Abdul Wakil Alivyokabili hoja ya Upemba na Uunguja

Muktasari:

  • Baada ya kutazama namna Rais wa Awamu ya Tatu, Ali Hassan Mwinyi alivyoingia madarakani na kuongoza Zanzibar akimteua Maalim Seif Sharrif Hamad kuwa Waziri Kiongozi na namna walivyoleta mageuzi ya kiuchumi pamoja na kuchochea ukuaji wa sekta binafsi, leo tutaanza kumuangalia Rais wa Awamu ya Nne, Idris Abdul Wakil.

Dodoma. Rais wa Awamu ya Nne, Idris Abdul Wakil baada ya kuingia madarakani kazi ya kwanza ilikuwa ni kuondoa tabaka lililoanza kujitokeza la Upemba na Uunguja kwa kumteua Maalim Seif Sharrif Hamad kuendelea na wadhifa wa Waziri Kiongozi.

Tabaka la Upemba na Uunguja lilijitokeza wakati wa mchujo ndani ya CCM wa kumteua mgombea urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1985, ambapo Wakil alimshinda Maalim Seif kwa kura 85 dhidi ya kura 78 alizopata Maalim Seif.

Maalim Seif, aliyeteuliwa kuwa Waziri Kiongozi na Rais Ali Hassan Mwinyi Februari 1984, alitarajia baada ya Mwinyi yeye ndiyo angesimamishwa na CCM kugombea urais wa Zanzibar.

Hata hivyo, Rais wa Awamu ya Nne, Wakil baada ya kuingia madarakani mwaka 1985, alimteua Maalim Seif kuendelea na wadhifa wa Waziri Kiongozi hadi Januari 1988 alipofanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na kumuondoa Maalim Seif kwenye nafasi hiyo.

Rais Wakil kwa moyo ule ule wa maridhiano kati ya Pemba na Unguja, alimteua Dk Omar Ali Juma kuwa Waziri Kiongozi, kuanzia Januari 1988 hadi 1995 alipoondoka madarakani. Dk Omar Ali Juma ni mzaliwa wa Chake Chake, kisiwani Pemba.

Kuondolewa kwa Maalim Seif kwenye wadhifa huo kulitokana na tuhuma za kukutwa na nyaraka za siri za Serikali, hivyo mbali na kuondolewa kwenye nafasi ya Waziri Kiongozi, pia alivuliwa nyadhifa zake zote ndani ya CCM.

Hali hiyo, ilimlazimu Rais Wakil kwenye uongozi wake kuanzisha misingi ya ujenzi wa umoja, upendo, mshikamano, furaha na amani kwa Wazanzibari wote wa Unguja na Pemba.

Pia, Rais Wakil hakuishia hapo, bali aliendeleza na kuimarisha yaliyofanywa na aliyemtangulia, Rais wa Awamu ya Tatu, Ali Hassan Mwinyi.

Rais Wakil aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar na ndiye aliyetangaza ushindi wa Aboud Jumbe Mwinyi kwenye uchaguzi wa kwanza uliowapa Wazanzibari haki ya kupiga kura wa mwaka 1980.

Uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 26, 1980, matokeo yaliyompa ushindi Jumbe yalitangazwa na Idris Abdul Wakil Oktoba 28, 1980 kwa wadhifa wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar.
 

Mageuzi ya kiuchumi

Pia, Rais Wakil kwenye uongozi wake alianzisha mageuzi ya sekta ya utalii kutoka mwelekeo wa kuimarisha urafiki, mashirikiano na maelewano na nchi za nje kwa kuiwekea sekta hiyo misingi ya kuendeleza Zanzibar kiuchumi.

Rais Wakil hakuishia hapo, alitangaza maeneo huru ya kiuchumi yaliyoko Fumba kwa Unguja na Micheweni kwa Pemba.
Alianzisha harakati za kutaka kuirejesha Zanzibar kuwa kituo muhimu cha biashara kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Rais Wakil pia aliweka misingi ya kuanzisha soko huria kwa kuwaruhusu watu binafsi kuendesha biashara ndani na nje ya nchi.
Aliweka misingi mizuri ya kuimarisha na kuendeleza michezo kwa kuunda Kamati ya Saidia Zanzibar Ishinde (SAZI).
 

Afananishwa na Mandela

Kuna wakati Jumuiya ya Umoja wa CCM (UVCCM), walimfananisha Rais Wakil na aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela aliyekaa madarakani kwa awamu moja pekee, kuanzia mwaka 1994 hadi mwaka 1999. Rais Wakil naye alikaa madarakani kwa awamu moja kuanzia Oktoba 24, 1985 hadi Oktoba 25, 1990.

Pia, ndiye kiongozi pekee aliyepongezwa na Mwalimu Nyerere kwenye mkutano mkuu wa CCM kwa kutokuwa na uchu wa madaraka licha ya Katiba kumruhusu kugombea kipindi kingine cha pili.

Mwalimu Nyerere alimwambia kama angegombea tena CCM ingempitisha na wananchi wangemchagua na kwamba amekuwa mfano wa viongozi wengine wanaougeuza urais ni ufalme.

"Je, ni wenzangu wangapi wamepata bahati yangu na wanang'ang'ania madaraka?" aliuliza Mwalimu Nyerere.

Alibainisha kuwa viongozi mashuhuri kama Kwame Nkrumah (Ghana), (Abubakar Tafawa), Balewa (waziri mkuu wa kwanza wa Nigeria) na Madibo Keita (Rais wa kwanza wa Mali) walipinduliwa hata kabla ya kupata muda wa kuongoza.

"Hakuna uhakika kwamba kama wangepewa nafasi ya kuongoza wangeng'ang'ania madarakani," alisema Mwalimu Nyerere.

Kwa upande wake Idris Abdul Wakil, aliueleza mkutano mkuu wa CCM kwamba uamuzi wake wa kustaafu alikuwa nao tangu mwaka 1989, lakini hakutaka kueleza mapema kwa hofu ya kushawishiwa aendelee kugombea.

Aliueleza mkutano huo kuwa alifikia uamuzi huo wa kustaafu tangu mwaka 1989, lakini hakutaka kutangaza mapema kwa sababu alihofia kushawishiwa kuibadilisha. "Hata hili nililificha kwa Mwenyekiti wa CCM," alisema Rais Wakil.
 

Kifo chake

Idris Abdul Wakil baada ya kustaafu aliishi maisha ya kawaida na alifariki dunia Machi 15, 2000 akiwa na umri wa miaka 75. Alizikwa kijijini kwao Makunduchi, Zanzibar.