki ya upatikanaji wa maji.
Alitaja maeneo ya mabondeni na yale yaliyo karibu na vyanzo vya maji kuwa miongoni mwa yanayopata mafanikio makubwa kupitia kilimo hicho. Hata hivyo, alikiri kuwa bado kuna changamoto kadhaa zinazoikabili sekta ya kilimo, zikiwemo uhaba wa rasilimali, miundombinu duni ya umwagiliaji katika baadhi ya maeneo na uelewa mdogo wa wakulima kuhusu matumizi ya teknolojia za kisasa.
Katika kukabiliana na changamoto hizo, Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifungo imeweka mikakati ya kuwasaidia wakulima kupata teknolojia za kisasa za umwagiliaji, ikiwemo mifumo ya matone (drip irrigation) na matumizi ya pampu za kisasa zinazotumia nishati mbadala.
“Tunaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wakulima wanapata vifaa na elimu ya kutumia teknolojia hizi ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uzalishaji,” amesisitiza. Mbali na hilo, wizara imeweka mkazo katika mazao ya kimkakati ambayo yana mchango mkubwa katika uchumi wa Zanzibar.
Mazao hayo ni pamoja na yale ya chakula na biashara ambayo yana soko la uhakika ndani na nje ya nchi. Pia, kuna jitihada za kuimarisha huduma za ugani ili kuwafikia wakulima wengi zaidi na kuwapatia elimu kuhusu mbinu bora za kilimo cha umwagiliaji.
Kupitia huduma hizi, wakulima wanapatiwa maarifa kuhusu matumizi sahihi ya maji, uchaguzi wa mazao na mbinu za kukabiliana na changamoto za tabianchi ikiwemo matumizi ya mbolea bora na kuacha kutumia kemikali zisizo na lazima. Serikali pia inahamasisha uwekezaji wa sekta binafsi katika kilimo, hasa katika maeneo ya usindikaji wa mazao na masoko.
Hatua hii inalenga kuongeza thamani ya mazao na kuhakikisha wakulima wanapata bei nzuri kwa mazao yao. Katika juhudi za kuvutia vijana kuingia katika sekta ya kilimo, waziri huyo alisema serikali inaendesha kampeni za uhamasishaji na kutoa motisha mbalimbali, ikiwemo mafunzo, mikopo nafuu na upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya kilimo.
“Tunataka kubadili mtazamo wa vijana kuhusu kilimo. Kilimo si kazi ya mwisho bali ni biashara yenye fursa kubwa kama itafanywa kitaalamu,” alisema.
Aidha, alieleza kuwa Serikali ina mkakati wa kuvutia uwekezaji katika sekta ya kilimo kwa kuboresha mazingira ya biashara na kuweka sera rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Alisema uwekezaji huo utasaidia kuongeza thamani ya mazao kupitia uchakataji, uhifadhi na usafirishaji, hivyo kupunguza upotevu wa mazao na kuongeza mapato kwa wakulima.
Katika kuimarisha mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo, wizara inaangazia hatua zote kuanzia uzalishaji hadi masoko, ikiwemo kuboresha miundombinu ya uhifadhi, usindikaji na masoko ya mazao.
“Tunataka mkulima anufaike katika kila hatua ya uzalishaji. Hii ina maana ya kuongeza thamani ya mazao na kuhakikisha yanapata soko la uhakika,” alieleza.
Kwa upande wa fursa, Waziri amesisitiza kuwa Zanzibar ina nafasi kubwa ya kuendeleza kilimo kutokana na uwepo wa hali ya hewa inayoruhusu kilimo cha mazao mbalimbali kwa mwaka mzima.
Fursa nyingine ni pamoja na kuongezeka kwa mahitaji ya chakula kutokana na ukuaji wa sekta ya utalii, ambayo inahitaji bidhaa za kilimo kwa wingi na ubora wa hali ya juu.“Sekta ya utalii ni soko kubwa kwa wakulima wetu. Tunachohitaji ni kuhakikisha tunazalisha kwa wingi na ubora unaokidhi mahitaji ya hoteli na migahawa,” anasisitiza.
Kuhusu mipango ya baadaye, waziri huyo alisema ndani ya miaka mitano ijayo, serikali inalenga kuona sekta ya kilimo ikichangia kwa kiwango kikubwa zaidi katika pato la Taifa, huku ikitoa ajira kwa maelfu ya vijana.
Aliongeza kuwa maono hayo yatafikiwa kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya umwagiliaji, uboreshaji wa teknolojia za kilimo na ushirikiano wa karibu kati ya serikali na sekta binafsi.
Sekta ya kilimo Zanzibar inaendelea kupiga hatua kubwa, hasa kupitia maendeleo ya kilimo cha umwagiliaji. Ingawa changamoto bado zipo, juhudi za Serikali pamoja na ushirikiano wa wadau mbalimbali zinatoa matu-maini makubwa ya kufikia kilimo chenye tija na endelevu.
Kwa kuzingatia umuhimu wa sekta hii, ni wazi kuwa kuwekeza zaidi katika kilimo cha umwagiliaji si tu kutaimarisha usalama wa chakula, bali pia kutachangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa Zanzibar na ustawi wa wananchi wake.