Hisia mchanganyiko Polisi ikikanusha mtandao wa udhalilishaji

Muktasari:

  • Wakati Jeshi la Polisi Zanzibar likikanusha uwepo wa mtandao maalumu unaojihusha na matendo ya udhalilishaji, wadau mbalimbali visiwani hapa wamelitaka jeshi hilo kujitathmini upya.

Unguja. Licha ya matukio ya udhalilishaji Zanzibar kuongezeka, Jeshi la Polisi visiwani hapa limekanusha kuwepo kwa mtandao wa watu wanaojihusisha na matendo hayo.

Takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali zinaonyesha matukio ya udhalilishaji Zanzibar yameongezeka kutoka 157 yaliyotokea  Septemba,  2023 dhidi ya  199 yaliyotokea Oktoba.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 22, 2023 Kamanda wa jeshi hilo Mjini Magharibi, Richard Mchomvu amesema walipata taarifa kutoka kwa vijana wanaodaiwa kufanyiwa vitendo hiyo.

“Novemba 11, mwaka huu, tulipitia taarifa kutoka kwa vijana watatu wenye umri kati ya miaka 15-17 ambao walifanyiwa ukatili wa kijinsia, kupitia msako maalumu, tumewakamata watuhumiwa 13, huku majalada manne yameshafikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP.

 “Kati ya majadalada hayo, matatu yamepelekwa mahakamani leo na mengine matano yanaendelea na upelelelezi,”amesema Kamanda Mchomvu.

Amewataja watuhumiwa wanaoshikilikwa na jeshi hilo kuwa ni pamoja na Ibrahim Salehe (29), Abrahman Saleh Rashid (22), Ali Abdalla Mohamed (27), Yassin Abdalla (17), na Twalib Salum Mohamed (25).

Wengine ni Suleiman Juma Omar (22), Othman Mohamed (49), Ali Haji Khamis (25), Mudathir Jacob Simon (27), Ali Salum Abdalla (53) na Mohamed Fuad (21).

Baada ya  jeshi hilo kukanusha  kuhusiana na uwepo wa mtandao huo, wananchi mbalimbali visiwani hapa wamekua na maoni tofauti juu ya taarifa hiyo, huku wakisema jeshi hilo linapaswa kufuatilia kwa umakini zaidi.

Abdalla Suedi mkazi wa Jangombe visiwani hapa amesema: “Ni jambo ambalo haliwezi kuingia akilini watoto watatu kufanyiwa ukatili na watu 13, bila ya wengine miongoni mwao kufanyiwa ukatili huko na watu wawili au watatu tofauti,”amesema.

Amesema inawezekana jeshi pamoja na kazi kubwa iliyofanya kuwakamata watu wanaodaiwa kuhusika, lakini pia kuna kitu hawajakitambua au wanataka kuficha ukweli.

‘’Hii haingii akilini kabisa watu 13 wafanyie ukatili watoto watatu halafu useme huu sio mtandao hili haliwezekani,  tukubali tatizo lipo kisha watu watafute njia,’’ amesema na kushauri Sued.

Kwa masharti ya kutotajwa jina mama mmoja wa makamo visiwani hapa ameiambia Mwananchi Digital kuwa tatizo la ulawiti kwa watoto wa kiume lipo na linaongezeka kadri siku zinavyozidi kusonga.

“Mtaani ninapoishi, kuna kesi nyingi za watoto kufanyiwa ukatili huo tena na watu zaidi ya moja...hii inamaanisha ni mtandao ambao watu wanakubaliana kufanya jambo fulani kwa pamoja,” amesema mama huyo.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Shirika la Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu Zanzibar (Zalho), Harusi Mpatani amesema taarifa ya jeshi hilo inaibua maswali mengi na kuacha mshangao katika jamii.

Amesema ikiwa watoto waliofanyiwa ukatili huo ni watatu na waliokamatwa ni 13 ni wazi kulikua na muunganiko wa wafanyaji wa matendo hayo na ndio maana kukaibuka dhana nzima ya kuwa huo ni mtandao wa watu wanaojuana.

Amesema inawezekana baadhi ya watu kwenye jamii zetu hawafahamu kuwa mtandao unaweza kuwepo bila ya kusajiliwa, hususani mitandao inayofanya kazi zisizokua rasmi kama hizo za ukatilili wa kijinsia.

‘’Hakuna maana kukataa kila jambo tunapotaka kujenga jamii bora yenye kuheshimu haki ya kila raia kwenye Taifa letu lazima tukubali ukweli huu ni mtandao na unahitaji kufanyiwa kazi zaidi kusambaratishwa,’’ ameongeza.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi Mtendaji wa jumuiya inayojihusisha na changamoto zinazowakabili vijana Zanzibar (Zafayco), Abdalla Abedi amesema baadhi ya vijana wanaojihusisha na matendo hayo, wamekosa elimu sahihi ya mfumo wa maisha bora na ulinzi kwa wengine.

Ameshauri wadau na Serikali kwa pamoja kuunganisha nguvu katika mapambano hayo ikiwemo kutoa elimu kwa wahusika katika maeneo mbalimbali na hata kuingizwa kwenye mitaala ya shule ili kila mtoto aweze kujisomea.