Jamii yahamasishwa ushiriki Mwenge wa Uhuru

Muktasari:

  •  Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuwasili Zanzibar Mei 13, 2024 na kukimbizwa katika mikoa na wilaya zote za Unguja na Pemba

Unguja. Viongozi, wafanyakazi, wananchi, vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na  wafanyabiashara wameombwa kushiriki mapokezi ya Mwenge wa Uhuru mwaka 2024.

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita ametoa ombi hilo jana Mei 10, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mapokezi ya Mwenge wa Uhuru Zanzibar.

Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuwasili Zanzibar Mei 13, 2024 na kukimbizwa katika mikoa na wilaya zote za Unguja na Pemba.

Hata hivyo, hakutaja miradi itakayotembelewa akieleza itatajwa wakati wa kuhitimisha mbio hizo.

“Mbio hizo zinaelimisha na kuhamasisha jamii ya Watanzania kuhusu kuzingatia lishe bora, mapambano dhidi ya rushwa, mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi, dawa za kulevya na ugonjwa wa malaria,” amesema.

Amesema ujumbe wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu unalenga kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa amani na utulivu.

Pia, kuendelea kushiriki kikamilifu katika harakati za kuhifadhi mazingira kwa ujenzi wa Taifa.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar, Shaibu Moh’d Ibrahim amesema maandalizi ya mbio hizo yamekamilika na miradi ya vijana, afya na wajasiriamali inatarajiwa kuzinduliwa katika mbio hizo.

Amesema Mwenge wa Uhuru upo kwa watu wote na hauna ubaguzi wa rangi, siasa, dini wala kabila, hivyo ni vyema wananchi hususani vijana kujitokeza ili kufanikisha mbio hizo.

Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2024, zimezinduliwa Aprili 2, 2024 katika Kiwanja cha Chuo cha Ushirika Moshi mkoani Kilimanjaro.

Ujumbe wa mbio mwaka huu ni uhifadhi wa mazingira na uchaguzi wa Serikali za Mitaa chini ya kaulimbiu isemayo, ‘Tunza mazingira na shiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ujenzi wa Taifa endelevu.’