Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kauli za kukemea ubaguzi zatikisa Bunge, Baraza la Wawakilishi

Mwakilishi nafasi za Wanawake, Dk Nasra Nassor Omar (ACT Wazalendo) akichangia mjadala wa bajeti kuu ya serikali barazani Chukwani Unguja Zanzibar

Dar/Zanzibar. Mjadala wa kurushiana vijembe kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar umeibuka baina ya wabunge na wawakilishi hali ambayo imekemewa na baadhi yao kuwa inaweza kuhatarisha Muungano na mshikamano wa kitaifa.

Wakichangia mjadala wa bajeti, baadhi ya wabunge wameonya kauli zinazotolewa na baadhi ya mawaziri upande wa Zanzibar, kuwa  ni za hatari, zinawagawa wananchi na zinaweza kuhatarisha Muungano. Kutokana na hali hiyo, wamemtaka Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, kuzikemea kauli zilizotolewa na mawaziri wake.

Kwa upande wa Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamesisitiza kuwa wataendelea kutetea masilahi ya Zanzibar ndani ya Muungano, licha ya baadhi ya kauli zao kutafsiriwa kama za kibaguzi.

Hoja hizo zimeibuka kufuatia kauli zilizotolewa nyakati tofauti na mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ambazo zimetafsiriwa kuwa ni za kibaguzi dhidi ya wananchi wasiokuwa Wazanzibar.

Juni 6, 2026, akizungumza kwenye Baraza la Wawakilishi, Kaimu Waziri wa Afya Zanzibar, Dk Saada Mkuya Salum, alinukuliwa akihoji mwenendo wa watu wasiokuwa Wazanzibar kwenda kutibiwa visiwani humo kupitia Matibabu Kadi, ambayo ni maalumu kwa Wazanzibari pekee.

Alisisitiza kuwa bajeti ya Zanzibar ni Sh8 trilioni pekee, hivyo haiwezi kubeba gharama za matibabu kwa watu milioni 60.

Kauli hiyo iliibua mjadala mpana, hasa kwa wananchi wa Tanzania Bara walioipokea kama ya kibaguzi.

Hata hivyo, akifafanua kauli yake katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni, Mkuya alisema bajeti ya Zanzibar haiwezi kubeba gharama za watu wengi, na Serikali imeweka mifumo inayowezesha watu wengine kuchangia ili kuboresha huduma za afya visiwani humo, huku baadhi ya wananchi kutoka Bara wakitumia bima zao za afya.

Aliongeza kuwa Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) unatoa huduma kwa mwanachama yeyote, wakiwamo wa kutoka Tanzania Bara.

Vilevile, Naibu Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Hassan Hamis Hafidh maarufu kama Diaspora, wakati akichangia hotuba ya bajeti ya wizara yake, alisema Zanzibar ina hoteli 1,184 zilizosajiliwa, lakini wafanyakazi wengi katika hoteli hizo si wazawa.

Mwakilishi wa Ziwani, Mohamed Ali Salim (ACT Wazalendo) akichangia mjadala wa bajeti kuu barazani Chukwani Unguja Zanzibar.

Alisema jukumu la wizara yake ni kuhakikisha kwamba Wazanzibari wanapata nafasi kubwa zaidi za ajira katika sekta hiyo. Kauli hiyo pia ilizua mjadala, huku baadhi ya watu wakiitafsiri kuwa ni ya kibaguzi dhidi ya wasiokuwa Wazanzibari.

Aliongeza kuwa alitembelea hoteli moja yenye wafanyakazi 156, ambapo Wazanzibari walikuwa 27 pekee. Alisema lengo ni kuhakikisha idadi kubwa ya wafanyakazi katika hoteli hizo wanakuwa Wazanzibari, huku nafasi chache zikichukuliwa na wasiokuwa wazawa.

Akifafanua kauli yake, Diaspora alisema alikuwa akijibu hoja za wajumbe waliokuwa wakihoji kwa nini ajira nyingi katika sekta ya utalii haziwanufaishi wazawa.

