Kujenga viwanda, kutafuta masoko vipaumbele wizara ya biashara

Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na Matumizi ya mwaka 2024/25 ya wizara yake katika Baraza la Wawakilishi Chukwani Juni 8, 2024. Picha BLW

Muktasari:

  • Kipaumbele ni miundombinu ya viwanda, masoko, ujenzi wa kituo cha mikutano, na kuboresha udhibiti wa bidhaa na huduma.

Unguja. Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, imepanga kutekeleza vipaumbele katika maeneo makuu matatu kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Maeneo hayo yanalenga kuimarisha sekta ya viwanda, biashara na kutafuta masoko pamoja na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na utoaji huduma.

 Hayo yamesemwa jana Jumamosi Juni 8, 2024 na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaaban alipowasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara hiyo katika Baraza la Wawakilishi, Chukwani, Zanzibar huku akiliomba baraza hilo liidhinishe Sh60.28 bilioni.

Kati ya fedha hizo, amesema Sh1.68 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kazi za kawaida na Sh3.13 bilioni ni za mishahara, huku Sh50.32 bilioni zimetengwa kwa kazi za maendeleo. Wizara imepangiwa ruzuku ya Sh5.15 bilioni.


Sekta ya viwanda

Waziri Shaaban amesema katika kuyaendeleza maeneo ya viwanda Dunga, Chamanangwe na Pangatupu, wizara inatarajia kuweka miundombinu ya majengo ya viwanda, maji, umeme pamoja na barabara za ndani.

Pia imepanga kufanya upimaji wa udongo na kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi na kuanzisha mfumo wa usajili wa takwimu za viwanda.

“Mfumo huo utatumika kukusanya takwimu na kutoa ripoti zinazohusiana na mwenendo mzima wa viwanda kwa upande wa Zanzibar na utajumuisha kwa pamoja na mfumo wa BPRA na Brela,” amesema.

Akizungumzia uimarishaji wa biashara na masoko, amesema wizara imepanga kuendeleza ujenzi katika eneo la maonyesho ya biashara Dimani sambamba na kuweka miundombinu ya maji ya uhakika katika eneo lote, kufunga kamera za CCTV na scanner, ununuzi wa vifaa na kuweka mifumo ya usajili wa washiriki.

Pamoja na hayo, itaratibu ujenzi wa kituo cha kimataifa cha mikutano na kutafuta wawekezaji wenye masharti nafuu, ili kushirikiana katika ujenzi wa kituo hicho.

Ili kuboresha mazingira, wizara hiyo itafanya ukaguzi na uchunguzi wa bidhaa, bei elekezi ya bidhaa na bidhaa bandia na kuweka mikakati kwa watumiaji pamoja na kusikiliza mashauri ya kumlinda mtumiaji.

Mambo mengine itakayofanya ni utafiti wa athari za kijamii na kiuchumi zinazotokana na matumizi ya bidhaa bandia na kupitia na kupendekeza marekebisho ya sheria 20 za mamlaka za utoaji leseni Zanzibar.

Pia wizara imepanga kuimarisha taasisi kupata ithibati ya maabara mbili ya chakula na ya umeme na kuimarisha huduma za udhibiti ubora ndani ya taasisi kwa upande wa Pemba ambako itajengwa ofisi na maabara.


Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC)

Shirika hilo linatarajia kuanzisha viwanda viwili vipya vya uzalishaji wa mafuta ya mimea vyenye uwezo wa kuchukua kilo 350 za majani kwa wakati mmoja ambazo zitakuwa na uwezo wa kuzalisha wastani wa lita sita za mafuta.

Kadhalika, litazalisha vifungashio vya bidhaa mbalimbali hasa bidhaa za karafuu na mazao mengine ya kilimo.

ZSTC inategemea kununua tani 5,000 za karafuu katika mwaka wa fedha 2024/25. Kuanzia Julai 2023 hadi Machi, 2024 shirika hilo limenunua tani 3,298.8 za karafuu kavu kwa Sh47.5 bilioni.

Akisoma maoni ya kamati, Makamu Mwenyekiti, Kamati ya Utalii, Biashara na Kilimo, Hussein Ibrahim Makungu amesema ili kuhakikisha mafanikio makubwa yanapatikana ndani ya shirika hilo, wizara inapanga mikakati ya kuliboresha kwa kukaa na wadau wote wa karafuu na kutatua changamoto zinazolirudisha nyuma shirika.