Chama cha AAFP chaunga mkono maridhiano ya kisiasa Zanzibar
Mwenyekiti wa chama cha wakulima Taifa (AAFP), Said Soud Said akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mwera Unguja. Picha na Zuleikha Fatawi
Muktasari:
- Kauli hiyo inakuja wakati tamko la pamoja la maridhiano kati ya CCM na ACT-Wazalendo likitarajiwa kutolewa kesho, Julai 9, Ikulu Zanzibar, ambapo linatarajiwa kushuhudiwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, pamoja na Kiongozi wa ACT-Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman.
Unguja. Chama cha Wakulima Zanzibar (AAFP), kimesema kinaunga mkono maridhiano ya kisiasa kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo, kikieleza kuwa hatua hiyo inaweza kufungua ukurasa mpya wa utulivu na maendeleo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Julai 8, 2026, Mwenyekiti wa Taifa wa AAFP, Said Soud Said amesema maridhiano hayo yamekuja wakati ambao wananchi wengi walikuwa wakiyasubiri na yanaashiria dhamira ya kutanguliza masilahi ya Taifa.
Kauli hiyo inakuja wakati tamko la pamoja la maridhiano kati ya CCM na ACT-Wazalendo likitarajiwa kutolewa kesho, Julai 9, Ikulu Zanzibar, ambapo linatarajiwa kushuhudiwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, pamoja na Kiongozi wa ACT-Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman.
Said amesema viongozi wa vyama hivyo wanastahili pongezi kwa kufikia mwafaka unaolenga kuondoa migogoro ya kisiasa na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
"Maridhiano haya yanaonyesha mwanga wa maendeleo. Uamuzi huu umefikiwa kwa maslahi ya nchi, na huo ndiyo uzalendo wa kweli," amesema.
Amesema anaamini tamko hilo litakuwa hatua muhimu ya kuijenga Zanzibar yenye utulivu na mazingira bora ya maendeleo.
Aidha, amesema tofauti na mataifa mengine ambako migogoro ya kisiasa husuluhishwa kwa ushiriki wa wapatanishi kutoka nje, Zanzibar imeonyesha uwezo wa kutatua changamoto zake kupitia viongozi na wadau wa ndani.
"Hii ni mara nyingine kwa Wazanzibari wenyewe kusimamia maridhiano yao bila ushiriki wa wageni. Hilo linapaswa kupongezwa," amesema.
Kwa mujibu wa Said, hatua hiyo inaonyesha kukomaa kwa demokrasia nchini na inatoa fursa kwa viongozi kuendelea kujadili masuala muhimu, ikiwemo yale yanayohusu mfumo wa uongozi na utawala, kwa lengo la kuimarisha amani na kuzuia migogoro ya baadaye.
Amewataka wanasiasa na wananchi kwa ujumla kuyaunga mkono maridhiano hayo, kuheshimu makubaliano yatakayofikiwa na kuweka mbele masilahi ya Taifa badala ya tofauti za kisiasa.
Makamu Mwenyekiti wa AAFP, Omar Juma Said, amesema chama hicho kina matumaini kuwa tamko la pamoja litakuwa mwanzo wa hatua mpya za kuimarisha demokrasia, umoja na maendeleo Zanzibar.