Alisema hali hiyo imechangiwa na mtazamo uliopo miongoni mwa baadhi ya vijana kwamba ajira za Serikali ndizo zenye manufaa zaidi.

Amesema vijana wengi wanaamini kuwa wakifanya kazi katika sekta binafsi hukosa uhuru wanaoupata katika ajira za Serikali.

Hivyo, alisema jukumu la wizara yake ni kubadilisha mtazamo huo ili vijana wa Zanzibar watumie fursa zilizopo katika sekta binafsi ambazo kwa sasa zinachukuliwa na wengine.


Wabunge waonya

Kauli hizo ndizo zimemwibua Mbunge wa Geita Vijijini Joseph Kasheku (Musukuma) akimtaka Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kukemea alichokiita ubaguzi wenye hatari kwa Muungano, ambao unatolewa na mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Musukuma ametoa kauli hiyo leo Jumanne Juni 16, 2026 wakati akichangia mjadala wa Bajeti ya Serikali, akisema kauli za kibaguzi zikitolewa na mawaziri zinaonekana ni kauli za Serikali hivyo akashauri mawaziri kuchunga kauli zao.

Amesema Muungano wa sasa si ule wa zamani wa kuchanganya udongo uliofanywa na waasisi Hayati Julius Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume, bali kwa sasa umekuwa ni muungano wa damu.

“Sisi kule Geita, robo tatu ya wachimbaji ni watu kutoka Zanzibar, tunawatibu na kuwalisha lakini hatujawahi kuwaambia maneno hayo, kama ni suala la sato, sijui sangara, basi nao walete kwerekwere ziboreshwe,” amesema na kuongeza:

“Mimi ni mjumbe wa NEC (Halmashauri Kuu ya Taifa na CCM), nachaguliwa Zanzibar na Tanzania Bara, sisi tumekuta maneno haya; muungano, muungano. Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar walichanganya udongo, sisi tumeenda mbali na kuchanganya damu, niwaombe wenzetu wanapochangia wazungumze mambo ya Tanzania, ni vizuri mawaziri mkachunga kauli zenu,” amesema Musukuma huku wabunge wakimshangilia.

Kwa upande wake, Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara amesema wanaopinga Muungano ulioasisiwa na waasisi ni wale waliokula, wakashiba na kuvimbiwa, ambao hawapaswi kuvumiliwa kwa namna yoyote.

“Tutaulinda Muungano wetu kwa nguvu zote, tutamlinda mama Samia (Rais Samia Suluhu Hassan) kwa wivu mkubwa na hakuna mtu anayeweza kuuharibu wala kuuvuruga Muungano wetu na kama ametumwa mtu kufanya hivyo hataweza,” amesema Waitara.

Mbunge huyo amesema hoja na chokochoko za kuvuruga Muungano hazipaswi kukubaliwa kwa namna yoyote, isipokuwa watu wa aina hiyo ambao amesema wapo hata kwa upande wa Tanzania Bara, wanapaswa kupuuzwa.

Waitara ambaye alishawahi kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, amesema kabla ya mambo yote ni lazima anayeitwa “Yuda” kama alivyodai mbunge kutoka Zanzibar, Simai Mohammed Said, aatajwe hadharani.

“Watu wanalewa maneno kana kwamba wamekula wakashiba na kuvimbiwa, lakini zipo kauli zinaleta ubaguzi na mimi nasema huenda wametumwa hao ambao tunapaswa kuwalaani, kama mtu anasema kuna Yuda humu ndani, je huyo Yuda ni nani, lazima atajwe vinginevyo hatutakubali maneno ya kibaguzi,” alisema Waitara.

Amesema wabunge hawawezi kuonekana watu wa hovyohovyo kwenye mambo ambayo yanakera sana kwa watu waliokwenda shule na kujifunza.

Amewataka waliowatuma kuacha mara moja kwa kuwa hawataweza.


Wawakilishi watetea

Wakati huohuo, baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamesema wataendelea kutetea masilahi ya Zanzibar ndani ya Muungano, licha ya kwamba wakati mwingine huonekana kama yanayosemwa ni ya kibaguzi.

Wakichangia wakati wa mjadala wa bajeti kuu leo Juni 16, 2026, wawakilishi hao wamesema ikiwa itaonekana wanatetea masilahi ya Wazanzibari ni ubaguzi basi hakuna haja ya kuendela na muungano huo.

Mwakilishi wa Ziwani, Mohamed Ali Salim (ACT Wazalendo) amesema: “Hata ajira chache zilizopo zinakamatwa na wenzetu wa upande wa pili, ingawa tukisema inakuwa ni nongwa kwamba eti tunapinga Muungano, lakini kama ni kuwatetea vijana wetu kupata ajira tunahatarisha muungano, basi na uvunjike.”

“Mie kama mwakilishi wa Ziwani ninaendelea kutetea na kuwaombea vijana na kama hii ndio sababu ya kuvunjika muungano wacha uvunjike kwa kuwa ajira ninazoziomba ni halali kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ingawa tafsiri zinakuja tofauti,” amesema.

Naye, Mwakilishi wa Viti Maalumu (CCM), Chumu Kombo Khamis amesema muungano hautavunjika utaendela kulindwa kwa nguvu zote kwa sababu tayari kuna mwingiliano wa kudugu baina ya pande zote mbili.

“Muungano utalindwa, haufi kwa sababu kuna ndugu zetu wapo huko na wa Tanganyika wapo huku Kahama, Sumbawanga na wanaendelea na maisha yao kama kawaida,” amesema.

Naye Mwakilishi nafasi za wanawake, Dk Nasra Nassor Omar (ACT Wazalendo) amesema kumekuwa kukijitokeza masuala mengi, hususan ajira za Zanzibar zikipigiwa kelele lakini ni uhalisia kwamba ajira zinachukuliwa na wengine, hivyo wanapaswa walizungumze bila kuogopa.

Amesema bajeti hiyo ina matundu kwani haiakisi hadhi ya Zanzibar katika Muungano na ya kikatiba kwani haitakiwi kuwa ni suala la kinamba bali liwe la kisiasa, kiuchumi na kijamii.

“Bado bajeti hii ina matundu mengi ambayo yanafanya kila siku turudi kuyazungumza lakini msingi wenyewe ni kuhakikisha bajeti hii inawagusa wananchi, kwa sababu ya muundo wa muungano na katiba unafanya mambo mengi yapalekwe juu badala ya chini,” amesema.

Amesema kwa kipindi cha miaka minne ya bajeti, Zanzibar haina uwezo kwenye hadhi ya muungano kwani uchumi wake haujaangalia namna gani itaweza kujiendesha yenyewe bila kutegemea muungano.


Hoja ya Matibabu Kadi

Akizungumza kuhusu hoja iliyoibuka karibuni kuhusu matibabu ya bima kwa Wazanzibari, Dk Nasra amesema kuibuka hoja hizo ndiyo ustawi wa jamii.

Amesema hoja ya kwamba wanaotoa vitambulisho vya Mzanzibari mkazi ni masheha haina mshiko kwani zipo taarifa tangu mapema, ulitengenezwa mkakati wa kutoa vitambulisho hivyo kwa wageni ili kuwasaidia katika masuala ya kura.

Mwakilishi huyo amesema upatikanaji wa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (ZAN ID) ulifanyika kisiasa.

“Watu walidhani unapokosa ZAN ID utashindwa wewe kupiga kura tu, lakini uliowapa kwa ajili ya kupigakura ndio hao wanakusakama. Wanataka Matibabu Kadi, kwa hiyo hilo sio kosa la mtu aliyetoka nje ya Zanzibar kuja kupata matibabu, kama ulimtumia kipindi cha uchaguzi, usije hapa ukalalamika kwamba matibabu kadi haitolewi kwa njia isiyo sahihi,” amesema.